SALA YA ASUBUHI

Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu: Amina.

Ee Baba yetu Mungu mkuu,
Umenilinda usiku huu,
Nakushukuru kwa moyo,
Ee Baba, Mwana na Roho.
Nilinde tena siku hii,
Niache dhambi nikutii.
Naomba sana Baba wee,
Baraka yako nipokee.
Bikira safi, ee Maria,
Nisipotee nisimamie,
Mlinzi mkuu malaika wee.
Kwa Mungu wetu niombee
Nitake nitende mema tu
Na mwisho nije kwako juu. Amina.

Nia njema
Kumheshimu Mungu wangu
Namtolea roho yangu,
Nifanye kazi nipumzike
Amri zake tu nishike.
Wazo, neno, tendo lote
Namtolea Mungu pote
Roho, mwili, chote changu,
Pendo na uzima wangu
Mungu wangu nitampenda,
Wala dhambi sitatenda.
Jina lako nasifia,
Utakalo hutimia.
Kwa utii navumilia
Teso na matata pia
Nipe, Bwana, neema zako
Niongeze sifa zako. Amina.

Sala ya Matoleo
Ee Yesu, kwa mikono ya Bikira Maria, na kwa maungano na sadaka yako kuu, ninakutolea sala, matendo, masumbuko na furaha zangu zote za leo. Ee Yesu,ufalme wako utufikie. Amina.

Baba yetu
Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku. Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.

Salamu Maria
Salamu, Maria, umejaa neema; Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu, mzao wa tumbo lako, amebarikiwa. Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina.

Kanuni ya Imani
Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi, Muumba wambingu na dunia; na kwa Yesu Kristo Mwanae pekee, Bwana wetu, aliyetungwa mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu; siku ya tatu akafufuka kutoka wafu, akapaa mbinguni; ameketi kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi; kutoka huko atakuja kuwahukumu walio hai na wafu.
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu Katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili, na uzima wa milele. Amina.

Amri za Mungu
1. Ndimi Bwana Mungu wako, usiabudu miungu wengine.
2. Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako.
3. Shika kitakatifu siku ya Mungu.
4. Waheshimu baba na mama; upate miaka mingi na heri duniani.
5. Usiue.
6. Usizini
7. Usiibe.
8. Usiseme uongo.
9. Usitamani mwanamke asiye mke wako.
10. Usitamani mali ya mtu mwingine.

Amri za Kanisa
1. Hudhuria Misa takatifu Dominika na Sikukuu zilizoamriwa.
2. Funga siku ya Jumatano ya Majivu; usile nyama siku ya Ijumaa Kuu.
3. Ungama dhambi zako walau mara moja kila mwaka.
4. Pokea Ekaristi Takatifu hasa wakati wa Pasaka.
5. Saidia Kanisa katoliki kwa zaka.
6. Shika sheria katoliki za ndoa.

Sala ya Imani
Mungu wangu, nasadiki maneno yote linayosadiki na linayofundisha Kanisa Katoliki la Roma, kwani ndiwe uliyefumbulia hayo, wala hudanganyiki, na wala hudanganyi. Amina.

Sala ya Matumaini
Mungu wangu, natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristo, neema zako duniani na utukufu mbinguni, kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi, nawe ni mwaminifu. Amina.

Sala ya Mapendo
Mungu wangu, nakupenda zaidi ya chochote; kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina.

Sala ya Kutubu
Mungu wangu, nimetubu sana dhambi zangu, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza, wachukizwa na dhambi. Basi sitaki kukosa tena, nitafanya kitubio, naomba neema yako nipate kurudi. Amina.

Sala kwa Malaika mlinzi
Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote za roho na za mwili. Amina.

Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu: Amina.