SALA YA USIKU
JUMATATU
(Kabla ya kulala)
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya
Kuchunguza dhambi:
K. Tuwaze katika moyo makosa tuliyomkosea Mungu, kwa mawazo kwa
maneno, kwa matendo na kwa kutotimiza wajibu: (kimya kifupi)
W. Namwungamia Mungu mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno,
kwa matendo, na kwa kutotimiza wajibu: nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana.
Ndiyo maana namwomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote,
nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.
K. Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele.
W. Amina
TENZI chagua 1-8
AU
1
Kristo mwanga wetu wa kweli,
Kristo asubuhi ya kweli,
Mwondoaji vya usiku vivuli,
Mwanga unaozaa kila mwanga,
Amana ya nuru ya heri, Bwana:
Uwe mlinzi wetu usiku kucha
Wewe ulindaye bila kulala
Uwe amani yetu, Ee Bwana,
Ili gizani tuwapo na Wewe,
Tuweze kupumzika kwa raha.
Macho yetu usingizi yapige,
Lakini moyo kamwe usilale,
Moyo uloelekezwa mbinguni;
Na twaomba salama uwalinde
Watumishi wanaokutamani.
Ututazame, Bwana, tutazame,
Nao maadui wetu na wako
Mbali nasi, Bwana, wafukuzie;
Maovuni waopoe wa'mini
Ulowakomboa kwa damu yako.
Wakati roho ingali mwilini,
Utulinde mwili na roho, Bwana,
Tuwe salama katika uvuli
Uvuli wa mabawa yako, Bwana,
Daima tulindwe kwa kinga yako.
AU
2
Wakati huu ni jioni
Muda wa kumaliza kazi;
Kadiri ya mapenzi yako,
Na utavyoridhika Baba,
Kipindi chote cha usiku
Watu wako waaminifu
Bwana utuweke salama.
Uyafukuze mashetani
Na zetu nyumba yawe mbali;
Tulinde katika uvuli
Ulo chini ya mbawa zako;
Uwe pia mlinzi wetu
Wakati wote wa usiku,
Utusimamie imara.
Na kabla hatujalala
Jina la Yesu twalitaja;
Tayari kukutumikia
Tuamkapo asubuhi;
Matendo yetu uyapange
Yaanze na yaishe vema,
Yote kwa utukufu wako.
Ewe chemchemi ya wema
Uwabariki wenye dhiki,
Mateka uwatembelee
Wafariji wanoteseka,
Uwahifadhi na wageni,
Lisha watoto wenye njaa,
Imarisha wanaokufa.
Ee Baba, usosinzia
Wewe kamwe usiyelala,
Kwako giza li mwanga 'tupu
Li angavu kama mchana,
Kwa mastahili ya Yesu
Twakuomba usiku huu
Sisi utuweke salama.
P. Herbert +1571
AU
3
Uniongoze, Mwanga mtulivu,
Katikati ya hili giza nene,
Niongoze mbele;
Usiku huu umejaa giza,
Na mimi nipo mbali na nyumbani,
Niongoze mbele;
Tia nguvu hii yangu miguu;
Siombi nione mbali upeo;
Hatua moja mbele yanitosha.
Kamwe na sijapata kuwa hivi
Na wala sijapata kukuomba
Uniongoze mbele;
Daima nilipenda kuchagua
Na kuona njia - lakini sasa
Niongoze mbele.
Nilipenda siku inayong'ara
Nikatawaliwa na majivuno:
Usikumbuke miaka ya nyuma.
Umenineemesha hadi sasa,
Na bila shaka utaendelea
Kuniongoza mbele
Katika nyika, mbuga na miamba,
Na kwenye mabubujiko - mpaka
Usiku upite!
Asubuhi nione za tabasamu
Nyuso za malaika nizipendazo,
Nilizozipoteza kwa kitambao.
J.H. Newman 1801-1890
AU
4
Yaja kwa kasi jioni,
Ukae pamoja nami;
Giza linaongezeka,
Sina wa kunifariji
Ukae Bwana na mimi;
U Auni kwa dhaifu,
Na uwe pamoja nami.
Yamesha fika mwishoni,
Maisha sasa yaisha,
Raha za dunia basi;
Zakoma fahari zake;
Yamegeuka uwozo,
Yote ninayoyaona;
Ee usobadilika
Ukae pamoja nami.
Nyosha wako msalaba
Kwa yangu macho, yafumba!
Nimulikie gizani,
Nielekeze angani;
Kunakucha uwinguni,
Vivuli hakuna chini;
Katika maisha, kifo,
Ee Bwana, uwe nami.
H.F.Lyte 1793-1847
AU
5
Siku ulotupa, Bwana, imesha.
Kwa neno lako giza huingia;
Asubuhi na tulikuimbia,
Hizo sifa kwako zilizopaa,
Pumziko letu tatakatifuza.
Kanisa lako li macho, asante,
Dunia izungukapo usiku,
Lakesha macho duniani kote,
Lipo macho mchana na usiku;
Kanisa halipumziki kamwe.
Kama ilivyo bara, visiwani
Mapambazuko hukarisha
Siku nyingine kila asubuhi,
Na masifu yetu hayafifii.
Jua linaloamuru tulale
Ndilo linalowaamsha pia
Ndugu zetu walio magharibi;
Hivi kuna midomo kila saa
Itangazayo yako maajabu.
Amina, enziyo haitapita
Kama tawala zinazojivuna;
Ufalme wako upo imara
Nao milele waenea, Bwana,
Hata viumbe vyote vikukiri.
J. Ellerton 1826-1893
AU
6
Sote twamshukuru Mungu wetu,
Kwa mioyo, mikono na sauti,
Kafanya maajabu Yeye huyo,
Vyake viumbe vinashangilia;
Tangu mwa mama zetu mikononi
Za kwetu njia kazibarikia
Tuna vipawa vya upendo tele,
Hata leo bado ni Mungu wetu.
Uwe karibu Mungu Mkarimu
Kwa siku zote za maisha yetu,
Mioyo yetu iwe mikunjufu
Kwa amani yako tuchangamshwe;
Katika neema yako tuweke,
Mashakani njia utuoneshe,
Utuepushe na maovu yote
Ya ulimwengu huu na ujao.
Sifa na shukrani kwako Mungu
Kwako Baba sasa na zitolewe,
Kwa Mwana, na kwa anayetawala
Pamoja na ninyi juu mbinguni,
Ewe Mungu Mmoja wa milele
Mbingu na dunia zakuabudu;
Vile ilivyokuwa ndo ilivyo,
Na hivyo itakuwa kwa milele.
M. Rinkart 1586-1649
AU
7
Bwana wa matumaini yote,
Ee Bwana wa furaha yote,
Hapana shughuli iwezayo
Kuharibu tumaini kwako;
Uwe nasi tunapoamka,
Na utujalie, twakuomba,
Furahayo mwetu mioyoni
Utujaze kila asubuhi.
Ewe Bwana wa juhudi yote,
Ewe Bwana wa imani yote,
Mikono yako yenye ufundi
Ilifanya sawa kila kazi;
Uwe na sisi kazini Bwana,
Na utujalie, twakuomba,
Nguvu yako mwetu mioyoni
Bwana, ua liwapo kichwani.
Ewe Bwana na wa wema wote
Ewe bwana wa neema zote,
U mwepesi wa kukaribisha,
U mwepesi wa kukumbatia;
Uwe nasi twendapo nyumbani,
Na utujalie, twakuomba,
Pendo lako mwetu mioyoni
Jua linapozama jioni.
Ewe Bwana wa upole wote,
Na Bwana wa utulivu wote,
Sauti yako inaridhisha,
Uwepo wako huburudisha;
Uwe na sisi tunapolala,
Na utujalie, twakuomba,
Amani yako mwetu nyoyoni
Mwisho wa siku, Bwana mwamini.
Jan Struther 1901-1953
AU
8
Tubariki pote, Mwokozi mwema,
Yetu akili neno lako ipe,
Washa mioyo yetu vuguvugu
Ipe pendo na utashi imara.
Tuwapo hai na tukisha kufa
Tuongoze, Ee Yesu mpole.
Siku imekwisha, saa 'mekwenda,
Na mambo yote wewe wayajua:
Neema imeshinda kidogo tu,
Makosa na kushindwa ni daima.
Tuwapo hai na tukisha kufa
Tuongoze, Ee Yesu mpole.
Na twawaombea wapenzi wote:
Maskini, wakosefu, wanyonge,
Kwa huruma yako tufurahishe;
Ndiwe Yesu wetu na yetu yote.
Tuwapo hai na tukisha kufa
Tuongoze, Ee Yesu mpole.
F. W. Faber 1814-1863
Ant. Wewe, Bwana Mungu, si mwepesi wa hasira; u mwingi wa fadhili.
Zab.86 Kuomba msaada
Atukuzwe Mungu... Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote (2Kor.1:3-4)
Unisikilize, Ee Mungu, unitegee sikio,*
maana mimi ni fukara na mnyonge.
Uilinde roho yangu, maana mimi ni mchaji wako;*
uniokoe mimi mtumishi wako, ninayekutegemea.
Wewe ni Mungu wangu; basi, unionee huruma.*
Mimi ninakulilia mchana kutwa.
Unifurahishe mimi mtumishi wako, Ee Mungu,*
maana sala zangu nazielekeza kwako.
Wewe, Ee Bwana, u mwema na mwenye huruma;*
umejaa upendo mkuu kwa wote wanaokuomba.
Usikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uangalie kilio cha ombi langu.
Siku za taabu nakuita,*
maana wewe wanisikiliza.
Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe;*
hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe.
Mataifa yote uliyoyaumba yatakuja na kukuabudu;*
yatatangaza ukuu wa jina lako.
Unifundishe, Ee Mungu, mwongozo wako,/
nami nitaufuata kwa uaminifu;*
uongoze moyo wangu nikuheshimu.
Nitakusifu, Ee Bwana, Mungu wangu, kwa moyo wote;*
nitatangaza ukuu wa jina lako hata milele.
Upendo wako ni mkuu mno!*
Umeniokoa kutoka chini kuzimu.
Ee Mungu, wenye kiburi wamenikabili;/
kundi la watu wakatili wanataka kuniua,*
watu ambao hawakujali wewe hata kidogo.
Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa huruma na mapendo;*
wewe ni mvumilivu, mpole na mwaminifu.
Unigeukie, unihurumie;/
unijalie nguvu yako, unisalimishe,*
mimi niliye mtumishi wako kama mama yangu.
Unioneshe ishara ya wema wako, Ee Mungu,/
ili wale wanaonichukia waaibike,*
wakiona wewe umenisaidia na kunifariji.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Wewe, Bwana Mungu, si mwepesi wa hasira; u mwingi wa fadhili.
SOMO: 1Tes.5:9-10
Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana
wetu Yesu Kristo, ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au
tumekufa.
KIITIKIZANO
K. Mikononi mwako, Ee Bwana, naiweka roho yangu. (W. Warudie)
K. Umetukomboa, Bwana Mungu wa kweli.
W. Mikononi mwako, naiweka roho yangu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mikononi...
Ant. Utuokoe, Ee Bwana, wakati tukiwa macho; utulinde tukiwa usingizini;
ili tukeshe pamoja na Kristo, na tupumzike naye kwa amani.
WIMBO wa Simeoni: Lk.2:29-32
Kristo ni nuru ya mataifa, na utukufu wa Israeli
Sasa, Bwana, umetimiza ahadi yako,/
waweza kumruhusu mtumishi wako,*
aende kwa amani.
Maana kwa macho yangu /
nimeuona wokovu utokao kwako,*
ambao umeutayarisha mbele ya watu wote:
Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa,*
na utukufu kwa watu wako Israeli.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Utuokoe, Ee Bwana, wakati tukiwa macho; utulinde tukiwa usingizini;
ili tukeshe pamoja na Kristo, na tupumzike naye kwa amani.
SALA
Tuombe: Bwana, utujalie usingizi mnono; na uzijalie kazi tulizofanya leo ziwe mbegu za mavuno ya
milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina
BARAKA
K. Bwana atujalie usiku mtulivu, na mwisho mkamilifu.
W. Amina
WIMBO kwa Bikira Maria
Ewe Mama wa Kristo, sikia kilio chetu,
Ewe nyota ya bahari, ewe Mlango wa mbingu,
Mama wa yeye mwenyewe, ambaye alikuumba,
Tunapozama topeni, msaada twakuomba;
Kwa furaha ile ile, Gabrieli alokupa,
E Bikira wa pekee, wa kwanza na mwisho pia,
Twakuomba tujalie, tupewe yako huruma.