TOKEO LA BWANA - EPIFANIA
MASIFU YA JIONI II
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. (Aleluya)
UTENZI
Betlehemu, ni wewe tuu!
Hakuna mji mwingine tena;
Ni wewe peke ulimshusha
Bwana Yesu kutoka mbinguni
Awe mtu kwa ajili yetu.
Nyota ile iliyotangaza
Kuzaliwa kwake huyo Mwana
Iling'ara kulishinda jua,
Ikaitangazia dunia
Mungu wake mtu kajifanya.
Ndo wafalme wa mashariki
Wakajitokeza, mamajusi,
Wakiongozwa na nyota nzuri;
Walimwinamia na kutoa
Ubani, dhahabu, manemane.
Na zawadi takatifu hizo
Zinaonesha maana nzito:
Ubani wadhihirisha Mungu,
Dhahabu, Mfalme wa Wafalme,
Manemane hubashiri kifo.
Katika utukufu, E Bwana,
Ulijionesha waziwazi,
Kwa Watu wasio Wayahudi;
Kwako Wewe na Roho na Baba,
Sifa tele milele. Amina.
ANT. I: Mfalme wa amani ni mtukufu kuliko wafalme wote wa dunia.
Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini
ya miguu yake (Kor.15:25)
Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,
Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."
Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"
Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.
Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.
Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.
Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Mfalme wa amani ni mtukufu kuliko wafalme wote wa dunia.
ANT. II: Sasa mwenge unamulika gizani kwa ajili ya watu waadilifu;
Bwana ni mwema, mpole na mwenye huruma.
Zab.112 Furaha ya mtu mwema
Heri mtu anayemcha Mungu,*
anayefurahia sana kutii amri zake
Watoto wake watakuwa wenye enzi duniani;*
wazao wake watabarikiwa.
Jamaa yake itakuwa tajiri,*
naye atakuwa na fanaka daima.
Watu wema huangaziwa mwanga wa furaha,/
kama vile taa iangazavyo gizani;*
naam, watu wenye huruma, wapole na waadilifu.
Heri mtu mkarimu, akopeshaye bila faida;*
aendeshaye shughuli zake kwa kutumia haki.
Mwadilifu hatashindwa kamwe,*
na atakumbukwa daima.
Akipata habari mbaya haogopi;*
moyo wake ni thabiti na humtumainia Mungu.
Hana wasiwasi, wala haogopi;*
ana hakika adui zake watashindwa.
Huwapa maskini kwa ukarimu./
Wema wake haubadiliki.*
Mtu wa namna hiyo atasifika daima.
Waovu huona hayo na kuudhika;/
husaga meno kwa chuki na kutoweka,*
mambo huenda kinyume cha matazamio yao.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Sasa mwenge unamulika gizani kwa ajili ya watu waadilifu;
Bwana ni mwema, mpole na mwenye huruma.
ANT. III: Bwana, watu wote, ambao umewaumba, watakujia na kukuabudu.
WIMBO: Ufu.15:3-4
Bwana, Mungu Mwenyezi,*
matendo yako ni makuu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,*
njia zako ni za haki na za kweli!
Bwana, ni nani asiyekucha wewe?/
Nani asiyelitukuza jina lako?*
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu,/
maana matendo yako ya haki*
yameonekana na wote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Bwana, watu wote, ambao umewaumba, watakujia na kukuabudu.
SOMO: Tito 3:4-5
Wakati wema na upendo wa Mungu, Mkombozi wetu, ulipofunuliwa, alitukomboa. Alitukomboa si kwa
sababu ya jambo lo lote jema tulilotenda sisi, bali alitukomboa kwa sababu ya huruma yake, kwa
njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji.
KIITIKIZANO
K. Mataifa yote yatabarikiwa katika yeye. (W. Warudie)
K. Mataifa yote yatamtukuza.
W. Yatabarikiwa katika yeye.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mataifa yote...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Maajabu matatu yanaipambanua sikukuu hii tunayoadhimisha: leo nyota iliwaongoza mamajusi
kwenye hori; leo maji yaligeuzwa kuwa divai arusini Kana; leo Kristo alitamani kubatizwa na
Yohane katika mto Yordani ili kutuletea wokovu, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Maajabu matatu yanaipambanua sikukuu hii tunayoadhimisha:
leo nyota iliwaongoza mamajusi kwenye hori; leo maji yaligeuzwa kuwa divai arusini Kana;
leo Kristo alitamani kubatizwa na Yohane katika mto Yordani ili kutuletea wokovu, aleluya.
MAOMBI
Leo mamajusi walipiga magoti mbele ya Mwokozi wetu. Nasi pia tumwabudu kwa furaha kuu, na kuomba:
W. Bwana, utusaidie katika dhiki zetu.
Mfalme wa mataifa, watu wenye hekima na busara walitoka Mashariki, wakaja kuabudu;
- utujalie roho ya kweli ya ibada na unyenyekekevu. (W.)
Mfalme wa utukufu, watu wako wanatazamia hukumu kutoka kwako:
-uijalie dunia yetu wingi wa amani. (W.)
Mfalme wa nyakati, neno lako lina nguvu milele;
- na lipenye mioyo na maisha yetu leo. (W.)
Mfalme wa haki, onesha upendo wako kwa maskini na wanyonge;
- uwaimarishe wale wanaoteseka. (W.)
Mfalme wa mbinguni, tumaini la wote wanaokutumainia;
- uwajalie waamini marehemu maajabu ya wokovu wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, siku ya leo ulimtambulisha Mwanao wa pekee kwa watu wote duniani kwa njia ya nyota.
Utuongoze kutoka kwenye imani, inayotuwezesha kukujua wewe sasa, hata tuuone kwa macho yetu utukufu
wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho
Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.