KUZALIWA BWANA
24 DESEMBA MISA YA KESHA

MASOMO MISA YA KESHA

Misa hii inasaliwa tarehe 24 Desemba, wakati wa jioni, au kabla au baada ya Vesperi ya Kwanza ya Noeli.

ANTIFONA YA KUINGIA: Kut.16:6-7

Leo ndipo mtakapojua ya kuwa Bwana atakuja naye atatuokoa; na asubuhi ndipo mtakapouona utukufu wake.

Utukufu husemwa

KOLEKTA:
Ee Mungu, unatufurahisha kila mwaka kwa kutazamia ukombozi wetu. Utujalie, ili Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao pekee, tunayempokea kwa furaha kama Mkombozi, tustahili kumwona pasipo hofu atakapokuja pia kama hakimu. Anayeishi na Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.62:1-5
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na Kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako. Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; Kwa kuwa Bwana anakufurahia na nchi yako itaokolewa. Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe, na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi harusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.89:3-4,15-16,26,28
1. Nimefanya agano na mteule wangu,
Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
Wazao wako nitawafanya imara milele,
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)

(K) Fadhili za Bwana nitaziimba milele.

2. Fadhili za Bwana nitaziimba milele.
Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe,
Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
Kwa Jina lako hufurahi mchana kutwa,
Na Kwa haki yako hutukuzwa. (K)

3. Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)

SOMO 2: Mdo.13:16-17,22-25
Paulo alipofika Antokia ya Pisidia, akasimama katika Sinagogi akawapungia mkono, akasema, Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni. Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na Kwa mkono ulioinuliwa akawatoa akawaongoza. Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, Akisema, Nimemwona Daudi mwana wa Yese, mtu anaye upendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani Yesu, kama alivyoahidi; Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba kabla ya kuja kwake. Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani Mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sisitahili kumlegezea viatu vya miguu yake.

SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Kesho dhambi ya ulimwengu itakomeshwa, Na Mwokozi wa ulimwengu atakuwa Mfalme wetu.
Aleluya!

SOMO: INJILI: Mt.1:1–17
Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu. Ibrahimu akamzaa Yuda na ndugu zake; Yuda akamzaa Peresi na zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu; Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni; Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese; Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia; Hezekia akamzaa Manase; Manase akamaza Amoni; Amoni akamzaa Yosia; Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli. Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli; Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori; Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi; Eliudi akamzaa Eleazari; eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo. Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo. Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi kumi na vinne. Kuzaliwa kwake Yesu Kristu kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba Kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, Kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, akiazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni Kwa uwezo wa Roho Mtakakitu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa ili litimie neno lililonenwa na Bwana Kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama bikira atachujua mimba, naye atazaa mwana; nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika alivyomwagiza; akamchukua mkewe; asimjue kamwe hata alipomzaa mwanawe; akamwita jina lake Yesu.

Nasadiki husemwa.
Wote hupiga magoti yasemwapo maneno Akapata mwili ...akawa mwanadamu.


MAOMBI
Ndugu, usiku huu ambapo wokovu na amani vilitangazwa na malaika wa Bwana kwa watu wote duniani, tumwombe Mungu ili atujalie nasi mahitaji yetu. Ee Mungu, kwa umwilisho wa Mwano Yesu Kristo, twakuomba:

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umbariki Baba Mtakatifu F. na Askofu wetu F.; na ulijalie Kanisa lako umoja na amani, na ulifanye kuwa chombo thabiti cha kuyapatanisha mataifa yote duniani.

2. Uyapatie mataifa yote ya dunia fikara za amani na uelewano, ili kuidumisha furaha hii uliyotuletea leo.

3. Uondoe giza la dhambi mioyoni mwa wote wenye mapenzi mema, ili amani yako ienee duniani kote.

4. Utuongezee sisi sote bidii ya kuitangaza habari njema ya wokovu kwa mataifa yote, ili yapate kuokoka.

5. Uwapokee marehemu wetu wapate kuishiriki furaha ya uzima mpya huko mbinguni.

Hayo ni baadhi tu ya tunayo kuomba kupitia kwa Mwanao, Yesu Kristo, aliyetwaa ubinadamu wetu ili tuuonje uwepo wake kati yetu, daima na milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie tuingie katika sikukuu hizi kwa juhudi kubwa zaidi, kama vile wewe unavyozidi kutuonesha kwamba hizo ndio mwanzo wa ukombozi wetu. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao anayeishi na kutawala nawe daima na milele.

UTANGULIZI: KUZALIWA KWA BWANA I:
(Kristo ni mwanga).

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Maana, kwa fumbo la Neno aliyetwaa mwili, mwanga mpya wa utukufu wako umetuangazia macho ya akili zetu; ili, tunapomjua Mungu katika hali ya kuonekana, kwa njia yake tuvutwe kuyapenda mambo yasiyoonekana.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.40:5
Utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu wetu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie nguvu mpya katika kukumbuka kuzaliwa kwake Mwanao pekee, ambaye anatulisha na kutunywesha kwa sakramenti yake ya mbinguni. Anayeishi na kutawala milele na milele.