TOKEO LA BWANA - EPIFANIA
MASIFU YA JIONI I
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Betlehemu mji ulo bora
Mji ulo sawa nawe hakuna:
Ndiwe peke uliyetuzalia
Bwana wa kutoka mbinguni juu.
Nyota ilotangaza kuzaliwa
Ilikuwa nzuri kuliko jua;
Ilitangazia nchi Mungu wao
Aloonekana katika mwili.
Wakiongozwa kwa mng'aro huo
Wafalme wa mashariki watokea;
Wasujudu na zawadi kutoa:
Ubani, dhahabu na manemane.
Zawadi takatifu zenye fumbo:
Ubani Mungu wamdhihirisha,
Dhahabu Mfalme yamtangaza,
Manemane yabashiri kaburi.
Sifa milele ziwe kwako Yesu,
Ulijionesha kwa Mataifa
Katika utukufu wako Bwana,
Pia ziwe kwa Roho na kwa Baba.
ANT. I: Yeye aliyezaliwa kwa Baba kabla ya alfajiri na kabla ya
nyakati zote, leo, Bwana, Mwokozi wetu, alizaliwa na Bikira.
Zab.135 Sifa kwa Mungu
I
Lisifuni jina la Mungu,*
enyi watumishi wake,
mnaosimama nyumbani mwa Mungu,*
Hekaluni mwa Mungu wetu.
Msifuni Mungu kwa kuwa ni mwema;*
liimbieni jina lake sifa maana inafaa.
Mungu amejichagulia Yakobo kuwa wake,*
watu wa Israeli kuwa mali yake mwenyewe.
Najua hakika kuwa Mungu ni mkuu;*
Bwana wetu ni mkuu juu ya miungu yote.
Mungu hufanya yote anayotaka,*
mbinguni, duniani, baharini na vilindini.
Huleta mawingu kutoka mipaka ya dunia;/
hufanya gharika kuu kwa umeme,*
na huvumisha upepo kutoka ghala zake.
Aliwaua wazaliwa wa kwanza kule Misri,*
wazaliwa wa watu na wanyama kadhalika.
Alifanya ishara na maajabu kwako, Ee Misri,*
dhidi ya Farao na maofisa wake wote.
Aliyaangamiza mataifa mengi,*
akawaua wafalme wenye nguvu:
akina Sihoni mfalme wa Waamori,*
na Ogu mfalme wa Bashani, na wafalme wote wa Kanaani.
Alichukua nchi zao na kuwapa watu wake;*
aliwapa Waisraeli ziwe urithi wao.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Yeye aliyezaliwa kwa Baba kabla ya alfajiri na kabla ya
nyakati zote, leo, Bwana, Mwokozi wetu, alizaliwa na Bikira.
ANT. II: Bwana, Mungu wetu, ni mkuu kuliko miungu yote.
II
Ee Mungu, jina lako lakumbukwa milele,*
utakumbukwa na watu wa vizazi vyote.
Maana Mungu atawatetea watu wake;*
atakuwa na huruma kwa watumishi wake.
Miungu ya mataifa ni fedha na dhahabu,*
imetengenezwa na mikono ya binadamu.
Ina vinywa, lakini haisemi;*
ina macho lakini haioni.
Ina masikio, lakini haisikii;*
wala haiwezi hata kuvuta pumzi.
Wote walioifanya wafanane nayo,*
naam, kila mmoja anayeitegemea!
Enyi watu wa Israeli, mtukuzeni Mungu!*
Enyi makuhani, wazao wa Aroni, mtukuzeni Mungu!
Enyi Walawi, mtukuzeni Mungu!*
Enyi wachaji wa Mungu, mtukuzeni.
Atukuzwe Mungu katika Sion,*
katika makao yake Yerusalemu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Bwana, Mungu wetu, ni mkuu kuliko miungu yote.
ANT. III: Nyota hii inang'ara kama mwali wa moto; inamtambulisha Mungu,
Mfalme wa wafalme: mamajusi waliiona, wakamtolea zawadi Mfalme mkuu.
WIMBO: 1Tim.3:16
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!
Alionekana katika umbo la kibinadamu,*
akathibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu.
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!
Alionekana na malaika,*
akahubiriwa kati ya mataifa.
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!
Aliaminiwa po pote ulimwenguni,*
akachukuliwa juu mbinguni katika utukufu.
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu*
Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina,
W. Msifuni Bwana, enyi mataifa yote!
ANT. III: Nyota hii inang'ara kama mwali wa moto; inamtambulista Mungu,
Mfalme wa wafalme: mamajusi waliiona, wakamtolea zawadi Mfalme mkuu.
SOMO: 2Tim.1:9-10
Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya mastahili ya matendo
yetu, bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo kwa ajili ya Kristo
Yesu kabla ya nyakati, lakini imefunuliwa kwetu sasa kwa kuja kwake Mkombozi wetu, Yesu Kristo;
yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Injili akadhihirisha uzima usio na kifo.
KIITIKIZANO
K. Watu wote watabarikiwa katika yeye. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtukuza.
W. Yatabarikiwa katika yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Watu wote...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mamajusi waliiona nyota, wakaambiana: Hii ni ishara ya Mfalme mkuu; twende tukamtafute;
tukamtolee zawadi: dhahabu, ubani na manemane.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Mamajusi waliiona nyota, wakaambiana: Hii ni ishara ya Mfalme
mkuu; twende tukamtafute; tukamtolee zawadi: dhahabu, ubani na manemane.
MAOMBI
Leo mamajusi walipiga magoti mbele ya Mwokozi wetu. Nasi pia tumwabudu kwa furaha kuu, na kuomba:
W. Bwana, utusaidie katika dhiki zetu.
Mfalme wa mataifa, watu wenye hekima na busara walitoka Mashariki, wakaja kukuabudu;
- utujalie roho ya kweli ya ibada na unyenyekevu. (W.)
Mfalme wa utukufu, watu wako wanatazamia hukumu kutoka kwako:
- uijalie dunia yetu wingi wa amani. (W.)
Mfalme wa nyakati, neno lako lina nguvu milele;
- na lipenye mioyo na maisha yetu leo. (W.)
Mfalme wa haki, onesha upendo wako kwa maskini na wanyonge;
- uwaimarishe wale wanaoteseka. (W.)
Mfalme wa mbinguni, tumaini la wote wanaokutumainia;
- uwajalie waamini marehemu maajabu ya wokovu wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, siku ya leo ulimtambulisha Mwanao wa pekee kwa watu wote duniani kwa njia ya nyota.
Utuongoze kutoka kwenye imani, inayotuwezesha kukujua wewe sasa, hata tuuone kwa macho yetu utukufu
wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho
Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.