BWANA WETU YESU KRISTO MFALME WA ULIMWENGU

MASOMO MWAKA B

ANTIFONA YA KUINGIA: Ufu.5:12;1:6
Astahili Mwanakondoo aliyechinjwa kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele.

KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi wa milele, umependa kuvifanya upya vitu vyote katika Mwanao mpenzi, Mfalme wa ulimwengu. Uwe radhi kuvijalia viumbe vyote, vilivyokombolewa katoka utumwani, vipate kukutumikia katika fahari yako na kukusifu bila mwisho. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele namilele.

SOMO 1: Eze.34:11-12,15-17
Bwana Mungu asema hivi; Tazama mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami mitawalaza, asema Bwana Mungu. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu. Na kwa habari zenu, Enyi kundi langu, Bwana Mungu asema hivi, Tazama, nahukumu kati ya mnyama na mnyama, kondoo waume na mbuzi waume pia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.93:1-2,5,(K)1
1. Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.

(K) Bwana ni mfalme, amejivika taji.

2. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani.
Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)

3. Shuhuda zako ni amini sana;
Utakatifu ndio uifaao nyumba yako.
Ee Bwana, milele na milele. (K)

SOMO 2: Ufu.1:5-8
Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina. Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam, Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.

SHANGILIO: Mk.11:10
Aleluya, aleluya!
Abarikiwe Yeye ajaye kwa jina la Bwana: Ubarikiwe na Ufalme ujao, wa baba yetu Daudi.
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Yn.18:33-37
Pilato aliingia ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je, wewe ni Mfalme wa Wayahudi? Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu? Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini? Yesu, akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, Mara kwa mara Yesu alieleweka vibaya alipotangaza ujio wa Ufalme wa Mungu. Wengi hata Petro walifikiri ufalme huu ni ufalme wa kidunia. Kumbe mbele ya Pilato Yesu alikiri wazi kabisa, kwamba ufalme wake si wa dunia hii. Ee Bwana Yesu,

1. Mbele ya Pilato ulikiri kwamba ufalme wako si wa dunia hii. Utusaidie kuelewa kwamba ufalme wako ni ufalme wa haki, amani na upole.

2. Utawale maisha yetu na kuziongoza familia zetu.

3. Wewe hukuogopa kusema ukweli mbele ya gavana wa Roma. Utuimarishe tusiogope kusema ukweli na haki mbele ya watu wote, wakubwa na wadogo.

4. Wewe ulikuwa tayari kutoa maisha yako kwa ajili ya ukweli wa kimungu. Utupe moyo kishujaa wa kutetea ukweli wa imani hata kuhatarisha maisha yetu.

5. Uwapokee marehemu wote katika enzi ya ufalme wako wa milele.

Ee Mungu Baba, Mwana wako aliyetangaza Ufalme wako, ni mfalme wetu. Utusaidie kumkimbilia yeye katika kila shida na hatari. Tunaomba hayo kwa njia yake yeye anayeishi na kutawala katika ufalme wako daima na milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, huku tukikutolea kafara ya upatanisho wa wanadamu wote, tunakusihi kwa unyenyekevu ili Mwanao mwenyewe awajalie mataifa yote zawadi za umoja na amani. Anayeishi na kutawala milele na milele.

UTANGULIZI
Kristo mfalme wa ulimwengu

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele.
Wewe ulimpaka mafuta ya furaha Mwanao pekee, Yesu Kristo Bwana wetu, awe Kuhani wa milele na Mfalme wa ulimwengu wote.
Alijitoa mwenyewe juu ya altare ya msalaba awe kafara safi iletayo amani, ili atimize mafumbo ya ukombozi wa watu.
Kwa kuviweka viumbe vyote chini ya utawala wake amekutolea wewe Mungu mkuu ufalme wa milele na wa ulimwengu wote; ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, upendo na amani.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na pamoja na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ...

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.29:10,11
Bwana ameketi hali ya mfalme milele; Bwana atawabariki watu wake kwa amani.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Baada ya kupokea chakula cha uzima wa milele, tunakuomba, ee Bwana, ili sisi, tunaoona fahari kuzitii amri za Kristo Mfalme wa ulimwengu, tuweze kuishi bila mwisho pamoja naye katika ufalme wa mbinguni. Anayeishi na kutawala milele na milele.