UBATIZO

Generic placeholder image
UBATIZO WA MTOTO KATIKA HATARI YA KUFA

Hutumika maji yoyote hata yasiyobarikiwa. Wazazi wawe karibu na mtoto wao mgonjwa pamoja na msimamizi wake, jamaa na marafiki pia. Mkristo atakayebatiza anaanza sala fupi za waamini.

Tumwombe Mwenyezi Mungu amshushie rehema yake mtoto huyu atakayepata neema ya Ubatizo, awashushie na wazazi wake na wasimamizi wake na watu wote waliobatizwa. Kwa Ubatizo, upende kumpokea mtoto huyu katika Kanisa lako:
W. Twakuomba, utusikie.
Kwa Ubatizo, upende kumjalia kuwa mmoja wa watoto wako:
W. Twakuomba, utusikie.
Mtoto huyu aliyezikwa na Kristo katika mauti yake kwa Ubatizo, upende kumshirikisha ufufuko wake:
W. Twakuomba, utusikie
Upende kutia nguvu neema ya Ubatizo ya wote waliopo hapa:
W. Twakuomba, utusikie
Upende kuwalinda daima katika imani na upendo wafuasi wote wa Kristo waliobatizwa na kuwa mwili mmoja:
W. Twakuomba, utusikie

Sala za waamini zinamalizika kwa maombi yafuatayo:
Ee Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, uliye asili, ya uzima na upendo, wewe u kitulizo cha wazazi na kinga ya watoto wadogo katika hatari zao. Umetufumbulia hekima ya upendo wako kwa uzima wao mpya wa milele. Usikilize kwa wema sala yetu: usikubali mtoto huyu akae chini ya utawala wa dhambi, bali umpokee kwa rehema katika ufalme wa Mwanao. Kutokana na maji haya utujalie ili kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, mtoto huyu tunaempa jina la F., akisha kufanana na fumbo la kifo cha Kristo wako, afanane na ufufuko wake. Awe mwanao na kupata urithi wa Kristo. Afurahi kukaa nawe katika Kanisa na kufurahi nawe siku zote pamoja na mwanao wa pekee na Roho Mtakatifu, milele na milele.
W. Amina.

Kisha mbatizaji anawaalika watu waliopo waungame imani yao, akisema:
Tukumbuke Ubatizo wetu, tuungame imani ya Yesu Kristo, yaani imani ya Kanisa wanamobatizwa watoto.
Kisha anauliza:
Je, mwasadiki kwa Mungu Baba mwenyezi, mwumba mbingu na dunia?
W. Ninasadiki.
Mwasadiki kwa Yesu Kristo, Mwanae pekee, Bwana wetu, aliyezaliwa na Maria Bikira, akateswa na kuzikwa, akafufuka katika wafu, amekaa kuume kwa Baba?
W. Ninasadiki
Mwasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele?
W. Ninasadiki

Kuungama imani kwaweza kufanyika kwa kusema kanuni ya imani ya Ubatizo ya Kanisa la Roma, iitwayo kanuni ya Mitume:
Nasadiki kwa Mungu Baba mwenyezi,
muumba wa mbingu na dunia,
na kwa Yesu Kristo, Mwanae pekee, Bwana wetu,
aliyetungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu,
akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato,
akasulubiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu,
siku ya tatu akafufuka kutoka wafu,
akapaa mbinguni,
ameketi kuume kwa Mungu Baba mwenyezi;
kutoka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu.
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu,
Kanisa takatifu katoliki,
ushirika wa watakatifu, maondoleo ya dhambi,
ufufuko wa miili, na uzima wa milele. Amina.

Kisha mwemye kubatiza anambatiza mtoto:
F., ninakubatiza kwa jina la Baba
anammwagia maji mara ya kwanza
na la Mwana
anammwagia maji mara ya pili
na la Roho Mtakatifu.
anammwagia maji mara tatu

Mwenye kubatiza aweza kumwekea mtoto nguo nyeupe, akisema:
F. umekuwa sasa kiumbe kipya na kumvaa Kristo. Nguo hii nyeupe iwe ishara ya cheo chako. Nawe ukisaidiwa kwa maneno na mifano ya jirani zako, ukaifikishe safi katika uzima wa milele mbinguni.
W. Amina

Ibada hii inamalizika kwa sala ya Bwana:
Baba yetu uliye mbinguni
jina lako litukuzwe,
ufalme wako ufike,
utakalo lifanyike duniani kama Mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku,
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina

Iwapo hakuna mtu awezaye kuziendesha sala hizo zote za Ubatizo, mwamini yeyote aweza kusema kanuni ya imani, kisha anammwagia maji mtoto, akisema maneno ya kawaida. Lakini kama haiwezekani kusema Kanuni ya imani, inaweza kuachwa. Ikiwa mtoto anazimia, mwenye kubatiza anaacha ibada nyingine na kusema tu maneno ya kubatiza. Yafaa mwenye kubatiza awe na mtu mwingine kama shahidi.


-----------------

Ikiwa Padri anabatiza katika hatari ya kufa, anaweza kumpa mtoto mgonjwa Kipaimara (tazama hapo chini).

KUMPA KIPAIMARA MGONJWA
ALIYE KATIKA HATARI YA KUFA

Ni jambo lifaalo sana kwa kila mwamini aliyebatizwa apate utimilifu wa ukristo wake kwa Sakramenti za Kipaimara na Ekaristi. Kwa hiyo mwamini aliyebatizwa akiwa katika hatari ya kufa, na bado ana akili zake timamu, apokee kwanza Kipaimara kabla ya Komunyopamba. Ikiwezekana apewe kwanza mafundisho muhimu juu ya Sakramenti hizo.
Kwa kawaida haifai kumpa mgonjwa aliye katika hatari ya kufa Kipaimara na Mpako wa wagonjwa katika ibada moja mfululizo.
Mtoto ambaye hajapata bado akili, apewe Kipaimara kwa kufuata misingi na kanuni zilezile zilizowekwa kwa kutoa Ubatizo.
Iwapo mazingira yanaruhusu sharti ibada yote ifuatwe kikamilifu, kama ikiwa hatari ya kufa ni kubwa na haraka yatakiwa, yule anayetoa Kipaimara humwekea mikono mgonjwa akisema:


Ee Mungu Mwenyezi, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ndiye uliyemzaa mtumishi wako huyu kwa maji na Roho Mtakatifu ukamwokoa katika dhambi. Basi, ee Bwana, umtie Roho Mtakatifu Mfariji, Umpe Roho wa hekima na akili, Roho wa shauri na nguvu, Roho wa elimu na ibada, umjaze Roho wa uchaji wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

Kisha hutia ncha ya kidole gumba cha mkono wa kuume katika mafuta ya Krisma. Na kwa kidole hicho humtia huyo anayepewa Kipaimara alama ya msalaba katika paji la uso, huku akisema:
F. pokea muhuri wa Paji la Roho Mtakatifu.
Aliyepata Kipaimara akiweza, huitikia:
Amina.

Mambo mengine yanaweza kutangulizwa kama matayarisho, na mengine yakafuata kama nyongeza kadiri mazingira yanavyoruhusu. Katika hatari kubwa sana ya kufa, yatosha mgonjwa apakwe mafuta ya Krisma huku akiambiwa maneno haya ya Sakramenti:

F. pokea muhuri wa Paji la Roho Mtakatifu.