Generic placeholder image

TOKEO LA BWANA - EPIFANIA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo ametutokea: njooni, tumwabudu.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI
Nyimbo za sifa na shukrani
Bwana Yesu tunakutolea;
Kwa njia ya nyota uwinguni
Mamajusi walikutambua;
Tawi la mfalme Daudi
Betlehemu ulizaliwa;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Ulidhihirishwa Yordani:
U kuhani, nabii, mfalme;
Na katika arusi ya Kana
Umungu wako ulionesha,
Ukageuza kwa yako nguvu
Maji yakawa divai tamu;

Nyimbo na shangwe na ziwe kwako,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

Tujalie ne'ma tukuone
Ee Bwana, katika neno lako;
Tuwezeshe kukuiga wewe,
Na tuwe safi kama mwenyewe,
Ili utapotokea tena
Tuwe watukufu kama wewe,

Na tukusifu Mbarikiwa,
Mungu uliyejifanya mtu
Ili watu wakuone wazi!

ANT. I: Mamajusi walifungua hazina zao, wakamtolea Bwana zawadi: Dhahabu, ubani na manemane, aleluya.

Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.

Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.

Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.

Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.

Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.

Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.

Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;

maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.

Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mamajusi walifungua hazina zao, wakamtolea Bwana zawadi: Dhahabu, ubani na manemane, aleluya.

ANT. II: Bahari na mito, msifuni Bwana; chemchemi za maji, mtukuzeni Bwana, aleluya.

WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)

Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.

Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.

Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.

Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.

Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.

Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.

Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.

Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.

Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.

Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.

Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.

Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.

Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.

Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.

Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.

Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

Ant. II: Bahari na mito, msifuni Bwana; chemchemi za maji, mtukuzeni Bwana, aleluya.

ANT. III: Yerusalemu, nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekutokea: mataifa yatatembea katika mwanga wako, aleluya.

Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo, mfalme wao (Hesychius)

Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!

Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.

Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.

Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.

Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.

Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,

ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;

wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.

kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Yerusalemu, nuru yako imekuja, na utukufu wa Bwana umekutokea: mataifa yatatembea katika mwanga wako, aleluya.

SOMO: Isa.52:7-10
Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu Auambiaye Sion, Mungu wako anamiliki! Sauti ya walinzi wako! Wanapaza sauti zao, wanaimba pamoja; Maana wataona jicho kwa jicho, Jinsi BWANA arejeavyo Sion. Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa BWANA amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu. BWANA ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu.

KIITIKIZANO
K. Wafalme wote wa dunia watamwabudu. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtumikia.
W. Wafalme watamwabudu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wafalme wote...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Leo Kanisa limeunganika na Bwana arusi wake wa mbinguni, maana Kristo amelitakasa na dhambi zake katika mto Yordani: Mamajusi wanafanya haraka kwenda kwenye arusi hiyo ya kifalme, na kutoa zawadi: wageni hufurahi kwa kuwa Kristo amegeuza maji yawe divai, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Leo Kanisa limeunganika na Bwana arusi wake wa mbinguni, maana Kristo amelitakasa na dhambi zake katika mto Yordani: Mamajusi wanafanya haraka kwenda kwenye arusi hiyo ya kifalme, na kutoa zawadi: wageni hufurahi kwa kuwa Kristo amegeuza maji yawe divai, aleluya.

MAOMBI
Mamajusi, leo, walipiga magoti mbele ya Mwokozi wetu. Nasi pia tumwabudu kwa furaha kuu.
W. Nuru ya mwanga wote, ujioneshe kwetu leo.

Kristo, uliyejionesha katika mwili:
- ututakase kwa neno la Mungu, na kwa sala. (W.)

Kristo, uliyeshuhudiwa na Roho;
- utuokoe na hali ya chuki na kutopatana maishani. (W.)

Kristo uliyeonwa na malaika;
- utushirikishe furaha ya mbinguni kuanzia sasa. (W.)

Kristo, uliyehubiriwa kati ya mataifa;
- uitawale mioyo yote kwa nguvu ya Roho wako. (W.)

Kristo, ambaye ulimwengu ulikusadiki;
- iamshe imani ya wafuasi wako. (W.)

Kristo, uliyepaa mbinguni na kutukuzwa:
- Washa ndani yetu hamu ya utawala wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, siku ya leo ulimtambulisha Mwanao wa pekee kwa watu wote duniani kwa njia ya nyota. Utuongoze kutoka kwenye imani, inayotuwezesha kukujua wewe sasa, hata tuuone kwa macho yetu utukufu wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.