UBATIZO

Generic placeholder image
KUMWINGIZA KANISANI MTOTO ALIYEKWISHA BATIZWA KATIKA HATARI YA KUFA

Wakati waamini wanaimba Zaburi au wimbo mwingine, Padri au shemasi anaandamana na watumishi, amevaa alba au kota na stola, na hata joho. Anafika mbele ya mlango wa kanisa au mahali pengine kanisani walipokusanyika wazazi na msimamizi pamoja na mtoto. Padri anawasalimu watu waliopo, hasa wazazi na msimamizi. Anawasifu kwa ajili ya mtoto wao aliyebatizwa mapema. Anamshukuru Mungu na kuwapa pongezi wazazi kwa ajili ya mtoto wao aliyepona.

Kwanza Padri anawauliza wazazi:

Mlimpa mtoto wenu jina gani?
Waz. F.
Sasa mwamwombea nini katika Kanisa la Mungu huyu F. hali amekwisha batizwa?
Waz. Tunaomba wote wajue kwamba yeye amepokelewa katika Kanisa.

Kisha Padri anawauliza wazazi:
Je, ninyi mnaomleta huyu mtoto kanisani, mwafahamu wajibu mlioupokea juu ya huyu aliyebatizwa, yaani kumfundisha imani apate kushika amri za Mungu na kumpenda jirani yake kama Kristo alivyotufundisha?
Waz. Twafahamu.

Kisha Padri anamwelekea msimamizi:
Nawe msimamizi, je, uko tayari kuwasaidia wazazi wa mtoto huyu katika wajibu wao?
Ms. Niko tayari.

Kisha Padri anaendelea kusema
F., jamii hii ya wakristo pamoja na wazazi wako wanamshukuru Mungu kwa furaha kubwa. Wanakupokea na kushuhudia kwamba umekwisha kupokewa na Kanisa. Kwa jina lao nakutia ishara ya Kristo aliyekupa uzima katika Ubatizo na kukuingiza katika kundi la Kanisa. Na wazazi wako (na msimamizi wako) watakutia pia ishara ya msalaba.

Padri anamtia mtoto ishara ya msalaba katika paji la uso, pasipo kusema neno. Kisha anawaambia wazazi:
Nanyi wazazi (na msimamizi), mtieni mtoto wenu ishara ya msalaba wa Kristo Mwokozi katika paji la uso.

Padri anawaalika wazazi, msimamizi na wote waliopo washiriki ibada ya neno la Mungu. Ikiwezekana hufanyika maandamano pamoja na nyimbo mpaka mahali penyewe.

NENO LA MUNGU
Masomo ya Biblia na Hotuba

Wote wawe wameketi.
AGANO LA KALE
1. Tumepewa moyo mpya Eze.36:24-28
Maji ya Ubatizo husafisha mioyo yetu, iliyo migumu, yenye dhambi na ukosefu wa mapendo. Mioyo yetu inageuka kuwa mipya, yenye kumpenda Mungu na kushika amri zake.
Somo la kitabu cha Nabii Ezekieli
Bwana Mungu asema hivi: Nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe, uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
Neno la Bwana
W. Tumshukuru Mungu

AGANO JIPYA
2. Tumepewa uzima mpya Rum.6:3-5
Tendo la Ubatizo huonyesha wazi kwamba kwa Ubatizo tumekataa dhambi, na tumepewa uzima wa milele. Kutiwa ndani ya maji ni kama kuzikwa pamoja na Kristo, na kuopolewa toka majini ni kama kufufuka pamoja naye katika uzima mpya wa kikristo.
Somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi.
Ndugu zangu, Sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake. Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya Ubatizo katika mauti yake, Kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake.
Neno la Bwana
W.Tumshukuru Mungu

AU
3. Sisi ni waana wa Mungu Rum.8:28-32
Kwa Ubatizo, Mungu ametupokea kama wana wake katika Kristo.
Somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi.
Ndugu zangu, twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki hao akawatukuza. Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye?
Neno la Bwana
W. Tumshukuru Mungu

AU
4. Mwili wa mtu kama mfano wa umoja wa Kristo na wakristo 1Kor.12:12-13
Kwa Ubatizo tumeunganishwa na Kristo katika umoja wa imani na wa mapendo.
Somo la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa
Wakorintho. Ndugu zangu, kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani, ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.
Neno la Bwana
W. Tumshukuru Mungu

INJILI
5. Amri kuu ya upendo Mt.22:35-40
Bwana Yesu ametufundisha kwamba amri zote za kikristo zinatokana na amri kuu ya mapendo. Kumpenda Mungu kwa moyo wote na kumpenda jirani kwa ajili ya Mungu, ndio ukamilifu wa kikristo.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Siku zile, mmoja wa Mafarisayo, mwanasheria, akamwuliza Yesu, akimjaribu: Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

AU
6. Yesu awatuma mitume kufundisha watu wote Injili Mt.28:18-20
Bwana Yesu aliwatuma Mitume wake duniani kote, wakawaingize watu wa mataifa yote katika Kanisa lake. Kwa njia ya Ubatizo.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo.
Siku zile, Yesu akaja kwa mitume, akasema nao akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kushika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

AU
7. Yesu anabatizwa Mk.1:9-11
Ubatizo wa Yesu katika Yordani ni mfano wa Ubatizo wetu: katika Ubatizo tunageuka kuwa wana wa Mungu Baba na tunampokea Roho Mtakatifu.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Marko.
Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohane katika Yordani. Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake; na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu, nimependezwa nawe.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

AU
8. Yesu na watoto wadogo Mk.10:13-16
Amin, nawaambieni, yeyote asiyekubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Marko.
Siku zile, walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao, Amin, nawaambieni, yeyote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

AU
9. Kubatizwa ni kuzaliwa tena Yn.3:1-6
Ubatizo ni kweli kuzaliwa mara ya pili, na kupewa uzima wa milele na kuingia katika Ufalme wa Mungu.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Yohane.
Palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
Neno la Bwana
W. Sifa kwako, ee Kristo

Baada ya somo, Padri anatoa hotuba fupi juu ya yale yaliyosomwa, na kuzidi kuwafahamisha watu waliopo fumbo la Ubatizo, na kuwahimiza wazazi na wasimamizi wapokee wajibu wao kwa furaha.

Sala za waamini
Tumwombe Kristo mwenye rehema na upole kwa ajili ya mtoto huyu, wazazi na msimamizi wake, na wote waliobatizwa.

Msomaji: Tuombe, ili mtoto huyu aliyebatizwa na kurudishiwa afya aoneshe kwamba atamkumbuka Mungu:
W. Kristo, twakuomba, utusikie.

Msomaji: Tuombe, ili aendelee kuwa kiungo hai cha Kanisa lako takatifu.
W. Kristo, twakuomba, utusikie.

Msomaji: Tuombe, ili aweze kusikia Injili yako, kuishika na kuishuhudia:
W. Kristo, twakuomba, utusikie.

Msomaji: Tuombe, ili aifikie kwa furaha meza ya sadaka yako.
W. Kristo, twaomba, utusikie.

Msomaji: Tuombe, ili ampende Bwana Mungu na jirani yake, kama ulivyotufundisha.
W. Kristo, twaomba, utusikie.

Msomaji: Tuombe, ili akishafundishwa kwa maneno na mifano ya wakristo, akue katika utakatifu na hekima:
W. Kristo, twakuomba, utusikie.

Msomaji: Tuombe ili wafuasi wako wote waishi daima katika imani moja na upendo.
W. Kristo, twakuomba, utusikie.

Kisha Padri anawaalika wote waliopo kuwaomba watakatifu:
Maria mtakatifu, mama wa Mungu,- utuombee.
Mtakatifu Yosefu,- utuombee.
Mtakatifu Yohane mbatizaji,- utuombee.
Watakatifu Petro na Paulo,- mtuombee.
Yafaa kuongeza majina ya Watakatifu wengine, hasa ya wale walio walinzi wa mtoto huyo na wa Kanisa au wa mahali hapo. Kisha humalizia:
Watakatifu wote wa Mungu,- mtuombee.

Baada ya sala hizo Padri anasema:
Ee Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, uliye asili ya uzima na upendo, unatukuka katika shughuli za wazazi. Watoto wachanga wanapokuwa hatarini unaonesha hekima yako, na katika Ubatizo wao unajionesha kuwa Mwokozi wao. Kanisa linashukuru kwa ajili ya huyu mtumishi wako F. Linakuomba, ili huyu uliyemuondoa katika ufalme wa giza na kumuweka katika nuru yako ya ajabu, ukamfanye kuwa mtoto wako na hekalu la Roho Mtakatifu kwa Sakramenti ya Ubatizo, umsaidie daima katika hatari za maisha haya. Umkinge daima kwa nguvu ya Kristo Mwokozi, katika vita vya kupigania ufalme wako. Tunakuomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.

MATENDO YA KUDHIHIRISHA UBATIZO
Kupakwa mafuta matakatifu ya Krisma

Padri anasema:
Mungu Mwenyezi, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, alimwokoa mtoto huyu katika dhambi, akampa uzima mpya kwa maji na Roho Mtakatifu. Unapakwa sasa mafuta matakatifu ya Krisma, ili uunganike na taifa lake. Uendelee kuwa kiungo cha Kristo, kuhani, nabii na mfalme, hadi upate uzima wa milele mbinguni.
Hapo Padri anampaka mtoto Krisma takatifu utosini, pasipo kusema neno.

Kuwekewa nguo nyeupe
Padri anasema:
F. umekuwa sasa kiumbe kipya na kumvaa Kristo. Nguo hii nyeupe iwe ishara ya cheo chako. Nawe ukisaidiwa kwa maneno na mifano ya jirani zako, ukaifikishe safi katika uzima wa milele mbinguni.
W. Amina
Na mtoto anavishwa vazi jeupe; vazi la rangi nyingine halikubaliwi isipokuwa ni desturi ya mahali hapo. Yafaa familia yenyewe ilete vazi hilo.

Kupewa mshumaa uwakao
Baadaye Padri anatwaa mshumaa wa Pasaka, akisema:
Pokea mwanga wa Kristo.
Mmojawapo (kwa mfano: baba, mama au msimamizi) anawasha mshumaa wa mtoto kwa mshumaa wa Pasaka.
Kisha Padri anasema:

Ninyi wazazi na msimamizi, mmepewa mwanga wa Kristo mpate kuulinda. Mumsaidie mtoto wenu, atembee daima kama mtoto wa nuru, adumu katika imani. Na hivyo, mwisho huko mbinguni, mtoto huyu, pamoja na watakatifu wote, aweze kumlaki Bwana.

MWISHO WA ADHIMISHO
Kisha huwa na maandamano ya kwenda altareni, pamoja na mshumaa uwakao wa mtoto. aliyebatizwa. Lakini kama Ubatizo umefanyika karibu na altare huwa hakuna maandamano.

Kusema sala ya Bwana
Padri anasimama mbele ya altare, anawaambia wazazi na msimamizi na watu waliopo:
Ndugu zangu, mtoto huyu alizaliwa upya kwa Ubatizo. Sasa anaitwa mtoto wa Mungu; na kweli ni mtoto wa Mungu, sawa na sisi. Baadaye, atapokea utimilifu wa Roho Mtakatifu kwa Sakramenti ya Kipaimara. Tena katika Komunyo takatifu atampokea Bwana aliyejitoa sadaka. Sasa, kwa jina la huyu mtoto wa Mungu, tusali kama Bwana alivyotufundisha kusali:

Wote wanasema pamoja na Padri:
Baba yetu uliye mbinguni
jina lako litukuzwe,
ufalme wako ufike,
utakalo lifanyike duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku,
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina

Baraka
Padri anawabariki waliopo na kuwaaga.
Ndugu zangu, tunawaweka ninyi mikononi mwa Baba mwenyezi, Mwanaye wa pekee, na Roho Mtakatifu. Mungu mwenye rehema na neema ayalinde maisha yenu, ili mpate kutembea katika nuru ya imani, na kufika nyumbani kwake mbinguni.
W. Amina.

Awabariki Mungu Mwenyezi, Baba, na Mwana + na Roho Mtakatifu.
W. Amina
Nendeni na Amani.
W. Tumshukuru Mungu.
Baada ya baraka, ikiwezekana, wote waimbe wimbo ufaao wa kuonesha furaha ya Pasaka na shukrani, au wimbo wa Bikira Maria mwenye heri: Moyo wangu wamtukuza Bwana.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.