5

Bwana arusi
1 Naingia bustanini mwangu, dada yangu, bi arusi. Nakusanya manemane na viungo, nala sega langu la asali, nanywa divai yangu na maziwa yangu.

Bibi arusi
Kuleni enyi marafiki, kunyweni; kunyweni sana wapendwa wangu.

Shairi la nne
Bibi arusi

2 Nililala, lakini moyo wangu haukulala. Sauti ya mpenzi wangu anabisha hodi.

Bwana arusi
“Nifungulie, dada yangu mpenzi wangu, bibiarusi wangu, hua wangu, usiye na kasoro. Kichwa changu kimelowa umande na nywele zangu manyunyu ya usiku.”

Bibi arusi
3 Nimekwisha yavua mavazi yangu, nitayavaaje tena? Nimekwisha nawa miguu yangu, niichafueje tena?
4 Hapo mpenzi wangu akaugusa mlango, moyo wangu ukajaa furaha.
5 Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu. Mikono yangu imejaa manemane, na vidole vyangu vyadondosha manemane, nilipolishika komeo kufungua mlango.
6 Nilimfungulia mlango mpenzi wangu, lakini kumbe, alikuwa amekwisha toweka. Moyo wangu ulifurahi alipokuwa akizungumza! Nilimtafuta, lakini sikumpata; nilimwita, lakini hakuniitikia.
7 Walinzi wa mji waliniona, walipokuwa wanazunguka mjini; wakanipiga na kunijeruhi; nao walinzi wa lango wakaninyanganya shela langu.
8 Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu, mkimwona mpenzi wangu, mwelezeni kwamba naugua kwa mapenzi!

Wanawake
9 Ewe upendezaye kuliko wanawake wote! Kwani huyo mpenzi wako ana nini cha zaidi ya mpenzi mwingine, hata utusihi kwa moyo kiasi hicho?

Bibi arusi
10 Mpenzi wangu ni mzuri na mwenye nguvu, mashuhuri miongoni mwa wanaume elfu kumi.
11 Kichwa chake kizuri kama dhahabu safi, nywele zake ni za ukoka, nyeusi ti kama kunguru.
12 Macho yake ni kama ya hua kandokando ya kijito, ni kama njiwa waliooga maziwa kando ya kijito.
13 Mashavu yake ni kama matuta ya rihani kama bustani iliyojaa manukato na manemane. Midomo yake ni kama yungiyungi, imelowa manemane kwa wingi.
14 Mikono yake imewekwa bangili za dhahabu, amevalia johari za Tarshishi. Kiwiliwili chake ni kama pembe za ndovu zilizopambwa kwa vito vya johari ya rangi ya samawati.
15 Miguu yake ni kama nguzo za alabasta zilizosimikwa katika misingi ya dhahabu. Umbo lake ni kama Lebanoni, ni bora kama miti ya mierezi.
16 Kinywa chake kimejaa maneno matamu, kwa ujumla anapendeza. Basi, hivyo ndivyo alivyo mpenzi wangu, naam, ndivyo alivyo rafiki yangu, enyi wanawake wa Yerusalemu.

Generic placeholder image