KUZALIWA BWANA
25 DESEMBA

MASOMO MISA YA USIKU

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.2:7
Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

Au:

Tufurahi sote katika Bwana, kwa sababu Mwokozi wetu amezaliwa duniani. Leo amani ya kweli imetushukia toka mbinguni.

Utukufu husemwa

KOLEKTA:
Ee Mungu, uliuangaza usiku huu mtakatifu sana kwa mng'ao wa Nuru halisi. Tunakuomba utujalie ili tufurahie kikamilifu pia mbinguni furaha zake yeye ambaye mafumbo yake ya mwanga tumeyajua hapa duniani. Anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.9:2-7
Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno; Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na Gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, Kama katika siku ya Midiani. Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni. Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:1-3,11-13 (K) Lk.2:11
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya.
Mwimbieni Bwana nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake.

(K) Leo amezaliwa kwa ajili yetu Mwokozi, Ndiye Kristo Bwana.

2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake
Na watu wote habari za maajabu yake. (K)

3. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha. (K)

4. Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
na mataifa kwa uaminifu wake. (K)

SOMO 2: Tit.2:11-14
Neema ya Mungu Mwokozi wetu inayowaokoa wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye Baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.

SHANGILIO: Lk.2:10-11
Aleluya, aleluya!
Malaika akawaambia, msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema. ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Lk.2:1-14
Siku zile amri ilitoka kwa Kaisari Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu. Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyoandikwa hapo Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. Watu wote wakaenda kuandikwa, kila mtu mjini kwao. Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba. Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni. Na katika nchi ileile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, utukufu wa Bwana ukawang'aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa katika hori ya kulia ng'ombe. Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.

Nasadiki husemwa. Wote hupiga magoti yasemwapo maneno Akapata mwili ...akawa mwanadamu.

MAOMBI
Ndugu zangu, usiku huu, Malaika wa Mungu walitangaza wokovu na amani, tumwombe Mungu atujalie sisi na watu wote amani. Ee Bwana Yesu Kristo,

1. Uliacha fahari ya mbingu na kushuka kwetu duniani: Utushirikishe heri na furaha ya mbinguni.

2. Ulijifanya binadamu na kushiriki maisha yetu ya taabu na shida: Utuimarishe kushinda magumu na makwazo ya maisha.

3. Uliunganisha mbingu na dunia: Utuvute tutamani mambo ya mbinguni zaidi kuliko yale ya duniani.

4. Malaika walitangaza amani kwa watu wenye mapenzi mema: Uwaongoze viongozi wa Serikali na Kanisa kutafuta na kutunza amani kati ya watu.

5. Ulifungua milango ya mbingu: Uwakaribishe marehemu wetu kwenye heri ya mbinguni.

Ee Mungu, Baba wa milele, uliyemtuma Mwanao hapa duniani, uyasikilize maombi yetu kwa jina la huyo Mwanao Yesu Kristo tunayemshangilia leo. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba sadaka ya sikukuu ya leo ikupendeze. Na, kwa njia ya mabadilishano haya matakatifu, tupate kushiriki umungu wake yeye, ambaye ndani yake ubinadamu wetu uko pamoja nawe. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: KUZALIWA KWA BWANA I:
(Kristo ni mwanga).

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Maana, kwa fumbo la Neno aliyetwaa mwili, mwanga mpya wa utukufu wako umetuangazia macho ya akili zetu; ili, tunapomjua Mungu katika hali ya kuonekana, kwa njia yake tuvutwe kuyapenda mambo yasiyoonekana.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.7:14
Neno alifanyika mwili, nasi tukauona utukufu wake.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana Mungu wetu, sisi tunafurahi kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwake Mkombozi wetu. Tunakuomba utujalie tuishi inavyostahili, tupate kufikia ushirika naye. Anayeishi na kutawala milele na milele.