UBATIZO WA BWANA YESU
ANTIFONA YA KUINGIA: Mt.3:16-17
Bwana alipokwisha kubatizwa, mbingu zikamfunukia, Roho akashuka kwa mfano wa hua, na kukaa juu yake;
na tazama, sauti ya Baba ikasema: Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.
Utukufu husemwa
KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi wa milele, ulimtangaza rasmi Kristo kuwa ndiye Mwanao mpenzi, hapo
alipobatizwa katika mto Yordani na kushukiwa na Roho Mtakatifu. Uwajalie uliowafanya
wanao kwa kuzaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu, wadumu daima katika upendo wako. Kwa
njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho
Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
Au:
Ee Mungu, Mwanao pekee amedhihirika katika ubinadamu wetu. Tunakuomba utujalie ili utu wetu
wa ndani uundwe upya kwa njia yake yeye, tuliyemfahamu kwa nje kuwa sawa nasi. Anayeishi na
kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Isa.42:1-4,6-7
Bwana asema: Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye;
nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala
kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima;
atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa
vitaingojea sheria yake. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na
kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa,
kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.29:1-4,9-10 (K)11
1. Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu;
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake;
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani.
2. Sauti ya Bwana i juu ya maji
Bwana yu juu ya maji mengi
Sauti ya Bwana ina nguvu,
Sauti ya Bwana ina adhama. (K)
3. Sauti ya Bwana yawazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake wanasema wote, Utukufu.
Bwana aliketi juu ya Gharika;
Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)
SOMO 2: Mdo.10:34-38
Siku ile: Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo,
bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Neno lile alilowapelekea
wana wa Israeli, akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote), jambo
lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya Ubatizo aliohubiri
Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye
akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu
alikuwa pamoja naye.
SHANGILIO: Kol.3:15,16
Aleluya, aleluya!
Mbingu zilifunguka na sauti ya Baba ikasikika,
“Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”
Aleluya!
Nenda Injili na Maombi mwaka B
Nenda Injili na Maombi mwaka C
INJILI NA MAOMBI MWAKA A
INJILI: Mt.3:13-17
Siku ile: Yesu alirudi kutoka Galilaya mpaka Yordani kwa Yohane ili abatizwe. Lakini Yohane
alitaka kumzuia, akisema, Mimi nahitaji kubatizwa na wewe, nawe waja kwangu? Yesu akajibu akamwambia,
Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali. Naye Yesu alipokwisha
kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka
kama hua, akija juu yake; na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu wapenzi, tumwombe sasa Mungu aliyemtuma Mwanae akamshuhudia kwamba ndiye
Mpendwa wake, tukisema: Bwana, utuhurumie. Ee Utatu Mtakatifu wa Mungu mmoja,
1. Ulimshuhudia Kristo kuwa ndiye Mkombozi wa dunia alipobatizwa mtoni Yordani: Uliwezeshe Kanisa lako
kumshuhudia Mwanao ulimwenguni kwa njia ya mafundisho na matendo ya huruma kwa watu.
2. Uwajalie wote waliobatizwa, na kupata Kipaimara, kumshuhudia Kristo kwa matendo ya kila siku maishani
mwao.
3. Uwasaidie watu kupokea wito wako, wachumba wafunge ndoa na waliofarakana katika ndoa kupatana na
kurudiana ili wakushuhudie wewe kama Mungu wao.
4. Utujalie sisi sote tuliobatizwa kukushuhudia kwa maneno na mwenendo wa maisha yetu.
5. Uwasamehe marehemu waliotubatiza na Uwaweke mahali pema huko mbinguni.
Ee Mungu, uliye na mapendo makubwa kwa sisi taifa lako, uyasikilize maombi
yetu kwa njia ya Mwanao Mpendwa, Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.
------------------------
INJILI NA MAOMBI MWAKA B
INJILI: MK1:7-11
Siku ile: Yohane alihubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi
sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake. Mimi nimewabatiza kwa maji; bali yeye
atawabatiza kwa Roho Mtakatifu. Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya,
akabatizwa na Yohane katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka,
na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa
wangu; nimependezwa nawe.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu zangu, tumwombe Mwokozi wetu aliyejinyenyekeza hata akabatizwa na Yohana
Mbatizaji. Tumuombe. Kristo, Mtumishi Mpendevu,
1. Umtume Roho wako kwetu atuongoze katika maisha yetu ya kila siku.
2. Ee Mteule wa Mungu, tete lililopondeka wewe hukulivunja, naam, wala hukuwakatisha tamaa wakosefu,
uwahakikishie watu wote huruma yako.
3. Ewe Nuru ya Mungu kwa mataifa, ponya upofu wa roho kwa maji na Roho Mtakatifu.
4. Uwape wakunga ushujaa wa kuwabatiza watoto wachanga wanaofariki mara baada ya kuzaliwa.
5. Uwapokee mbinguni wale wote waliofariki dunia katika ubatizo wa tamaa tu.
Ee Mungu Baba, ulimshuhudia Mwanao kwa sauti yako kutoka mbinguni. Uwaongoze
wazazi kuwapeleka watoto wao kwa ajili ya sakramenti ya ubatizo. Tunakuomba hayo, Wewe unayeishi pamoja
na Mungu Mwana na Roho Mtakatifu, daima na milele. Amina.
------------------------
INJILI NA MAOMBI MWAKA C
INJILI: Lk.3:15-16,21-22
Siku ile: watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohane,
kama labda yeye ndiye Kristo, Yohane alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini
yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye
atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye
amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka; Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili;
kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu wapendwa, tumwombe Mkombozi wetu aliyeomba yeye mwenyewe abatizwe na
Yohana Mbatizaji, Mtoni Yordani. Tumwombe tukisema: Bwana utusikie, Bwana utusikilize! Ee Mungu, Nabii
Isaya alikuagua akisema kuwa, watu waliokaa gizani wameona nuru kubwa, twakuomba:
1. Umzuie shetani asiwahadae watu wanaoomba ubatizo.
2. Uwasaidie wakatekumeni kuamua kubatizwa bila kuwaogopa jamaa zao.
3. Tunakuomba uamshe roho ya umisionari katika vijana wetu, wajitoe kutenda kazi ya kuhubiri habari njema
kwa watu.
4. Wabatizwa wote ni watoto wa Mungu. Uwawezeshe watu kujali na kuheshimu utu na haki za binadamu.
5. Uwapokee marehemu wabatizwa wote kwenye ufalme wako.
Ee Bwana, twakuomba, imarisha na kudumisha uzima wa roho ndani yetu. Tunaomba
hayo kwa njia ya Kristo Mwanao, Bwana wetu. Amina
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uvipokee vipaji tunavyokutolea katika sikukuu ya kujidhihirisha kwake
Mwanao mpendwa. Nayo matoleo ya waamini wako yageuzwe kuwa sadaka yake Yeye, ambaye katika
huruma yake alitaka kuzifuta dhambi za ulimwengu. Anayeishi na kutawala milele na milele.
UTANGULIZI: Ubatizo wa Bwana.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru
wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Katika mto Yordani ulianzisha kwa ishara za ajabu ubatizo mpya. Kwa sauti iliyotoka mbinguni ulitaka watu wasadiki kwamba Neno
wako anakaa kati yao. Tena, kwa Roho Mtakatifu kumshukia kwa sura ya njiwa, ulitaka Kristo
Mtumishi wako ajulikane kuwa amepakwa mafuta ya furaha na kutumwa kuwahubiria maskini Habari
njema.
Kwa hiyo, sisi pamoja na Nguvu za mbinguni, tunakutukuza daima hapa duniani, tukisifu
bila mwisho adhama yako kwa sauti kuu:
Mtakatifu...
ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.1:32,34
Tazama, Yohane alinena hivi juu yake: Mimi nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kushibishwa kwa kipawa chako kitakatifu, tunakuomba sana huruma yako, ili,
kwa kumsikiliza kiaminifu Mwanao pekee, tupate kweli kuitwa na kuwa wanao. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu.