14

Danieli na Makuhani wa Beli
1 Baada ya kifo cha mfalme Astiage, Koreshi, Mpersi, alishika ufalme.
2 Danieli alikuwa rafiki mwandani wa mfalme naye mfalme alimheshimu kuliko wenzake wote.
3 Basi, Wababuloni walikuwa na sanamu ya mungu aitwaye Beli; kila siku waliitolea dhabihu: pishi kumi na mbili za nafaka, kondoo arubaini na lita mia mbili na arubaini za divai.
4 Mfalme Koreshi aliiheshimu sanamu hiyo, akawa anakwenda kuiabudu kila siku. Lakini Danieli alimwabudu Mungu wake binafsi.
5 Basi, siku moja, mfalme akamwuliza Danieli, "Kwa nini humwabudu Beli?" Danieli akamjibu, "Mimi siabudu sanamu ambazo zimetengenezwa na watu. Mimi namwabudu Mungu aliye hai, Mungu Muumba wa mbingu na dunia na mwenye mamlaka juu ya wanadamu wote."
6 Hapo, mfalme akamwambia Danieli, "Je, wewe huamini kwamba, Beli ni mungu wetu aliye hai? Huoni jinsi anavyokula na kunywa kwa wingi kila siku?" "Danieli akacheka na kumwambia mfalme, "Ewe mfalme, usidanganyike! Mungu huyo ni udongo ndani na shaba nje; hali wala hanywi chochote!"
8 Hapo, mfalme alikasirika, akawaita makuhani wake, akawaambia, "Msiponiambia ni nani anayekula vyakula vyote hivyo mtakufa!
9 Lakini mkinihakikishia kwamba Beli ndiye anayevila, basi, Danieli atauawa, kwa sababu amemkufuru Beli." Naye Danieli akamwambia mfalme, "Sawa; na iwe kama ulivyosema!"
10 Basi, mfalme akaingia ndani ya hekalu la Beli pamoja na Danieli. Humo ndani mlikuwa na makuhani sabini wa Beli, pamoja na wake zao na watoto wao.
11 Makuhani hao wakamwambia mfalme, "Sasa, sisi tutatoka nje. Nawe, ee mfalme, mwandalie. Beli chakula na kumwekea gudulia la divai, kisha ufunge mlango kabisa na kuweka mhuri kwa pete yako mwenyewe.
12 Ukifika kesho asubuhi ukakuta kwamba Beli hajala kila kitu, basi, hapo na tuuawe; la sivyo, itamlazimu Danieli auawe, kwa sababu ametusingizia bure."
13 Makuhani hawakuwa na wasiwasi, maana chini ya meza walikuwa wameweka mlango wa siri waliopitia kila mara na kula vyakula hivyo.
14 Basi, makuhani wakatoka nje, naye mfalme akamwandalia Beli vyakula. Kisha, Danieli akaamuru watumishi wake walete majivu na kuyanyunyizia kila mahali hekaluni, bila mtu mwingine kujua isipokuwa mfalme peke yake. Kisha wakatoka nje, wakaufunga mlango na kuutia mhuri kwa pete ya mfalme; kisha wakaenda zao.
15 Usiku, kama ilivyokuwa kawaida yao, wale makuhani walikuja pamoja na wake zao na watoto wao, wakala chakula chote na kunywa divai yote.
16 Mapema kesho yake asubuhi, mfalme akaenda hekaluni pamoja na Danieli.
17 Basi, mfalme akamwuliza Danieli, "Je, mihuri iko sawasawa?" Danieli akajibu, "Naam, mfalme; iko sawasawa.
18 Mara tu mlango ulipofunguliwa, mfalme aliitazama meza tupu mbele ya Beli, akapaaza sauti, "Wewe u mkuu ewe Beli! Kwako hamna udanganyifu, hamna hata kidogo!"
19 Lakini Danieli akaangua kicheko, na kumzuia mfalme asiingie ndani. Kisha akamwambia, "Hebu tazama sakafuni, mfalme! Nyayo hizo zote ni za kina nani?"
20 Mfalme akasema, "Naam, naona nyayo za wanaume, wanawake na watoto."
21 Basi, mfalme hasira zikampanda, akaamuru makuhani na jamaa zao wote wakamatwe na kuletwa kwake. Nao wakamwonyesha milango ya siri waliyozoea kuingilia ndani kula vyakula vilivyowekwa mezani.
22 Basi, mfalme akaamuru wauawe; na ile sanamu ya Beli akamwachia Danieli, naye akaivunjavu nja pamoja na hekalu lake. Danieli anaua Joka
23 Wababuloni vilevile waliiabudu joka moja kubwa sana.
24 Siku moja, mfalme akamwambia Danieli, "Huwezi kukana kuwa huyu si mungu hai. Kwa hiyo mwabudu!"
25 Danieli akasema, "Mimi humwabudu Bwana Mungu wangu; yeye peke yake ndiye Mungu aliye hai.
26 Kama wewe mfalme utaniruhusu, mimi nitaliua hilo joka bila kutumia panga wala rungu." Mfalme akamwambia, "Haya! Nakuruhusu!"
27 Basi, Danieli akachukua lami, mafuta na nywele, akavitokosa pamoja na kufanya donge, akalitupia mdomoni joka hilo, nalo likameza; ghafla likapasuka. Hapo Danieli akasema, "Haya! Liangalieni joka hilo ambalo mmekuwa mkiliabudu!'
28 Wababuloni walipoona jambo hilo, walifanya maandamano ya hasira dhidi ya mfalme, wakapaaza sauti wakisema, "Mfalme amekuwa Myahudi! Yeye alimwangamiza Beli na makuhani akawachinja! Na sasa ameliua joka letu."
29 Basi, wakamwendea mfalme, wakasema, "Tutolee huyo Danieli! La sivyo, tutakuua pamoja na jamaa yako!"
30 Mfalme alipoona kwamba wamembana sana na kumshurutisha, akamkabidhi Danieli kwao. Danieli katika pango la simba
31 Basi, wakamchukua Danieli na kumtumbukiza ndani ya pango la simba, naye akakaa humo kwa muda wa siku sita.
32 Humo pangoni mlikuwa na simba saba ambao kwa desturi walikuwa wanalishwa binadamu wawili na kondoo wawili kila siku. Kwa muda wa siku sita, simba hao hawakupewa chochote ili wamtafune Danieli mara moja.
33 Wakati huo, nabii Habakuki alikuwa huko Yuda. Basi, Habakuki alikuwa amepika mchuzi na mkate, akaviweka ndani ya bakuli, na akawa anakwenda shamba kuwapelekea wavunaji.
34 Lakini, malaika wa Bwana akamwambia Habakuki, "Peleka chakula hicho Babuloni, kwa Danieli"
35 aliye katika pango la simba. Habakuki akasema, "Bwana, mimi sijapata kufika Babuloni, wala sijui chochote kuhusu pango hilo.
36 Hapo malaika wa Bwana akamshika Habakuki nywele, akamnyanyua na kumpeleka kasi Kisha kwa upepo hadi Babuloni. Kisha akamweka palepale ukingoni mwa pango la hao simba.
37 Basi, Habakuki akapaaza sauti, "Danieli! Danieli! Chukua chakula ambacho Mungu amekuletea:"
38 Danieli akasema, "Ee Mungu, kweli umenikumbuka! Wewe kamwe huwaachi watu wakupendao katika taabu."
39 Basi, Danieli akainuka, akala. Malaika wa Bwana akamrudisha Habakuki nyumbani kwake.
40 Mnamo siku ya saba, mfalme alikwenda kwenye pango la simba kumwomboleza Danieli. Lakini alipofika na kuchungulia ndani, alimwona Danieli ameketi, salama salimini.
41 Mfalme akapaaza sauti na kusema, "Ee Bwana, Mungu wa Danieli! Wewe ni mkuu, na hakuna Mungu mwingine ila wewe!"
42 Basi, akamtoa Danieli mle pangoni, na badala yake akawatupa ndani wale waliokuwa wanataka kumuua Danieli. Mara, wakararuliwa na simba na kuliwa mara moja, mfalme akiwa anatazama.

Generic placeholder image