MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Yesu Kristo ni mfalme wa wafalme: njooni, tumwabudu.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab. 95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
----------------------------
Kama Masifu yametanguliwa na Kipindi cha masomo,
anza kama ifuatavyo
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
----------------------------
UTENZI
Twamwimbia Kristo
Bwana wa viumbe vyote,
Mfalme mtawala
Wa mataifa ndo yote.
Salamu Kristo mshinda,
Ambaye tunakukiri
Peke yako watawala
Mioyo na roho zetu.
Kristo ujulikanaye
U mkuu wa amani,
Amuru ghasia zote
Za maasi na zikome;
Uwarudishe nyumbani
Kondoo walopotea,
Na milele uwatunze
Katika kundi amini.
Kwa ajili yao hao,
Mlimani Kalvari,
Ulisulibiwa Bwana
Katika mti azizi,
Ule mkuki mkali
Ambao ulikuchoma
Uliufungua moyo
Uunguao kwa pendo.
Kwa ajili yao hao,
Wajificha ewe Mungu
Katika maumbo duni
Ya mkate na divai,
Na kutoka mwili wako,
Mwili ulojeruhiwa,
Yatoka mito ya ne'ma
Wanao kuwaendea.
ANT. I: Tazameni, mtu ambaye jina lake ni 'Jua Lichomozalo';
atakalia kiti cha enzi na kutawala vyote; atayatangazia mataifa amani.
Zab.63:1-8 Hamu ya kuwa pamoja na Mungu
Mtu aliyeacha matendo ya giza, na amtafute Mungu.
Ee Mungu, wewe ni Mungu wangu;*
nakutafuta kwa moyo.
Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu,*
nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.
Nina hamu ya kukuona patakatifuni pako,*
ili nione enzi yako na utukufu wako.
Upendo wako mkuu ni bora kuliko maisha,*
kwa hiyo nitakusifu.
Nitakushukuru maisha yangu yote,*
katika sala nitainua mikono yangu.
Roho yangu itafanya karamu na kushiba vinono;*
kwa shangwe nitaimba sifa zako.
Niwapo kitandani ninakukumbuka,*
usiku kucha ninakufikiria;
maana wewe umenisaidia daima.*
Kivulini mwa mabawa yako nitashangilia.
Roho yangu inaambatana nawe kabisa,*
mkono wako wa kuume wanitegemeza.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Tazameni, mtu ambaye jina lake ni 'Jua Lichomozalo'; atakalia
kiti cha enzi na kutawala vyote; atayatangazia mataifa amani.
ANT. II: Atatukuzwa duniani kote, na yeye mwenyewe atakuwa amani.
WIMBO: Dan:3.37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Ant. II: Atatukuzwa duniani kote, na yeye mwenyewe atakuwa amani.
ANT. III: Bwana amempa mamlaka, heshima na ufalme; kila kabila na
taifa, na watu wote watamwabudu.
Zab.149 Wimbo wa ushindi
Wana wa Kanisa, taifa jipya la Mungu, watashangilia katika Kristo,
mfalme wao (Hesychius)
Mwimbieni Mungu wimbo mpya,*
msifuni kati ya jamii ya watu wake waaminifu!
Furahi, Ee Israeli, kwa sababu ya Mwumba wako,/
enyi wakazi wa Sion,*
shangilieni kwa sababu ya mfalme wenu.
Lisifuni jina lake kwa michezo,*
mwimbieni kwa ngoma na kinubi.
Mungu amependezwa na watu wake;*
yeye huwapa wanyonge ushindi.
Watu waaminifu wafurahi kwa fahari;*
washangilie hata usiku kucha.
Watangaze daima sifa kuu za Mungu,*
wakiwa na panga zenye makali kuwili mikononi mwao,
ili wawalipe kisasi watu wa mataifa,*
wawaadhibu watu wasiomjua Mungu;
wawafunge wafalme wao kwa minyororo,*
na viongozi wao kwa pingu za chuma.
kusudi watekeleze adhabu iliyoamriwa!*
Hiyo ndiyo fahari ya waaminifu wa Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Bwana amempa mamlaka, heshima na ufalme; kila kabila na
taifa, na watu wote watamwabudu.
SOMO: Ef.4:15-16
Kama tukizingatia ukweli kwa moyo wa mapendo, tutazidi katika kila jambo kulingana na Kristo,
ambaye ndiye kichwa; chini ya uongozi wake, yungo vyote vya mwili hushikamana pamoja, na mwili
wote hutegemezwa kwa msaada wa viungo yake. Basi, kila kiungo kikitekeleza kazi yake ipasavyo,
mwili wote hukua na kujijenga katika upendo.
KIITIKIZANO
K. Ee Bwana, watakatifu wako watasimulia utukufu wa utawala wako. (W. Warudie)
K. Watazungumzia uwezo wako.
W. Watasimulia utukufu wa utawala wako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Ee Bwana...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Alitufanya tuwe ufalme kwa ajili ya Mungu Baba yake; yeye ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu,
kiongozi wa wafalme wa dunia, aleluya.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Alitufanya tuwe ufalme kwa ajili ya Mungu Baba yake; yeye ni
mzaliwa wa kwanza kutoka wafu, kiongozi wa wafalme wa dunia, aleluya.
MAOMBI
Kwa imani na matumaini, tumwombe Kristo Mfalme wetu, ambaye ni wa kwanza katika vitu vyote,
na vitu vyote vimo ndani yake.
W. Bwana, utawala wako uje.
Bwana Yesu Kristo, Mungu na Mwokozi wetu, wewe ni mfalme na mchungaji wetu:
- uwaongoze watu wako wayashinde matatizo ya maisha. (W.)
Yesu, Mchungaji Mwema, uliutoa uhai wako kwa ajili ya kondoo wako:
- utuongoze tutumie vema fursa tuzipatazo ili tunufaike. (W.)
Yesu, Mkombozi wetu, wewe ni mfalme wa ulimwengu mzima:
- uvikamilishe vitu vyote ndani yako. (W.)
Yesu, mfalme wa wanadamu wote, ulifika ulimwenguni kuushuhudia ukweli:
- uwafanye binadamu watambue ukuu wako katika vitu vyote. (W.)
Yesu, mwalimu na mfano wetu, umetuweka chini ya utawala wako:
- utusaidie tuweze kutoa mfano wa maisha yasiyo na hatia, maisha matakatifu na yanayolingana
na hadhi yako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, umependa kuunganisha ulimwengu mzima katika Mwanao mpendwa, Yesu
Kristo, Mfalme wa mbingu na dunia. Uvijalie viumbe vyote uhuru, na uviwezeshe kutukuza na
kutumikia enzi yako milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.