SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ee fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu
Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Bwana ni hakimu wetu, Bwana anatutungia sheria zetu,
Bwana ni mfalme wetu; yeye ndiye atakayetuokoa.
Adhuhuri
ANT.: Maji ya uzima yatatiririka kutoka Yerusalemu, na Bwana,
mfalme wa dunia nzima, atatawala.
Baada ya Adhuhuri
ANT.: Milki yake ni kuu, yenye amani isiyo na mwisho.
Zab.118 Sala ya shukrani
Huyu ndiye lile jiwe mlilokataa ninyi waashi, ambalo sasa limekuwa jiwe kuu la msingi
(Mate.4:11)
I
Mshukuruni Mungu, kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Watu wa Israeli waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wazao wa Aroni waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Wote wamchao Mungu waseme:*
"Upendo wake mkuu ni wa milele."
Katika taabu yangu nilimlilia Mungu,*
naye akanisikiliza na kuniokoa.
Mungu yuko nami, siogopi kitu;*
mwanadamu atanifanya nini?
Mungu yuko nami, ananisaidia;*
nami nitashuhudia kushindwa kwa adui zangu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kumtegemea mwanadamu.
Ni afadhali kumtumainia Mungu,*
kuliko kuwategemea viongozi wa dunia.
Watu wote wasiomjua Mungu walinizingira,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Walinizunguka kila upande,*
lakini kwa nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Walinivamia kwa wingi kama nyuki,/
lakini wakateketea kama kichaka motoni;*
kwangu nguvu ya Mungu nikawapondaponda.
Nilishambuliwa mno karibu nishindwe,*
lakini Mungu alinisaidia.
Mungu hunijalia nguvu na uhodari;*
yeye mwenyewe aminiokoa.
Sikilizeni sauti za furaha na ushindi/
katika mahema ya watu waadilifu;*
"Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!
Mkono wa Mungu umeleta ushindi!*
Mkono wa Mungu umetenda mambo ya ajabu!"
Sitakufa, bali nitaishi,*
na kutangaza matendo ya Mungu.
Mungu ameniadhibu sana,*
lakini hakuniacha nife.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
III
Nifungulie milango ya Hekalu;*
nitaingia na kumshukuru Mungu!
Huu ndio mlango wa Mungu,*
ambao waadilifu waweza kupitia.
Nakushukuru, Ee Mungu, kwa kunisikiliza;*
kwa sababu wewe umeniokoa.
Jiwe walilolikataa waashi,*
limekuwa jiwe kuu la msingi.
Jambo hili limefanywa na Mungu;*
nalo ni jambo la ajabu mno kwetu.
Hii ndiyo siku aliyoifanya Mungu;*
basi, tushangilie na kufurahi.
Utuokoe, Ee Mungu, utuokoe!*
Ee Mungu, tunakusihi, utupe fanaka!
Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Mungu!*
Twakubariki toka nyumbani mwa Mungu.
Mungu ni Mungu, naye ni mwema kwetu./
Shikeni matawi mikononi, anzeni sherehe,*
mkiandamana mpaka madhabahuni.
Ndiwe, Mungu wangu, ninakushukuru*
ninakutukuza, Ee Mungu wangu.
Mshukuruni Mungu kwa kuwa ni mwema,*
kwa maana upendo wake mkuu ni wa milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Kabla ya Adhuhuri
ANT.: Bwana ni hakimu wetu, Bwana anatutungia sheria zetu,
Bwana ni mfalme wetu; yeye ndiye atakayetuokoa.
Adhuhuri
ANT.: Maji ya uzima yatatiririka kutoka Yerusalemu, na Bwana,
mfalme wa dunia nzima, atatawala.
Baada ya Adhuhuri
ANT.: Milki yake ni kuu, yenye amani isiyo na mwisho.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Kol.1:12-13
Kwa furaha, mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale Mungu
aliyowawekea watu wake katika Utawala wa mwanga. Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,
akatuleta salama katika Utawala wa Mwanae mpenzi.
K. Bwana, mfalme, atatawala milele.
W. Bwana atawajalia watu wake amani.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Kol.1:16b-18
Vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake. Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote,
na, kwa kuungana naye, kila kitu hudumu mahali pake. Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani
kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa
katika wafu, ili yeye peke yake awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote.
K. Mwimbieni mfalme wetu, imbeni tenzi.
W. Yeye ni mfalme wa dunia yote.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Kol.1:19-20
Mungu mwenyewe aliamua kwamba Mwana anao ukamilifu wote wa kimungu ndani yake. Basi, kwa
njia yake, Mungu aliamua kuupatanisha ulimwengu wote naye. Kwa damu ya Kristo msalabani
Mungu alifanya amani, na hivyo akavipatanisha naye vitu vyote duniani na mbinguni.
K. Furahini mbele ya Bwana, mfalme wetu.
W. Amekuja kuitawala dunia.
SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi wa milele, umependa kuunganisha ulimwengu mzima katika Mwanao mpendwa,
Yesu Kristo, Mfalme wa mbingu na dunia. Uvijalie viumbe vyote uhuru, na uviwezeshe kutukuza
na kutumikia enzi yako milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) Tumshukuru Mungu.