13

Kisa cha Susana
1 Palikuwa na mtu mmoja jina lake Yoakimu aliyeishi Babuloni.
2 Mtu huyo alioa mwanamke aliyeitwa Susana, binti Hilkia. Susana alikuwa mwanamke mzuri sana na mcha Mungu.
3 Wazazi wake walikuwa waadilifu na walimfunza binti yao kufuata sheria ya Mose.
4 Yoakimu alikuwa mtu tajiri sana, na alikuwa na bustani kubwa karibu na nyumba yake. Kwa vile yeye alikuwa anaheshimika kuliko Wayahudi wote mjini humo, Wayahudi wenzake walikuwa wakijumuika nyumbani mwake kila wakati.
5 Basi, mwaka huo, wazee wawili miongoni mwa jumuiya hiyo waliteuliwa kuwa waamuzi. Hao ndio wale ambao Bwana alisema juu yao: "Ufisadi utatokea huko Babuloni, kutoka kwa wazee waamuzi, ambao wanapaswa kuwaongoza watu!"
6 Kila siku wazee hao walikuwa nyumbani kwa Yoakimu na mtu yeyote aliyekuwa na shtaka lake alilileta kwao.
7 Basi, kila siku adhuhuri, wakati watu wote walipokuwa wameondoka Susana aliingia bustanini kwa mumewe kutembea.
8 Wazee hao wawili walimwona akitembeatembea humo bustanini kila siku, nao wakaanza kumtamani.
9 Walivutiwa na uzuri wake hata wakapoteza hamu ya kuomba wala kufikiria wajibu wao wa kutoa hukumu za haki.
10 Wote walimtamani sana Susana, lakini kila mmoja wao hakumjulisha mwenzake shida yake. "
11 Kila mmoja aliona haya kumjulisha mwenzake kuwa alikuwa anamtamani kumpata yule mwanamke.
12 Kila siku walikuwa wakichungulia kwa hamu kubwa ili mradi tu wamwone.
13 Basi, siku moja adhuhuri wakaambiana; "Saa ya chakula imefika. Twende zetu nyumbani!"
14 Basi, wakaondoka na kila mmoja akashika njia yake. Lakini kila mmoja akarudi nyuma. Mara wakakutana ana kwa ana. Walipoulizana kisa kila mmoja akakiri kuwa anamtamani Susana. Basi, wakaamua kwa pamoja kungojea wakati mzuri wa kumpata Susana akiwa peke yake.
15 Ikawa nafasi waliyongojea ikapatikana: Susana aliingia bustanini ameandamana na watumishi wake kama ilivyokuwa desturi yake, akiwa wili. Kwa vile kulikuwa na joto jingi siku hiyo, yeye alitaka kuoga humo bustanini.
16 Kwa bahati nzuri, hapakuwa na mtu mwingine yeyote bustanini, ila tu wale wazee wawili waamuzi ambao walikuwa wamekaa chonjo mafichoni wakimvizia.
17 Basi, Susana akawatuma watumishi wa kike nyumbani akisema,
18 "Nendeni mkaniletee mafuta na marashi. Kisha fungeni milango ya bustani nipate kuoga." Watumishi wa kike wakafanya kama walivyoambiwa; wakaifunga milango ya bustani na kupitia mlango wa pembeni kuchukua vitu wale walivyotumwa. Hawakuwaona wazee wawili waliokuwa wamejificha.
19 Mara, wale watumishi wa kike walipotoka, wale wazee wawili wakajitokeza, wakamkimbilia Susana,
20 wakamwambia, "Tazama, milango imefungwa, hivyo hakuna mtu atakayetuona. Sisi tunakupenda! Basi, tutimizie haja zetu.
21 Ukikataa, tutakupeleka mahakamani na kutoa ushahidi kuwa ulikuwa na kijana fulani, ndiyo maana ukawaambia wale watumishi wa kike waende zao."
22 Susana alipiga kite, akasema, "Nimebanwa kila upande! Nikifanya mnalotaka, nitauawa; nikikataa, sitaweza kuokoka mikononi mwenu!
23 Lakini afadhali mniue kuliko kufanya dhambi mbele ya Bwana."
24 Hapo, Susana akapiga kelele, nao wale wazee wawili wakampigia kelele.
25 Mmoja wao akapiga mbio na kuifungua milango ya bustani.
26 Watumishi wa nyumbani waliposikia makelele bustanini, wakakimbilia bustanini kwa kupitia mlango wa pembeni kuona yaliyompata Susana.
27 Wale wazee wakamsingizia Susana kama walivyopanga. Wale watumishi wakaona aibu kubwa sana, maana Susana alikuwa hajawahi kupatikana na jambo kama hilo.
28 Kesho yake, watu walipokusa nyika tena nyumbani kwa Yoakimu, mumewe Susana, wale wazee wawili waamuzi walikuwapo pia. Walikuwa wamejizatiti kikamilifu kutekeleza njama zao ili Susana ahukumiwe adhabu ya kifo.
29 Basi, wakasema mbele ya watu waliokuwa hapo, "Mwiteni Susana, binti Hilkia, mkewe Yoakimu."
30 Basi, watu wakaenda kumwita. Susana akaja, huku ameandamana na wazazi wake, mama yake na watoto wake, pamoja na ndugu zake wote.
31 Susana alikuwa mwanamke mzuri na wa kupendeza sana.
32 Alikuwa amejifunika shela usoni. Basi, waovu hao wawili wakaamuru shela liondolewe usoni ili wajishibishe kwa uzuri wake
33 Ndugu zake na wote waliomwona wakatokwa na machozi!
34 Hapo, wale wazee wawili waamuzi wakasimama mbele ya watu wote, wakaiweka mikono yao juu ya kichwa yao juu ya kichwa cha Susana.
35 Lakini yeye, huku ma chozi yanamchuruzika, akatazama juu mbinguni, maana, kwa moyo wake alimtumainia Bwana.
36 Wale wazee wakasema, "Sisi, tulipokuwa tunazee mbeatembea bustanini peke yetu, mwanamke huyu aliingia ndani ya bustani pamoja na watumishi wa kike wawili, wakafunga milango ya bustani, kisha akawaruhusu waende zao.
37 Punde si punde, kijana mmoja aliyekuwa amejificha, akatokea, akamwendea, akalala naye.
38 Wakati huo wote, sisi tulikuwa pembeni mwa bustani. Tulishuhudia uovu wote huo, ndipo tukakimbilia mahali walipokuwa.
39 Tuliwafumania wakikumbatiana. Lakini tulishindwa kumkamata yule kijana, kwani alituzidi nguvu, aliufungua mlango wa bustani, akatoroka.
40 Lakini tulifaulu kumkamata huyu mwanamke. Na tulipomwuliza yule kijana ni nani, yeye alikataa kutuambia. Tunaapa kwamba hiyo ni kweli tupu."
41 Watu waliokusanyika mahali hapo wakawasadiki hao wazee wawili kwa vile wao walikuwa wazee wa watu tena ni waamuzi. Basi, wakamhukumu Susana auawe..
42 Lakini Susana akalia kwa sauti kubwa, "Ee Mungu wa milele! Wewe waona yaliyofichika; wajua kila kitu hata kabla hakijatukia.
43 Wewe wajua kwamba wazee hawa wananishuhudia uongo. Mimi sasa nitauawa. Lakini sikufanya hata mojawapo ya mambo wanayonisingizia!"
44 Bwana akakisikia kilio cha Susana
45 Basi, alipokuwa anachukuliwa kwenda kuuawa, roho ya Mungu ikamchochea kijana mmoja aitwaye Danieli,
46 akapiga kelele kwa sauti kubwa: "Mimi sihusiki na kifo cha mwanamke huyu!",
47 Watu wote wakamgeukia, wakasema, "Unamaanisha nini kwa maneno hayo?"
48 Danieli akajitokeza katikati yao, akasema, "Enyi Waisraeli! Je mmekuwa wapumbavu kiasi hicho? Mtamhukumuje binti wa Israeli auawe bila kufanya uchunguzi na kupata ukweli wake?
49 Rudini mahakamani. Wazee hawa wameshuhudia uongo dhidi ya Susana."
50 Basi, harakaharaka watu wakarudi nyumbani kwa Yoakimu. Wazee wakamwambia Danieli, "Haya kijana! Njoo uketi karibu nasi, utuambie hayo unayojua. Wewe ni kijana bado lakini Mungu amekujalia hekima!"
51 Danieli akawaambia, "Watenganisheni hao waamuzi wawili, nami nitawahoji mmojammoja."
52 Walipotenganishwa, Danieli akamwita mmoja wao, akamwambia, "Wewe ni mzee lakini mwovu! Sasa utalipa kutokana na dhambi zako zote ulizotenda hapo awali.
53 Wewe ulihukumu bila kutumia haki; asiye na hatia ukampatiliza na mwovu ukamwachilia. Ingawa Bwana alisema, Mtu asiye na hatia, na mwenye haki, usimwue!"
54 Haya basi, kama kweli ulimwona waziwazi hebu: niambie, walikuwa chini ya mti gani?" Mzee huyo akajibu, "Chini ya msandarusi."
55 Hapo Danieli akasema, "Barabara! Umejitia kitanzi kwa moyo wako mwenyewe! Sasa hivi malaika wa Mungu amekwisha pewa amri ya kukukata vipande viwili.
56 Kisha Danieli akamtoa huyo mzee, akaagiza yule mzee mwingine aletwe. Alipofika, Danieli akamwuliza, "Wewe ni mzawa wa Kanaani na si mzawa wa Yuda! Uzuri umekuhadaa mzee! Tamaa za mwili zimeupotosha moyo wako!
57 Binti za Israeli wamekuwa wakitembea nawe kwa kuwa walikuogopa, lakini huyu binti wa Yuda hakukubaliana na uovu wako.
58 Haya basi, hebu niambie: walikuwa chini ya mti gani ulipowaona wakifanya mapenzi?" Naye akajibu, "Chini ya mwaloni.
59 Danieli akasema, "Barabara! Nawe pia umejitia kitanzi kwa uongo wako mwenyewe. Malaika wa Mungu anakungoja mwenye upanga na atakukata vipande viwili. Nyote wawili mtaa ngamizwa."
60 Kisha, watu wote waliojumuika hapo wakapaaza sauti na kumsifu Mungu awaokoaye wenye kumtumainia.
61 Basi, wakawavamia wale wazee wawili ambao Danieli alithibitisha uongo wa shtaka lao kwa maneno yao wenyewe.
62 Kufuatana na sheria ya Mose, wanaotoa ushahidi wa uongo watapewa adhabu ileile ambayo aliyeshtakiwa angepewa. Basi, hao wazee wawili wakauawa na mama huyo asiye na hatia akaokolewa siku hiyo.
63 Hilkia, baba yake Susana, mama yake, mumewe Yoakimu na ndugu zake, wakamsifu Mungu kwa sababu Susana hakupatikana na hatia yoyote dhidi ya shtaka hilo la aibu.
64 Tangu siku hiyo, Danieli akaheshimika sana kati ya watu wake.

Generic placeholder image