28

Unabii juu ya mfalme wa Tiro
1 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
2 “Wewe mtu! Mwambie mfalme wa Tiro kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe una kiburi cha moyo, na umesema kwamba wewe ni mungu, kwamba umekalia kiti cha enzi cha miungu, umekaa mbali huko baharini. Lakini, wewe ni binadamu tu wala si Mungu, ingawa wajiona kuwa una hekima kama Mungu.
3 Haya! Wewe wajiona mwenye hekima kuliko Danieli, wadhani hakuna siri yoyote usiyoijua.
4 Kwa hekima na akili yako umejipatia utajiri, umejikusanyia dhahabu na fedha ukaziweka katika hazina zako.
5 Kwa busara yako kubwa katika biashara umejiongezea utajiri wako, ukawa na kiburi kwa mali zako!
6 Kwa hiyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa vile unajiona mwenye hekima kama Mungu,
7 basi nitakuletea watu wageni, mataifa katili kuliko yote. Wataharibu fahari ya hekima yako na kuchafua uzuri wako.
8 Watakutumbukiza chini shimoni, nawe utakufa kifo cha kikatili kilindini mwa bahari.
9 Je, utajiona bado kuwa mungu mbele ya hao watakaokuua? Mikononi mwa hao watakaokuangamiza, utatambua kuwa wewe ni mtu tu, wala si Mungu!
10 Utakufa kifo cha aibu kubwa mikononi mwa watu wa mataifa. Ni mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Kuanguka kwa mfalme wa Tiro:
11 Tena neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
12 “Wewe mtu! Imba wimbo wa maombolezo juu ya mfalme wa Tiro. Mwambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe mfalme wa Tiro ulikuwa upeo wa ukamilifu; ulijaa hekima na uzuri kamili.
13 Ulikaa Edeni, bustani ya Mungu. Ulipambwa kwa kila namna ya johari, akiki, topazi, yaspi, zabarajadi, berili, sardoniki, johari ya rangi ya samawati, almasi na zumaridi. Ulikuwa na mapambo ya dhahabu. Yote uliwekewa tayari siku ulipoumbwa.
14 Nilimteua malaika kukulinda, uliishi katika mlima wangu mtakatifu na kutembea juu ya vito vinavyometameta.
15 Uliishi maisha yasiyo na lawama, tangu siku ile ulipoumbwa, hadi ulipoanza kufanya uovu.
16 Ufanisi wa biashara yako ulikujaza dhuluma, ukatenda dhambi. Kwa hiyo nilikufukuza kama kinyaa, mbali na mlima wangu mtakatifu. Na yule malaika aliyekulinda akakufukuzia mbali na vito vinavyometameta.
17 Ulikuwa na kiburi kwa sababu ya uzuri wako. Uliharibu hekima yako kwa sababu ya fahari yako. Nilikubwaga chini udongoni, nikakufanya kuwa kioja kwa wafalme.
18 Kwa wingi wa uhalifu wako na udanganyifu katika biashara yako ulipachafua mahali pako pa ibada; kwa hiyo nilizusha moto kwako, nao ukakuteketeza, nami nikakufanya majivu juu ya nchi, mbele ya wote waliokutazama.
19 Wote wanaokufahamu kati ya mataifa wameshikwa na mshangao juu yako. Umeufikia mwisho wa kutisha, na hutakuwapo tena milele.”

Unabii juu ya Sidoni
20 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
21 “Wewe mtu! Ugeukie mji wa Sidoni,
22 utoe unabii juu yake kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi nitapambana nawe Sidoni, na kuudhihirisha utukufu wangu kati yako. Nitakapotekeleza hukumu zangu juu yako na kukudhihirishia utakatifu wangu, ndipo utakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
23 Nitakupelekea maradhi mabaya na umwagaji damu utafanyika katika barabara zako. Utashambuliwa kwa upanga toka pande zote na watu wako watakaouawa, watakuwa wengi. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Waisraeli watapata baraka
24 Mungu asema, “Mataifa jirani na Waisraeli ambayo yalikuwa yanawaudhi hayataweza tena kuwaumiza Waisraeli kama vile kwa miiba na michongoma. Ndipo watakapojua ya kuwa mimi ni Bwana Mwenyezi-Mungu.
25 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawakusanya na kuwaleta Waisraeli kutoka katika mataifa yote ambamo walitawanywa. Hivyo nitawafanya watu wa mataifa waone kuwa mimi ni mtakatifu. Watu wa Israeli wataishi katika nchi yao ambayo mimi nilimpa mtumishi wangu Yakobo.
26 Watakaa humo salama salimini; watajenga nyumba na kupanda mizabibu. Wataishi bila hofu maana mataifa jirani zao ambayo yaliwaudhi, mimi nitayaadhibu. Hapo watatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.”

Generic placeholder image