Generic placeholder image

SHEREHE YA YESU KRISTO MFALME
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI
Salaamu Mkombozi,
Ewe Mungu Mfalme!
Kuhani, Mwana Kondoo,
Kiti cha enzi ni chako,
Utawala wako Bwana
Milele hautakoma,
U Mkuu wa amani
Inayodumu milele.

W. Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'

Jina lako Mfalme
Lasisimua viumbe,
Tawala akili zetu,
Mioyo, utashi wetu,
Hadi katika amani
Ambapo kila taifa
Litaimba zako sifa
Mfalme wa wafalme.

W. Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'

Mfalme mtakatifu,
Mfalme wa ukweli,
Uwaongoze wanyonge,
Vijana uwaongoze;
Kristo wewe Mfalme
Wa utukufu mwangavu,
Uwe kwetu sisi nuru
Inayong'ara milele.

W. Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'

Mfalme - Mchungaji
Kwenye milima mikali,
Uwarudishe nyumbani
Kondoo walopotea;
Kundi moja la kifalme-
Uzihifadhi kundini-
Nchi na falme zote
Mpya na zile za kale.

W. Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'

ANT. I: Ataitwa 'Msuluhishi', na kiti chake cha enzi kitadumu milele.

Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!.

Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.

Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!

Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.

Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;

lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.

Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,

na kumweka pamoja na wakuu:*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.

Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Ataitwa 'Msuluhishi', na kiti chake cha enzi kitadumu milele.

ANT. II: Utawala wake ni wa milele; watawala wote watamtumikia na kumtii.

Zab.117 Kumsifu Mungu
Enyi mataifa yote, msifuni Mungu,*
Enyi watu wote, msifuni!

Upendo wake mkuu kwetu ni thabiti;*
na uaminifu wake wadumu milele!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Utawala wake ni wa milele; watawala wote watamtumikia na kumtii.

ANT. III: Kristo amepewa mamlaka na utukufu wa kifalme; kila kabila na taifa, na watu wote watamtumikia milele.

WIMBO: Ufu.4:11;5:9,10,12
Wewe ni Bwana na Mungu wetu,*
Unastahili utukufu na heshima na nguvu;

maana wewe uliumba vitu vyote,/
na kwa matakwa yako*
kila kitu kimepewa uhai na uzima.

Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu*
na kuivunja mihuri yake,

kwa sababu wewe umechinjwa,/
na kwa damu yako umemnunulia Mungu*
watu kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani/
wamtumikie Mungu wetu,*
nao watatawala duniani.

Mwana - kondoo aliyechinjwa*
anastahili kupokea

uwezo, utajiri, hekima,*
nguvu, heshima, utukufu na sifa.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Kristo amepewa mamlaka na utukufu wa kifalme; kila kabila na taifa, na watu wote watamtumikia milele.

SOMO: Ef.1:20-23
Mungu alimfufua Kristo kutoka wafu, akamketisha kulia kwake mbinguni. Huko, Kristo anatawala juu ya kila utawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao. Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa, akiwa ndio mkuu wa vitu vyote. Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.

KIITIKIZANO
K. Enzi na nguvu ni vyako; Bwana, utawala ni wako. (W. Warudie)
K. Wewe ni mtawala wa vyote.
W. Bwana, utawala ni wako.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Enzi...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake; atautawala ukoo wa Yakobo milele, na utawala wake hautakuwa na mwisho, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake; atautawala ukoo wa Yakobo milele, na utawala wake hautakuwa na mwisho, aleluya.

MAOMBI
Kwa imani na matumaini, tumwombe Kristo MfaIme wetu, ambaye ni wa kwanza katika vitu vyote, na vitu vyote vimo ndani yake.
W. Bwana, utawala wako uje.

Bwana Yesu Kristo, mfalme wetu na mchungaji wetu, uwakusanye kondoo wako kutoka kila pembe ya dunia:
- uwachunge katika malisho yako yenye majani mabichi. (W.)

Yesu, kiongozi na Mwokozi wetu, uwafanye watu wote wawe wako; uwaponye wagonjwa, uwatafute waliopotea, uwahifadhi wenye nguvu:
- uwarudishe wanaotangatanga, uwakusanye pamoja wale waliotawanyika, na uwatie matumaini mapya waliovunjika moyo. (W.)

Yesu, hakimu wa milele, utakapomkabidhi Baba yako utawala wako, utukumbuke sisi, taifa lako aminifu:
- utuwezeshe kuurithi ufalme tuliotayarishiwa toka mwanzo wa ulimwengu. (W.)

Yesu, mfalme wa amani, ondoa uroho katika mioyo ya watu, uroho ambao husababisha vita:
- liambie taifa lako maneno ya amani. (W.)

Yesu, mrithi wa mataifa yote, uwaweke binadamu wote chini ya utawala wa Kanisa lako, ulilokabidhiwa na Baba:
- wafanye watu wote wakukiri wewe kuwa ni kichwa, katika utoaji wa Roho Mtakatifu. (W.)

Yesu, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, na wa kwanza kuzaliwa kutoka wafu:
- uwafikishe marehemu wote kwenye utukufu wa ufufuko wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, umependa kuunganisha ulimwengu mzima katika Mwanao mpendwa, Yesu Kristo, Mfalme wa mbingu na dunia. Uvijalie viumbe vyote uhuru, na uviwezeshe kutukuza na kutumikia enzi yako milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.