MASIFU YA JIONI II
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Salaamu Mkombozi,
Ewe Mungu Mfalme!
Kuhani, Mwana Kondoo,
Kiti cha enzi ni chako,
Utawala wako Bwana
Milele hautakoma,
U Mkuu wa amani
Inayodumu milele.
W.
Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'
Jina lako Mfalme
Lasisimua viumbe,
Tawala akili zetu,
Mioyo, utashi wetu,
Hadi katika amani
Ambapo kila taifa
Litaimba zako sifa
Mfalme wa wafalme.
W.
Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'
Mfalme mtakatifu,
Mfalme wa ukweli,
Uwaongoze wanyonge,
Vijana uwaongoze;
Kristo wewe Mfalme
Wa utukufu mwangavu,
Uwe kwetu sisi nuru
Inayong'ara milele.
W.
Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'
Mfalme - Mchungaji
Kwenye milima mikali,
Uwarudishe nyumbani
Kondoo walopotea;
Kundi moja la kifalme-
Uzihifadhi kundini-
Nchi na falme zote
Mpya na zile za kale.
W.
Watakatifu, malaika
Na mataifa waimba:
'Asifiwe Yesu Kristo,
Mfalme wetu na Bwana
Wa uzima na dunia,
Wa mbingu na wa bahari,
Mfalme wa upendo
Mlimani Kalvari.'
ANT. I: Atakalia kiti cha enzi cha Daudi, na atatawala ufalme
wake milele, aleluya.
Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini
ya miguu yake (Kor.15:25)
Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,
Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."
Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"
Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.
Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.
Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."
Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.
Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Atakalia kiti cha enzi cha Daudi, na atatawala ufalme
wake milele, aleluya.
ANT. II: Ufalme wako ni wa milele; Bwana, utawala wako wadumu
kizazi hata kizazi.
Zab.145:1-13 Wimbo wa kumsifu Mungu
Nitakutukuza, Ee Mungu wangu na mfalme wangu;*
nitalitukuza jina lako daima na milele.
Nitakushukuru kila siku;*
nitalisifu jina lako daima na milele.
Mungu ni mkuu, astahili kusifiwa sana;*
ukuu wake hauwezi kuelezeka.
Matendo yako yatatukuzwa kizazi hata kizazi,*
watu watatangaza matendo yako ya enzi.
Watanena juu ya utukufu na fahari yako,*
nami nitatafakari matendo yako ya ajabu.
Watu watanena juu ya matendo yako ya kutisha,*
nami nitatangaza ukuu wako.
Watatangaza sifa za wema wako mwingi,*
na kuimba juu ya uadilifu wako.
Mungu ni mwema na mwenye huruma,*
hakasiriki ovyo, amejaa upendo mkuu.
Mungu ni mwema kwa wote,*
ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote.
Ee Mungu, viumbe vyote vitakushukuru,*
nao waaminifu wako watakutukuza.
Watanena juu ya utukufu wa utawala wako,*
na kutangaza juu ya enzi yako kuu,
ili kila mtu ajue matendo yako makuu,*
na fahari tukufu ya utawala wako.
Utawala wako ni utawala wa milele;*
mamlaka yako yadumu vizazi vyote.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Ufalme wako ni wa milele; Bwana, utawala wako wadumu
kizazi hata kizazi.
ANT. III: Katika joho lake na paja lake paliandikwa jina: Mfalme
wa wafalme, na Bwana wa mabwana. Atukuzwe na kuheshimiwa daima na milele.
WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo
Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).
Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).
ANT. III: Katika joho lake na paja lake paliandikwa jina: Mfalme
wa wafalme, na Bwana wa mabwana. Atukuzwe na kuheshimiwa daima na milele.
SOMO: 1Kor.15:25-28
Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake.
Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo. Maana Maandiko yasema: "Mungu ataweka kila kitu chini
ya miguu yake." Lakini, Maandiko yanaposema: 'Kila kitu kitawekwa chini ya miguu yake' ni dhahiri
kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya
Kristo. Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya Utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka
chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya Utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote.
KIITIKIZANO
K. Utawala wako, Ee Mungu, utadumu milele na milele. (W. Warudie)
K. Utawala wako ni utawala wa haki.
W. Utadumu milele na milele.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utawala...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani, asema Bwana.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani, asema Bwana.
MAOMBI
Kwa imani na matumaini, tumwombe Kristo Mfalme wetu, ambaye ni wa kwanza katika vitu vyote,
na vitu vyote vimo ndani yake:
W. Bwana, utawala wako uje.
Bwana Yesu Kristo, mfalme wetu na mchungaji wetu, uwakusanye kondoo wako kutoka kila pembe ya dunia:
- uwachunge katika malisho yako yenye majani mabichi. (W.)
Yesu, kiongozi na Mwokozi wetu, uwafanye watu Wote wawe wako; uwaponye wagonjwa, uwatafute
waliopotea, uwahifadhi wenye nguvu:
- uwarudishe wanaotangatanga, uwakusanye pamoja wale waliotawanyika, na uwatie matumaini
mapya waliovunjika moyo. (W.)
Yesu, hakimu wa milele, utakapomkabidhi Baba yako utawala wako, utukumbuke sisi, taifa lako aminifu:
- utuwezeshe kuurithi ufalme tuliotayarishiwa toka mwanzo wa ulimwengu. (W.)
Yesu, mfalme wa amani, ondoa uroho katika mioyo ya watu, uroho ambao husababisha vita:
- liambie taifa lako maneno ya amani. (W.)
Yesu, mrithi wa mataifa yote, uwaweke binadamu wote chini ya utawala wa Kanisa lako, ulilokabidhiwa na Baba:
- uwafanye watu wote wakukiri wewe kuwa ni kichwa, katika umoja wa Roho Mtakatifu. (W.)
Yesu, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote, na wa kwanza kuzaliwa kutoka wafu:
- uwafikishe marehemu wote kwenye utukufu wa ufufuko wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi wa milele, umependa kuunganisha ulimwengu mzima katika Mwanao mpendwa, Yesu
Kristo, Mfalme wa mbingu na dunia. Uvijalie viumbe vyote uhuru, na uviwezeshe kutukuza na
kutumikia enzi yako milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.