UBATIZO

Generic placeholder image
UBATIZO WA WATOTO WENGI


KUWAPOKEA WATOTO
Waamini wanaimba zaburi au wimbo mwingine na Padri au shemasi mwenye kubatiza, anaandamana na watumishi amevaa alba au kota na stola na hata joho. Anafika mbele ya mlango wa Kanisa au mahali pengine Kanisani walipokusanyika wazazi na wasimamizi pamoja na watoto wa kubatizwa. Padri anawasalimu watu waliopo, hasa wazazi na wasimamizi. Kwa maneno machache anawakumbusha furaha ya wazazi hao waliopata watoto kama zawadi ya Mungu aliye asili ya uzima wa wote, mwenye kutaka kuwapa sasa uzima wake mwenyewe. Kisha anawauliza wazazi na wasimamizi wote pamoja:

MWANZO WA ADHIMISHO
P: Mnawaombea nini watoto wenu katika Kanisa la Mungu?
Familia zote pamoja:
W: Ubatizo

Kisha Padri anawaambia kwanza wazazi:
Wajibu wa wazazi ni kuwafundisha watoto wao imani, wapate kushika amri za Mungu, na kuwapenda wanadamu wenzao, kama Kristo alivyotufundisha. Je, ninyi wazazi, mwafahamu wajibu huo?
Wazazi wote pamoja:
W: Twafahamu.

Kisha Padri anawaelekea wasimamizi wote, anawauliza:
Nanyi wasimamizi, je, mko tayari kuwasaidia wazazi wa watoto hawa katika wajibu wao?
Wasimamizi wote pamoja:
W: Tuko tayari.

Padri anaendelea kusema:
Wanangu, jamii hii ya wakristo inawapokea ninyi kwa furaha kubwa. Nami nawatia ishara ya msalaba kwa jina lao.
Padri anamtia kila mtoto ishara ya msalaba katika paji la uso. Kisha anawaambia wazazi wafanye vilevile, na hata likifaa hata wasimamizi.
Nanyi wazazi (na wasimamizi), watieni watoto wenu ishara ya msalaba wa Kristo Mwokozi katika paji la uso.

NENO LA MUNGU
Somo na Hotuba

Padri anawaalika wazazi na wasimamizi na wote waliopo washiriki katika ibada ya neno la Mungu.

MASOMO YA BIBLIA
AGANO LA KALE
1. Tumepewa moyo mpya Eze.36:24-28
Maji ya Ubatizo husafisha mioyo yetu, iliyo migumu, yenye dhambi na ukosefu wa mapendo. Mioyo yetu inageuka kuwa mipya, yenye kumpenda Mungu na kushika amri zake.
Somo la kitabu cha Nabii Ezekieli
Bwana Mungu asema hivi: Nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe, uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
Neno la Bwana
W. Tumshukuru Mungu

AGANO JIPYA
2. Tumepewa uzima mpya Rum.6:3-5
Tendo la Ubatizo huonesha wazi kwamba kwa Ubatizo tumekataa dhambi, na tumepewa uzima wa milele. Kutiwa ndani ya maji ni kama kuzikwa pamoja na Kristo, na kuopolewa toka majini ni kama kufufuka pamoja naye katika uzima mpya wa kikristo.
Somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi.
Ndugu zangu, Sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake. Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya Ubatizo katika mauti yake, Kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake.
Neno la Bwana
W.Tumshukuru Mungu

AU
3. Sisi ni waana wa Mungu Rum.8:28-32
Kwa Ubatizo, Mungu ametupokea kama wana wake katika Kristo.
Somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi.
Ndugu zangu, twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki hao akawatukuza. Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?
Neno la Bwana
W. Tumshukuru Mungu

AU
4. Mwili wa mtu kama mfano wa umoja wa Kristo na wakristo 1Kor.12:12-13
Kwa Ubatizo tumeunganishwa na Kristo katika umoja wa imani na wa mapendo.
Somo la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa
Wakorintho. Ndugu zangu, kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani, ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Neno la Bwana
W. Tumshukuru Mungu

INJILI
5. Amri kuu ya upendo Mt.22:35-40
Bwana Yesu ametufundisha kwamba amri zote za kikristo zinatokana na amri kuu ya mapendo. Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kumpenda jirani kwa ajili ya Mungu, ndio ukamilifu wa kikristo.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Siku zile, mmoja wa Mafarisayo, mwanasheria, akamwuliza Yesu, akimjaribu: Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako,ee Kristo

AU
6. Yesu awatuma mitume kufundisha watu wote Injili Mt.28:18-20
Bwana Yesu aliwatuma Mitume wake duniani kote, wakawaingize watu wa mataifa yote katika Kanisa lake. Kwa njia ya Ubatizo.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Siku zile, Yesu akaja kwa mitume, akasema nao akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kushika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako,ee Kristo

AU
7. Yesu anabatizwa Mk.1:9-11
Ubatizo wa Yesu katika Yordani ni mfano wa Ubatizo wetu: katika Ubatizo tunageuka kuwa wana wa Mungu Baba na tunampokea Roho Mtakatifu.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Marko.
Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohane katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, nimependezwa nawe.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako,ee Kristo

AU
8. Yesu na watoto wadogo Mk.10:13-16
Amin, nawaambieni, yeyote asiyekubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Marko.
Siku zile, walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao, Amin, nawaambieni, yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako,ee Kristo

AU
9. Kubatizwa ni kuzaliwa tena Yn.3:1-6
Ubatizo ni kweli kuzaliwa mara ya pili, na kupewa uzima wa milele na kuingia katika Ufalme wa Mungu.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Yohane.
Palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

Baada ya somo, Padri anatoa hotuba fupi juu ya yale yaliyosomwa, na kuzidi kuwafahamisha watu waliopo fumbo la Ubatizo, na kuwahimiza wazazi na wasimamizi wapokee wajibu wao kwa furaha.

Sala za Waamini
Padri anasema:
Ndugu zangu, tumwombe Bwana wetu Yesu Kristo awashushie rehema yake watoto hawa watakaopata neema ya Ubatizo, wazazi wao na wasimamizi, nao wote waliobatizwa.

Msomaji: Kwa fumbo takatifu la kifo na ufufuko wako, upende kuwajalia watoto hawa uzima mpya kwa Ubatizo na kuwakusanya katika Kanisa lako takatifu.
W. Twakuomba, utusikie.

Msomaji: Kwa Ubatizo na Kipaimara, upende kuwafanya wawe wafuasi wako waaminifu na mashahidi wa Injili yako.
W. Twakuomba, utusikie.

Msomaji: Kwa utakatifu wa maisha yao, upende kuwafikisha kwenye furaha za ufalme wa mbinguni.
W. Twakuomba, utusikie.

Msomaji: Upende kuwafanya wazazi na wasimamizi hawa wawe mfano mwema wa imani kwa watoto wao.
W. Twakuomba, utusikie.

Msomaji: Upende kuwahifadhi daima jamaa zao katika upendo wako.
W. Twakuomba, utusikie.

Msomaji: Upende kufufua ndani yetu sote neema ya Ubatizo.
W. Twakuomba, utusikie.

Kisha Padri anawaalika wote waliopo kuwaomba Watakatifu.
Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu,- utuombee.
Mtakatifu Yosefu, - utuombee.
Mtakatifu Yohane Mbatizaji, - utuombee.
Watakatifu Petro na Paulo, - mtuombee.
Yafaa kuongeza majina ya Watakatifu wengine, kama ya wote walinzi wa watoto hawa na wa Kanisa au wa mahali hapo. Kisha humalizia:
Watakatifu wote wa Mungu, - mtuombee.

Sala ya uwingaji na kupakwa mafuta kabla ya Ubatizo
Padri husema:
Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulimtuma Mwanao ulimwenguni, apate kufukuza ndani yetu nguvu za shetani, aliye pepo mwovu; apate pia kumwondoa mwanadamu gizani na kumwingiza katika ufalme wa ajabu wa nuru yake. Tunakuomba kwa unyenyekevu, ili watoto hawa watakaoondolewa dhambi ya asili uwafanye hekalu la utukufu wako, naye Roho Mtakatifu apende kukaa ndani yao. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

Padri anaendelea kusema:
Iwakinge nguvu ya Kristo Mwokozi. Tunawatia alama yake kwa mafuta ya wokovu katika huyo Kristo Bwana wetu, anayeishi na kutawala milele na milele.
W. Amina.
Kila mtoto anayebatizwa anapakwa mafuta ya wakatekumeni kifuani. Watoto wakiwa wengi kidogo Mapadri wengine wanaweza kusaidia. Kisha wanakwenda mahali pa kubatizia

UBATIZO WENYEWE
Padri anasimama mbele ya kisima cha Ubatizo, anawakumbusha waliopo hekima ya Mungu aliyependa kumtakasa mwanadamu roho na mwili kwa maji:
Ndugu zangu, tumwombe Bwana Mungu Mwenyezi awajalie watoto hawa uzima mpya kwa maji na Roho Mtakatifu.

Kubariki maji
Kisha Padri anakielekea kisima cha maji ya Ubatizo, na iwapo si wakati wa Pasaka, anayabariki maji kwa sala ifuatayo:
Ee Baba mwema, umeufanya uzima mpya wa watoto wako ututiririkie kama maji kutoka katika kisima cha Ubatizo.
W. Utukuzwe, ee Mungu.

Umependa kuwakusanya katika taifa moja wote walio batizwa katika Mwanao Yesu Kristo kwa maji na Roho Mtakatifu.
W. Utukuzwe, ee Mungu.

Unatuokoa sisi kwa Roho wa upendo wako, ambaye unamshusha moyoni mwetu, ili imani yako itufurahishe.
W. Utukuzwe, ee Mungu.

Unawateua watu waliobatizwa wakatangaze kwa furaha Injili ya Kristo wako kwa mataifa yote.
W. Utukuzwe, ee Mungu.

Basi, upende kuyabariki sasa + maji haya watakayobatiziwa watumishi wako. Umewaita waoshwe kwa maji haya ya kuwapatia uzima mpya katika imani ya Kanisa, ili wapate uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

Kumkataa shetani na kuungama imani
Padri anawashauri wazazi. na wasimamizi kwa maneno yafuatayo:
Ndugu zangu, wazazi na wasimamizi, watoto mliowaleta karibu watapata uzima mpya utokao katika mapendo ya Mungu, kwa maji na Roho Mtakatifu, kwa Sakramenti ya Ubatizo. Basi, ninyi jitahidini kuwalea katika imani, kusudi uzima ule wa Mungu usichafuke, bali uweze kukua ndani yao siku kwa siku. Basi, iwapo kwa imani yenu mko tayari kupokea wajibu huo, mkikumbuka na Ubatizo wenu ninyi wenyewe, kataeni dhambi na kuungama imani katika Yesu Kristo, hiyo ndiyo imani ya Kanisa wanamobatizwa watoto.

Mwamkataa shetani?
Waz. na Ws. Ninamkataa.
Na mambo yake yote?
Waz. na Ws. Ninayakataa.
Na fahari zake zote?
Waz. na Ws. Ninazikataa.

Mwasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, mwumba mbingu na dunia?
Waz. na Ws. Ninasadiki.

Mwasadiki kwa Yesu Kristo, Mwanae pekee, Bwana wetu, aliyezaliwa na Bikira Maria, akateswa, akafa, akazikwa, akafufuka katika wafu, ameketi kuume kwa Baba?
Waz. na Ws. Ninasadiki.

Mwasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele?
Waz. na Ws. Ninasadiki.

Hiyo ndiyo imani yetu. Hiyo ndiyo imani ya Kanisa, tunayoona fahari kuungama katika Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
Inaruhusiwa kutumia maneno mengine ifaapo. Watu wanaweza pia kuimba wimbo wa kufaa kuonesha imani yao kwa pamoja.

Ubatizo
Padri anaita kwanza familia ya mtoto mmoja wafike kwenye kisima cha Ubatizo. Analitaja jina la mtoto na kuwauliza wazazi na wasimamizi:
Je, mwataka F. apate Ubatizo katika imani ya Kanisa, imani tuliyokiri sote sasa hivi pamoja nanyi?
Waz. na Ws. Twataka.

Mara hapo Padri anambatiza mtoto, akisema:
F. ninakubatiza kwa jina la Baba,
Anamzamisha au anammwagia maji mara ya kwanza.
na la Mwana,
Anamzamisha au anammwagia maji kwa mara ya pili.
na la Roho Mtakatifu.
Anamzamisha au anammwagia maji kwa mara ya tatu.

Kubatiza kukiwa kwa kumwagia maji, yafaa watoto washikwe na mama (au na baba), walakini palipo na desturi ya mtoto kushikwa na msimamizi, desturi hiyo na iendelee. Watoto wote wakisha batizwa, watu wanaweza kushangilia au kuimba.

MATENDO YA KUDHIHIRISHA UBATIZO
Kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma

Padri anasema sala ya kupaka mafuta mara moja tu kwa wote:
Mungu Mwenyezi, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliwaokoa watoto hawa katika dhambi, akawapa uzima mpya kwa maji na Roho Mtakatifu. Mnapakwa sasa mafuta matakatifu ya Krisma, Ili muunganike na taifa lake. Muendelee kuwa viungo vya Kristo, kuhani, nabii na mfalme, hadi mpate uzima wa milele mbinguni.
Hapo Padri anampaka kila aliyebatizwa mafuta matakatifu ya Krisma utosini, pasipo kusema neno.

Kuwekewa nguo nyeupe
Padri anasema:
F. na F., mmekuwa sasa viumbe vipya na kumvaa Kristo. Nguo hii nyeupe iwe ishara ya cheo chenu, Nanyi mkisaidiwa kwa maneno na mifano ya jirani zenu, mkaifikishe safi katika uzima wa milele mbinguni.
W. Amina
Watoto waliobatizwa wakiwa wengi sana hawatajwi majina. Wote wavishwa vazi jeupe; vazi la rangi nyingine halikubaliwi isipokuwa ni desturi ya mahali hapo. Yafaa familia yenyewe ilete vazi hilo.

Kupewa mshumaa uwakao
Baadaye Padri anatwaa mshumaa wa Pasaka, akisema:
Pokeeni mwanga wa Kristo.
Mmojawapo (k.m. baba au msimamizi) anawasha mshumaa kwa mshumaa wa Pasaka. Kisha Padri anasema:
Ninyi wazazi na wasimamizi, mmepewa mwanga wa Kristo mpate kuulinda. Muwasaidie watoto hawa, watembee daima kama watoto wa nuru, wadumu katika imani. Na hivyo, mwisho huko mbinguni, watoto hawa, Pamoja na wakatifu wote, waweza kumlaki Bwana.

Efatha
Padri anamgusa mtoto masikio na kinywa kwa kidole gumba, akisema:
Bwana Yesu, aliyefanya viziwi wasikie, na bubu waseme, akujalie uweze kusikia kwa masikio neno lake, na kuungama kwa mdomo imani ya kikristo, kwa sifa na utukufu wa Mungu Baba.
W. Amina.
Kama watoto ni wengi sana, Padri anasema maneno hayo mara moja kwa wote.

MWISHO WA ADHIMISHO
Kisha huwa na maandamano ya kwenda altareni, pamoja na mishumaa iwakayo ya watoto waliobatizwa. Lakini kama Ubatizo umefanyika karibu na altare huwa hakuna maandamano.

Kusema sala ya Bwana
Padri anasimama mbele ya altare, anawaambia wazazi na wasimamizi na watu waliopo:
Ndugu zangu, watoto hawa waliozaliwa upya kwa Ubatizo, sasa wanaitwa watoto wa Mungu; nao kweli ni watoto wa Mungu, sawa na sisi. Baadaye, watapokea utimilifu wa Roho Mtakatifu kwa Sakramenti ya Kipaimara. Tena katika Komunyo takatifu watampokea Bwana aliyejitolea sadaka. Sasa kwa jina la hawa watoto wa Mungu, tusali kama Bwana alivyotufundisha kusali:

Wote wanasema pamoja na Padri:
Baba yetu uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe,
ufalme wako ufike,
utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku,
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina

Baraka
Padri anawabariki waliopo na kuwaaga.
Ndugu zangu, tunawaweka ninyi mikononi mwa Baba Mwenyezi, Mwanaye wa pekee, na Roho Mtakatifu. Mungu mwenye rehema na neema ayalinde maisha yenu, ili mpate kutembea katika nuru ya imani, na kufika nyumbani kwake mbinguni.
W. Amina.

Awabariki Mungu Mwenyezi, Baba, na Mwana + na Roho Mtakatifu.
W. Amina.
Nendeni na Amani.
W. Tumshukuru Mungu.
Baada ya baraka, ikiwezekana, wote waimbe wimbo ufaao wa kuonesha furaha ya Pasaka na shukrani, au wimbo wa Bikira Maria mwenye heri: Moyo wangu wamtukuza Bwana.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.