8

Maono ya nne: Kikapu cha matunda
1 Bwana Mwenyezi-Mungu alinijalia maono mengine: Niliona kikapu kilichojaa matunda ya kiangazi.
2 Naye Mwenyezi-Mungu akaniuliza: “Amosi, unaona nini?” Nami nikamjibu, “Naona kikapu cha matunda ya kiangazi.” Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Mwisho umewafikia watu wangu wa Israeli. Sitavumilia tena maovu yao.
3 Siku hiyo, nyimbo za ikulu zitakuwa maombolezo. Kutakuwa na maiti nyingi, nazo zitatupwa nje kimyakimya.”

Mungu ataiadhibu Israeli
4 Sikilizeni enyi mnaowakandamiza wanyonge na kuwaletea maangamizi fukara wa nchi.
5 Mnajisemea mioyoni mwenu: “Sikukuu ya mwezi mwandamo itakwisha lini ili tuanze tena kuuza nafaka yetu? Siku ya Sabato itakwisha lini ili tupate kuuza ngano yetu? Tutatumia vipimo hafifu vya wastani na uzito, tutadanganya watu kwa mizani isizo sawa,
6 hata kuuza ngano hafifu kwa bei kubwa. Tutaweza kununua watu fukara kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya kandambili.”
7 Mwenyezi-Mungu, fahari ya Yakobo, ameapa: “Hakika, sitayasahau matendo yao maovu.
8 Kwa hiyo, dunia itatetemeka na kila mtu nchini ataomboleza. Nchi yote itayumbayumba; itapanda na kushuka, kama yanavyojaa na kupwa maji ya mto Nili!”
9 Bwana Mwenyezi-Mungu asema, “Siku hiyo nitalifanya jua litue adhuhuri, na kuijaza nchi giza mchana.
10 Sherehe zenu nitazigeuza kuwa kilio, na nyimbo zenu za furaha kuwa maombolezo. Nitawafanya nyote mvae magunia kwa huzuni na kunyoa vipara vichwa vyenu, kama kuomboleza kifo cha mtoto wa pekee; na siku ya mwisho itakuwa ya uchungu mkubwa.”
11 Bwana Mwenyezi-Mungu asema, “Siku zaja ambapo nitaleta njaa nchini. Lakini sio njaa na kiu ya chakula na maji, bali njaa ya kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu.
12 Watu watatangatanga kutoka bahari hata bahari, kutoka upande wa kaskazini mpaka mashariki. Watakimbia huko na huko wakitafuta neno la Mwenyezi-Mungu, lakini hawatalipata.
13 “Siku hiyo, hata vijana wenye afya, wa kiume kwa wa kike, watazimia kwa kiu.
14 Wale wanaoapa kwa mungu wa uongo wa Samaria, na kusema: ‘Kwa nafsi ya mungu wako ee Dani’; na, ‘Kwa nafsi ya mungu wa Beer-sheba’, wote wataanguka na hawatainuka tena kamwe.”

Generic placeholder image