SALA YA JIONI

Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu: Amina.

Sala ya kushukuru
Tunakushukuru, ee Mungu, kwa mapaji yote uliyotujalia leo. Amina.

Baba yetu
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.

Salamu Maria
Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu, mzao wa tumbo lako, amebarikiwa. Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.

Sala ya Imani
Mungu wangu, nasadiki maneno yote linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma, kwani ndiwe uliyefumbulia hayo, wala hudanganyiki, na wala hudanganyi. Amina.

Sala ya Matumaini
Mungu wangu, natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo, neema zako duniani na utukufu mbinguni, kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi, nawe ni mwaminifu. Amina.

Sala ya Mapendo
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote; kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.

Sala ya Kutubu
Tuwaze katika mioyo yetu makosa ya leo tuliyomkosea Mungu kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwakutotimiza wajibu. (husubiri kidogo)

Namwungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu,
kwani nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno,
kwa matendo, na kwa kutotimiza wajibu.
Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana.
Ndiyo maana namwomba Maria mwenye heri,
Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu.

K. Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe kwenye uzima wa milele.
W. Amina.

Sala ya kuwaombea watu
Mungu wangu, nawaombea watu wa nchi hii, wapate kusikia maneno yako na kukupenda wewe Bwana Mungu Wetu. Amina.

Kusifu
(Malaika wa Bwana, uliye mlinzi wangu, uniangaze, unilinde, uniongoze mimi, niliyekabidhiwa kwako na huruma yake Mungu. Amina.
Baba yetu ...
Salamu Maria ... (mara kumi)
Atukuzwe Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu kama mwanzo na sasa na siku zote na milele Amina.)

Enyi, Yesu na Maria na Yosefu, nawatolea moyo na roho na uzima wangu!
Enyi, Yesu na Maria na Yosefu, nijilieni saa ya kufa kwangu!
Enyi, Yesu na Maria na Yosefu, mnijalie nife mikononi mwenu!

Kwa heri, Yesu, mpenzi mwema, Nakwenda siudhike mno. Nakushukuru, nakupenda. Kwa hizo nyimbo za mwisho. Asubuhi nitarudi. Yesu kwa heri.
Kwa heri Mama mtakatifu, Sasa napata pumzika. Asante kwa moyo na nguvu, Leo, umeniombea. Asubuhi nitarudi. Mama kwa heri.
Kwa heri, Yosefu mnyenyekevu, Kazi zatimilizika. Kama mchana, leo usiku Nisimamie salama. Asubuhi nitarudi. Yosefu kwa heri.

Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu: Amina.