SALA YA USIKU
VIJILIA YA SHEREHE

(Kabla ya kulala)
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

Kuchunguza dhambi:
K. Tuwaze katika moyo makosa tuliyomkosea Mungu, kwa mawazo kwa maneno, kwa matendo na kwa kutotimiza wajibu: (kimya kifupi)

W. Namwungamia Mungu mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kwa kutotimiza wajibu: nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana namwomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.

K. Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele.
W. Amina

TENZI chagua 1-8

AU
1
Kristo mwanga wetu wa kweli,
Kristo asubuhi ya kweli,
Mwondoaji vya usiku vivuli,
Mwanga unaozaa kila mwanga,
Amana ya nuru ya heri, Bwana:

Uwe mlinzi wetu usiku kucha
Wewe ulindaye bila kulala
Uwe amani yetu, Ee Bwana,
Ili gizani tuwapo na Wewe,
Tuweze kupumzika kwa raha.

Macho yetu usingizi yapige,
Lakini moyo kamwe usilale,
Moyo uloelekezwa mbinguni;
Na twaomba salama uwalinde
Watumishi wanaokutamani.

Ututazame, Bwana, tutazame,
Nao maadui wetu na wako
Mbali nasi, Bwana, wafukuzie;
Maovuni waopoe wa'mini
Ulowakomboa kwa damu yako.

Wakati roho ingali mwilini,
Utulinde mwili na roho, Bwana,
Tuwe salama katika uvuli
Uvuli wa mabawa yako, Bwana,
Daima tulindwe kwa kinga yako.

AU
2
Wakati huu ni jioni
Muda wa kumaliza kazi;
Kadiri ya mapenzi yako,
Na utavyoridhika Baba,
Kipindi chote cha usiku
Watu wako waaminifu
Bwana utuweke salama.

Uyafukuze mashetani
Na zetu nyumba yawe mbali;
Tulinde katika uvuli
Ulo chini ya mbawa zako;
Uwe pia mlinzi wetu
Wakati wote wa usiku,
Utusimamie imara.

Na kabla hatujalala
Jina la Yesu twalitaja;
Tayari kukutumikia
Tuamkapo asubuhi;
Matendo yetu uyapange
Yaanze na yaishe vema,
Yote kwa utukufu wako.

Ewe chemchemi ya wema
Uwabariki wenye dhiki,
Mateka uwatembelee
Wafariji wanoteseka,
Uwahifadhi na wageni,
Lisha watoto wenye njaa,
Imarisha wanaokufa.

Ee Baba, usosinzia
Wewe kamwe usiyelala,
Kwako giza li mwanga 'tupu
Li angavu kama mchana,
Kwa mastahili ya Yesu
Twakuomba usiku huu
Sisi utuweke salama.
P. Herbert +1571

AU
3
Uniongoze, Mwanga mtulivu,
Katikati ya hili giza nene,
Niongoze mbele;
Usiku huu umejaa giza,
Na mimi nipo mbali na nyumbani,
Niongoze mbele;
Tia nguvu hii yangu miguu;
Siombi nione mbali upeo;
Hatua moja mbele yanitosha.

Kamwe na sijapata kuwa hivi
Na wala sijapata kukuomba
Uniongoze mbele;
Daima nilipenda kuchagua
Na kuona njia - lakini sasa
Niongoze mbele.
Nilipenda siku inayong'ara
Nikatawaliwa na majivuno:
Usikumbuke miaka ya nyuma.

Umenineemesha hadi sasa,
Na bila shaka utaendelea
Kuniongoza mbele
Katika nyika, mbuga na miamba,
Na kwenye mabubujiko - mpaka
Usiku upite!
Asubuhi nione za tabasamu
Nyuso za malaika nizipendazo,
Nilizozipoteza kwa kitambao.
J.H. Newman 1801-1890

AU
4
Yaja kwa kasi jioni,
Ukae pamoja nami;
Giza linaongezeka,
Sina wa kunifariji
Ukae Bwana na mimi;
U Auni kwa dhaifu,
Na uwe pamoja nami.

Yamesha fika mwishoni,
Maisha sasa yaisha,
Raha za dunia basi;
Zakoma fahari zake;
Yamegeuka uwozo,
Yote ninayoyaona;
Ee usobadilika
Ukae pamoja nami.

Nyosha wako msalaba
Kwa yangu macho, yafumba!
Nimulikie gizani,
Nielekeze angani;
Kunakucha uwinguni,
Vivuli hakuna chini;
Katika maisha, kifo,
Ee Bwana, uwe nami.
H.F.Lyte 1793-1847

AU
5
Siku ulotupa, Bwana, imesha.
Kwa neno lako giza huingia;
Asubuhi na tulikuimbia,
Hizo sifa kwako zilizopaa,
Pumziko letu tatakatifuza.

Kanisa lako li macho, asante,
Dunia izungukapo usiku,
Lakesha macho duniani kote,
Lipo macho mchana na usiku;
Kanisa halipumziki kamwe.

Kama ilivyo bara, visiwani
Mapambazuko hukarisha
Siku nyingine kila asubuhi,
Na masifu yetu hayafifii.

Jua linaloamuru tulale
Ndilo linalowaamsha pia
Ndugu zetu walio magharibi;
Hivi kuna midomo kila saa
Itangazayo yako maajabu.

Amina, enziyo haitapita
Kama tawala zinazojivuna;
Ufalme wako upo imara
Nao milele waenea, Bwana,
Hata viumbe vyote vikukiri.
J. Ellerton 1826-1893

AU
6
Sote twamshukuru Mungu wetu,
Kwa mioyo, mikono na sauti,
Kafanya maajabu Yeye huyo,
Vyake viumbe vinashangilia;
Tangu mwa mama zetu mikononi
Za kwetu njia kazibarikia
Tuna vipawa vya upendo tele,
Hata leo bado ni Mungu wetu.

Uwe karibu Mungu Mkarimu
Kwa siku zote za maisha yetu,
Mioyo yetu iwe mikunjufu
Kwa amani yako tuchangamshwe;
Katika neema yako tuweke,
Mashakani njia utuoneshe,
Utuepushe na maovu yote
Ya ulimwengu huu na ujao.

Sifa na shukrani kwako Mungu
Kwako Baba sasa na zitolewe,
Kwa Mwana, na kwa anayetawala
Pamoja na ninyi juu mbinguni,
Ewe Mungu Mmoja wa milele
Mbingu na dunia zakuabudu;
Vile ilivyokuwa ndo ilivyo,
Na hivyo itakuwa kwa milele.
M. Rinkart 1586-1649

AU
7
Bwana wa matumaini yote,
Ee Bwana wa furaha yote,
Hapana shughuli iwezayo
Kuharibu tumaini kwako;
Uwe nasi tunapoamka,
Na utujalie, twakuomba,
Furahayo mwetu mioyoni
Utujaze kila asubuhi.

Ewe Bwana wa juhudi yote,
Ewe Bwana wa imani yote,
Mikono yako yenye ufundi
Ilifanya sawa kila kazi;
Uwe na sisi kazini Bwana,
Na utujalie, twakuomba,
Nguvu yako mwetu mioyoni
Bwana, ua liwapo kichwani.

Ewe Bwana na wa wema wote
Ewe bwana wa neema zote,
U mwepesi wa kukaribisha,
U mwepesi wa kukumbatia;
Uwe nasi twendapo nyumbani,
Na utujalie, twakuomba,
Pendo lako mwetu mioyoni
Jua linapozama jioni.

Ewe Bwana wa upole wote,
Na Bwana wa utulivu wote,
Sauti yako inaridhisha,
Uwepo wako huburudisha;
Uwe na sisi tunapolala,
Na utujalie, twakuomba,
Amani yako mwetu nyoyoni
Mwisho wa siku, Bwana mwamini.
Jan Struther 1901-1953

AU
8
Tubariki pote, Mwokozi mwema,
Yetu akili neno lako ipe,
Washa mioyo yetu vuguvugu
Ipe pendo na utashi imara.
Tuwapo hai na tukisha kufa
Tuongoze, Ee Yesu mpole.

Siku imekwisha, saa 'mekwenda,
Na mambo yote wewe wayajua:
Neema imeshinda kidogo tu,
Makosa na kushindwa ni daima.
Tuwapo hai na tukisha kufa
Tuongoze, Ee Yesu mpole.

Na twawaombea wapenzi wote:
Maskini, wakosefu, wanyonge,
Kwa huruma yako tufurahishe;
Ndiwe Yesu wetu na yetu yote.
Tuwapo hai na tukisha kufa
Tuongoze, Ee Yesu mpole.
F. W. Faber 1814-1863

Ant. 1: Bwana, unihurumie na unisikilize.

Zab.4 Kuomba msaada jioni
Bwana alimfufua kutoka wafu, akamfanya astahili sifa zote (Mt. Augustino)

Ee Mungu mtetezi wangu, unisikilize niombapo./
Nilipokuwa katika shida, wewe ulinisaidia;*
sasa nionee huruma, na kusikiliza sala yangu.

Jamani! Ninyi mtanitukana mpaka lini?*
Mbona mwapenda upuuzi na kusema uwongo?

Fahamuni kwamba Mungu amejiteulia mwadilifu wake.*
Mungu hunisikiliza kila nimwombapo.

Tetemekeni kwa uchaji na msitende dhambi;*
tafakarini kwa makini vitandani mwenu, tulieni.

Toeni sadaka za haki;*
na kumtumainia Mungu.

Wengi huomba: "Utujalie tupate fanaka;*
Ee Mungu, utuangalie kwa wema!"

Lakini furaha uliyonijalia moyoni/
ni kubwa zaidi kuliko yao,*
hata kama wanao wingi wa divai na ngano.

Mimi nalala na kupata usingizi kwa amani;/
maana wewe peke yako, Ee Mungu,*
wanilinda salama salimini.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. 1: Bwana, unihurumie na unisikilize.

Ant. 2: Msifuni Bwana, usiku kucha.

Zab.134 Msifu Mungu
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote, nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa (Ufu.19:5)

Njoni kumsifu Mungu, enyi watumishi wake wote,*
enyi nyote mnaotumikia usiku nyumbani mwake.

Inueni mikono kuelekea mahali patakatifu,*
na kumtukuza Mungu!

Mungu akubariki kutoka Sion;*
yeye aliyeumba mbingu na dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. 2: Msifuni Bwana, usiku kucha.

SOMO: Kum.6:4-7
Sikiliza, Ee Israeli; BWANA, Mungu wetu, BWANA ndiye mmoja. Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.

KIITIKIZANO
K. Mikononi mwako, Ee Bwana, naiweka roho yangu. (W. Warudie)
K. Umetukomboa, Bwana Mungu wa kweli.
W. Mikononi mwako, naiweka roho yangu.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Mikononi...

Ant. Utuokoe, Ee Bwana, wakati tukiwa macho; utulinde tukiwa usingizini; ili tukeshe pamoja na Kristo, na tupumzike naye kwa amani.

WIMBO wa Simeoni: Lk.2:29-32
Kristo ni nuru ya mataifa, na utukufu wa Israeli

Sasa, Bwana, umetimiza ahadi yako,/
waweza kumruhusu mtumishi wako,*
aende kwa amani.

Maana kwa macho yangu/
nimeuona wokovu utokao kwako,*
ambao umeutayarisha mbele ya watu wote:

Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa,*
na utukufu kwa watu wako Israeli.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Utuokoe, Ee Bwana, wakati tukiwa macho; utulinde tukiwa usingizini; ili tukeshe pamoja na Kristo, na tupumzike naye kwa amani.

SALA
Tuombe: Ee Bwana, twakuomba uingie katika nyumba hii, na uondolee mbali mitego yote ya adui. Malaika wako watakatifu wabaki humu, watulinde kwa amani; na baraka yako idumu nasi daima. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

W. Amina

BARAKA
K. Bwana atujalie usiku mtulivu, na mwisho mkamilifu.

W. Amina

WIMBO kwa Bikira Maria
Salamu Malkia wa mbingu,
Malkia usiye kifani,
Malaika wanakuheshimu;
Salamu ewe Shina la Yese,
Salamu wewe Lango la Nuru,
Uliifungukia dunia
Ili siku mpya ianze.

Ebu furahi, Ee Bikira,
Hakuna wa kukuzidi wewe,
Hata ukombozi wetu sisi
Ulianzishwa ndani mwako,
Sote watoto wako wapenzi
Utuombee kwa Kristo
Mkombozi wetu na Mwanao.