MPAKO WA WAGONJWA

Generic placeholder image
Mpako wa wagonjwa


Maandalizi kwa adhimisho
Kila inapowezekana Padri amwungamishe mgonjwa kabla ya kutoa Mpako. Kama mgonjwa haungami, tendo la toba laweza kufanywa wakati wa kutoa Mpako, kama ilivyo katika kanuni ya Misa.

MWANZO WA ADHIMISHO
P: Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu:
W: Amina.

Padri anamsalimu mgonjwa kirafiki. Anaweza kutumia salamu hii:
Amani kwa nyumba hii, na kwa wote wanaokaa humu.

Halafu, anamnyunyizia mgonjwa na chumba maji ya baraka, akisema:
Maji haya yatukumbushe ubatizo wetu katika Kristo, aliyetukomboa kwa kifo na ufufuko wake.

Kisha anaweka Hostia takatifu juu ya meza na wote wanaiabudu.

Wimbo
Ninakulilia katika unyonge wangu,
Ewe kinga yangu.
Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia;
Bwana, uisikie sauti yangu.
Masikio yako na yaisikilize sauti ya dua zangu.
Bwana, haja zangu zote ziko mbele zako,
kuugua kwangu hakukusitirika kwako.
Wewe, Bwana, usiniache,
Mungu wangu, usijitenge nami.
Kwa maana mimi ni karibu na kusita,
na maumivu yangu yako mbele yangu daima.

Kisha, Padri akiwaelekea wote waliopo, anasema maneno kama haya:
Ndugu wapendwa, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye katika Injili wagonjwa walimwendea kuomba uponyaji, na ambaye ameteswa sana kwa ajili yetu, yupo kati yetu, katika jina la waliokusanyika, akiagiza kwa njia ya Mtume Yakobo: "Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa Kanisa, nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa". Basi, tumkabidhi ndugu (dada) yetu mgonjwa kwa neema na nguvu ya Kristo, ili apate nafuu na usalama.

Tendo la toba
Iwapo mgonjwa hakuungama mwanzoni, Padri anawaalika mgonjwa na wale waliopo washiriki tendo la toba:
Ndugu zangu, tukiri dhambi zetu, ili tupate kustahilishwa kuadhimisha mafumbo matakatifu.
Husubiri kidogo
Namwungamia Mungu mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kwa kutotimiza wajibu: nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana namwomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.

Padri anaendelea:
Mungu mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele.
W. Amina.

LITURUJIA YA NENO
INJILI Mt.8:5-10,13
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia, akamsihi, akisema; "Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana.” Yesu akamwambia: "Nitakuja, nimponye." Yule akida akamjibu, akasema: “Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu, lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu 'Nenda,' huenda; na huyu 'Njoo', huja; na mtumwa wangu fanya hivi,' hufanya. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata: "Amin, nawaambieni, sijaona imani kubwa namna hii, kwa yeyote katika Israeli."
Naye Yesu akamwambia yule akida: "Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini." Mtumishi wake akapona saa ileile.
Neno la Bwana.
W. Sifa kwako, ee Kristo

Padri akiona inafaa, atoe homilia fupi juu ya hayo yaliyosomwa. Wote watafakari neno la Mungu na kuimba wimbo ufaao, kwa mfano huu ufuatao.

WIMBO: Zab.62:1-2;7-8(K)5

(K) Tumaini letu ni kwa Bwana.

Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya,
wokovu wangu hutoka kwake.

Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu,
ngome yangu, sitatikisika sana.

Kwa Mungu wokovu wangu, na utukufu wangu;
mwamba wa nguvu zangu,
na kimbilio langu ni kwa Mungu.

Enyi watu, mtumainini sikuzote,
Mungu ndiye kimbilio letu.

Iwapo hali ya mgonjwa inaruhusu, Litania fupi yaweza kusemwa. Mgonjwa akiweza, anaitika pamoja na watu waliopo.

Litania
Ndugu zangu, kwa unyenyekevu, tumwombe sana Bwana kwa sala ya imani yetu, tumsihi kwa ajili ya huyu ndugu (dada) yetu F. Upende, Ee Bwana, kumfikia kwa huruma na kumtuliza kwa Mpako Mtakatifu.
W. Twakuomba utusikie.

Upende kumuokoa na uovu wowote.
W. Twakuomba utusikie.

Upende kuyapunguza mateso ya wagonjwa wote wanaolala hapa.
W. Twakuomba utusikie.

Upende kuwasaidia hao wanaotoa huduma kwa wagonjwa wanaotakiwa kutunzwa.
W. Twakuomba utusikie.

Upende kumuokoa na dhambi na majaribu yoyote.
W. Twakuomba utusikie.

Upende kumjalia uzima na wokovu huyo tunayemuwekea mikono kwa jina lako.
W. Twakuomba utusikie.

MPAKO WENYEWE

Kuweka mikono

Padri anaweka mikono yake juu ya kichwa cha mgonjwa bila kusema neno.

------------------
Kubariki mafuta
Ikiwa inahitajika kubariki mafuta, Padri anasema
Tuombe:
Ee Mungu, Baba wa faraja zote, umependa kuponya maradhi ya wagonjwa kwa njia ya Mwanao. Tunaomba usikilize kwa wema sala yetu sisi tunaokuamini. Umpeleke Roho wako Mtakatifu Mfariji kutoka mbinguni ashuke katika Mafuta haya uliyotaka yatoke katika mti mbichi, yawanufaishe wanadamu mwilini. Nayo baraka + yako iwashukie watakaopakwa mafuta haya ili yawaondolee maumivu yote, maradhi na magonjwa yote; yawakinge mwilini, akilini na rohoni mwao. Basi, ee Bwana, uyabariki kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo mafuta yako haya kwa matumizi yetu. Anayeishi na kutawala nawe milele na milele.
W. Amina.

Mafuta yakishabarikiwa, Sala ya kushukuru juu ya mafuta inaweza kusemwa:
Utukuzwe Ee Mungu, Baba Mwenyezi, uliyemtuma Mwana wako duniani kwa ajili yetu sisi na kwa ajili ya wokovu wetu.
W. Utukuzwe ee Mungu.

Utukuzwe Ee Mungu, Mwana pekee, uliyependa kuponya maradhi yetu, ukashuka kwetu sisi watu.
W. Utukuzwe ee Mungu.

Utukuzwe Ee Mungu Roho Mtakatifu Mfariji, unayetujalia nguvu ya kuvumilia kihodari mateso ya mwili wetu.
W. Utukuzwe ee Mungu.

Mtumishi wako, Ee Bwana, anayepakwa Mafuta Matakatifu katika imani, astahili kupata nafuu katika mateso yake na kutulizwa katika maradhi yake. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
------------------

Mpako Mtakatifu
Kisha Padri anachukua mafuta, anampaka mgonjwa katika paji la uso, akisema:
Kwa Mpako huu mtakatifu na kwa huruma yake kuu, Bwana akusaidie kwa neema ya Roho Mtakatifu.
W. Amina.

Kisha Padri anampaka mafuta mikononi, akisema:
Na Yeye mwenyewe anayekuondolea dhambi, kwa wema wake akupe nafuu na kukujalia afya.
W. Amina.

Tuombe. Ee Mkombozi wetu, twakuomba, ponya maradhi ya mgonjwa huyu kwa neema ya Roho Mtakatifu; ponya na majeraha yake na umwondolee dhambi zake, uyatoe toka kwake mateso yote ya mwili na ya roho, umrudishie kwa huruma yako afya kamili kwa ndani na nje, ili baada ya kuponywa kwa kazi ya huruma yako, arudie kazi zake za zamani. Unayeishi na kutawala milele na milele.
W. Amina.

MWISHO WA ADHIMISHO
Padri anawaalika wote kwa maneno kama haya:
Na sasa tumwombe Mungu kwa pamoja kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyotufundisha kusali.

Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike;
utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni.
Amina.

Ikiwa mgonjwa hakomuniki:


Ikiwa mgonjwa anakomunika, hapo ndipo nafasi.
------------
KOMUNYO
Kisha Padri anamwonesha mgonjwa Hostia takatifu, akisema:
Tazama, Mwanakondoo wa Mungu,
tazama, aondoaye dhambi za ulimwengu.
Heri yao walioalikwa kwenye karamu ya Mwanakondoo.

Mgonjwa na wale waliopo wanasema mara moja:
Ee Bwana, sistahili uingie kwangu,
lakini sema neno tu, na roho yangu itapona.

Hapo Padri anamwendea mgonjwa, anamwonesha Hostia takatifu anayoishika mkononi ameinua juu kidogo, akisema:
Mwili wa Kristo
Mgonjwa anajibu: Amina.
na kupokea Komunyo. Halafu wengine wanaotaka wanapokea Komunyo kama kawaida.
Baada ya kusafisha vyombo, Padri anaendelea na baraka.

-------------
BARAKA
Kisha Padri anambariki mgonjwa:
Mungu Baba akubariki.
W. Amina.

Mwana wa Mungu akuponye.
W. Amina.

Roho Mtakatifu akuangaze.
W. Amina.

Aulinde mwili wako na aiokoe roho yako.
W. Amina.

Autakase moyo wako na akufikishe kwenye uzima wa milele.
W. Amina.

Kisha Padri anawabariki wote waliopo:
Nanyi nyote mliopo hapa pamoja, awabariki Mungu mwenyezi, Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Amina.