KOMUNYO YA WAGONJWA

Generic placeholder image
Kumunyo ya Wagonjwa

Chumba cha mgonjwa kiwe safi. Iwekwe meza au sanduku lililofunikwa kwa kitambaa safi cheupe cha kuwekea Sakramenti. Maji ya baraka yakitumiwa, pawepo na chombo, mrashi au kitawi kidogo. Ni vema pia kuwasha mishumaa miwili.

P: Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu:
W: Amina.

Kusalimu
Padri anamsalimu mgonjwa na wote waliopo kwa kufuata mazingira:
Amani kwa nyumba hii na kwa wote wanaokaa humu.

Halafu, anamnyunyizia mgonjwa na chumba maji ya baraka, akisema:
P: Maji haya yawe ukumbusho wa Ubatizo uliopokelewa na yawe ukumbusho wa Kristo aliyetukomboa sisi kwa Mateso na Ufufuko wake.

Kisha anaweka Hostia takatifu juu ya meza na wote wanaiabudu.

Majuto
Tendo la toba linafanyika kama ilivyo katika kanuni ya Misa.
P: Ndugu zangu, tukiri dhambi zetu, ili tupate kustahilishwa kuadhimisha mafumbo matakatifu.
Husubiri kidogo. Kisha wanasema pamoja:
Namwungamia Mungu mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kwa kutotimiza wajibu: nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana namwomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi, ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.

P: Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele.
W: Amina.

Sala ya Bwana
P: Kwa kulitii agizo la Mwokozi wetu, na tukifuata mafundisho yake ya kimungu, tunathubutu kusema:

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike;
utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni.
Amina.

Sehemu ya maandiko matakatifu yaweza kusomwa na Padri au mtu mwingine.

MASOMO YA BIBLIA
1: Mt.11:25-30
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyo kupendeza mbele zako. Akasema, nimekabidhiwa vyote na Baba yangu; wala hakuna amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia.
Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.

2: Mt.25:31-40
Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.

Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.
Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.
Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.

3: Mk.16:15-20
Wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.

Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Marko.
Yesu akawaambia wafuasi wake, Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.
Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo

4: Lk.10:5-6,8-9
Wapozeni wagonjwa

Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Luka.
Na nyumba yoyote mtakoyoingia, semeni kwanza, Amani iwemo nyumbani humu; na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu. Na mji wowote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu; wapozeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa Mungu umewakaribia.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.

5: Lk.10:25-37
Ni nani aliyekuwa jirani?

Somo la Injili Takatifu ilvyoandikwa na Luka.
Na tazama, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.
Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang'anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.
Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia katika wanyanganyi? Akasema ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.

6: Lk.11:5-10
Nami nawaambia, ombeni nanyi mtapewa; kwa kuwa kila aombaye hupokea.

Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Luka.
Akawaambia, ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake; na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe? Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.
Nami nawaambia, ombeni nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.
Neno la Bwana
W: Sifa kwako, ee Kristo.

KOMUNYO
Kisha Padri anamwonesha mgonjwa Hostia takatifu, akisema:
Tazama, Mwanakondoo wa Mungu,
tazama, aondoaye dhambi za ulimwengu.
Heri yao walioalikwa kwenye karamu ya Mwanakondoo.

Mgonjwa na wale waliopo wanasema mara moja:
Ee Bwana, sistahili uingie kwangu,
lakini sema neno tu, na roho yangu itapona.

Hapo Padri anamwendea mgonjwa, anamwonesha Hostia takatifu anayoishika mkononi ameinua juu kidogo, akisema:
Mwili wa Kristo
Mgonjwa anajibu: Amina.
na kupokea Komunyo. Halafu wengine wanaotaka wanapokea Komunyo kama kawaida.

Sala ya kumalizia
Baada ya kusafisha vyombo, Padri anasema sala.
Tuombe. Ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu Mwenyezi wa milele, tunakuomba kwa imani, ili Mwili mtakatifu sana (na Damu takatifu sana) ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, aliopokea ndugu yetu (dada) umfae kwa mwili na roho kuufikia uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa imani na kwa jina la Yesu Kristo, anayeishi na kutawala pamoja nawe milele na milele.
W: Amina.

Baraka
Kisha Padri anambariki mgonjwa na hao waliopo, kama kawaida:
Awabariki Mungu mwenyezi, Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W: Amina.