9

Adhabu ya Mungu
1 Nilimwona Mwenyezi-Mungu amesimama kando ya madhabahu, naye akaniamuru: “Zipige hizo nguzo za hekalu mpaka misingi yake itikisike. Zivunje hizo nguzo ziwaangukie watu vichwani. Wale watakaosalia nitawaua kwa upanga; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika, naam, hakuna atakayetoroka.
2 Wajapojichimbia njia ya kwenda kuzimu, huko nitawachukua kwa mkono wangu; wajapopanda mbinguni, nitawaporomosha chini.
3 Wajapojificha juu ya mlima Karmeli, huko nitawasaka na kuwachukua; wajapojificha mbali nami vilindini mwa bahari, humo nitaliamuru joka la baharini liwaume.
4 Wajapochukuliwa mateka na adui zao, huko nitatoa amri wauawe kwa upanga. Nitawachunga kwa makini sana niwatendee mabaya na si mema.”
5 Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi, anaigusa ardhi nayo inatetemeka na wakazi wake wanaomboleza; dunia nzima inapanda na kushuka kama kujaa na kupwa kwa mto Nili wa Misri.
6 Mwenyezi-Mungu amejenga makao yake mbinguni, nayo dunia akaifunika kwa anga; huyaita maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya nchi kavu. Mwenyezi-Mungu, ndilo jina lake!

Marekebisho baada ya uharibifu
7 Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Kwangu mimi, nyinyi Waisraeli, hamna tofauti yoyote na watu wa Kushi! Niliwatoa Wafilisti kutoka Krete, na Waashuru kutoka Kiri, kama nilivyowatoa nyinyi kutoka Misri.
8 Mimi, Bwana Mwenyezi-Mungu nautazama ufalme wenye dhambi, na nitauangamiza kabisa kutoka duniani. Lakini sitawaangamiza wazawa wote wa Yakobo.
9 “Tazama, nitatoa amri, na kuwapepeta Waisraeli kati ya mataifa kama mtu achekechavyo nafaka niwakamate wote wasiofaa.
10 Wenye dhambi miongoni mwa watu wangu, watafia vitani kwa upanga; hao ndio wasemao: ‘Maafa hayatatukumba wala kutupata!’
11 “Siku yaja nitakapoisimika nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitazitengeneza kuta zake, na kusimika upya magofu yake. Nitaijenga upya kama ilivyokuwa hapo zamani.
12 Nao Waisraeli watamiliki mabaki ya Edomu na mataifa yote yaliyokuwa yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hivyo.
13 “Wakati waja kwa hakika, ambapo mara baada ya kulima mavuno yatakuwa tayari kuvunwa; mara baada ya kupanda mizabibu utafuata wakati wa kuvuna zabibu. Milima itabubujika divai mpya, navyo vilima vitatiririka divai.
14 Nitarekebisha hali ya watu wangu Waisraeli. Watajenga miji yao iliyoharibiwa na kuishi humo; watapanda mizabibu na kunywa divai yake; watalima mashamba na kula mazao yake.
15 Nitawasimika katika nchi yao, wala hawatang'olewa tena kutoka katika nchi niliyowapa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

Generic placeholder image