1 Maono ya Obadia. Mambo aliyosema Bwana Mwenyezi-Mungu kuhusu taifa la Edomu.

Mwenyezi-Mungu ataadhibu Edomu
Tumepata habari kutoka kwa Mwenyezi-Mungu; mjumbe ametumwa kati ya mataifa: “Inukeni! Twende tukapigane na Edomu!”
2 Mwenyezi-Mungu aliambia taifa la Edomu: “Nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa, utadharauliwa kabisa na wote.
3 Kiburi chako kimekudanganya: Kwa kuwa mji wako mkuu ni ngome ya miamba imara na makao yako yapo juu milimani, hivyo wajisemea, ‘Nani awezaye kunishusha chini?’
4 Hata ukiruka juu kama tai, ukafanya makao yako kati ya nyota, mimi nitakushusha chini tu. Nasema mimi Mwenyezi-Mungu.
5 “Kama wezi au wanyang'anyi wangekujia usiku, je, wasingechukua tu kiasi cha kuwatosha? Ikiwa wavunaji zabibu wangekujia, je, wasingekuachia kiasi kidogo tu? Lakini wewe, adui zako wamekuangamiza kabisa.
6 Enyi wazawa wa Esau, mali zenu zimetekwa; hazina zenu zote zimeporwa!
7 Washirika wenzenu wamewadanganya, wamewafukuza nchini mwenu. Mliopatana nao wamewashinda vitani, rafiki wa kutegemewa ndio waliokutegea mitego, nawe hukuelewa yaliyokuwa yanatendeka.
8 Mimi Mwenyezi-Mungu nakuuliza hivi: Je, siku hiyo, sitawaangamiza wenye hekima kutoka Edomu na wenye maarifa kutoka mlima Esau?
9 Ewe Temani, mashujaa wako watatishika na kila mtu atauawa mlimani Esau.

Sababu za Edomu kuadhibiwa
10 “Kwa sababu ya matendo maovu mliyowatendea ndugu zenu wazawa wa Yakobo, mtaaibishwa na kuangamizwa milele.
11 Siku ile mlisimama kando mkitazama tu, wakati wageni walipopora utajiri wao, naam, wageni walipoingia malango yao na kugawana utajiri wa Yerusalemu kwa kura. Kwa hiyo nanyi mlitenda kama wazawa wao.
12 Msingalifurahia siku hiyo ndugu zenu walipokumbwa na mikasa; msingaliwacheka Wayuda na kuona fahari wakati walipoangamizwa; msingalijigamba wenzenu walipokuwa wanataabika.
13 Msingeliingia katika mji wa watu wangu, siku walipokumbwa na maafa; msingelipora mali zao, siku hiyo ya maafa yao.
14 Msingelisimama kwenye njia panda na kuwakamata wakimbizi wao; wala msingeliwakabidhi kwa adui zao wale waliobaki hai.

Mungu atayahukumu mataifa
15 “Siku inakaribia ambapo mimi Mwenyezi-Mungu nitayahukumu mataifa yote. Kama mlivyowatendea wengine, ndivyo mtakavyotendewa, mtalipwa kulingana na matendo yenu.
16 Maana, kama walivyokunywa kikombe cha ghadhabu yangu kwenye mlima wangu mtakatifu ndivyo na mataifa jirani yatakavyokunywa; watakunywa na kupepesuka, wataangamia kana kwamba hawakuwahi kuwapo duniani.

Waisraeli watashinda
17 “Lakini mlimani Siyoni watakuwapo wale waliosalimika nao utakuwa mlima mtakatifu. Wazawa wa Yakobo wataimiliki tena nchi iliyokuwa yao.
18 Wazawa wa Yakobo watakuwa kama moto na wazawa wa Yosefu kama miali ya moto. Watawaangamiza wazawa wa Esau kama vile moto uteketezavyo mabua makavu, asinusurike hata mmoja wao. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.
19 Wale wanaokaa Negebu wataumiliki mlima Esau; wale wanaokaa Shefela wataimiliki nchi ya Wafilisti. Waisraeli watamiliki nchi za Efraimu na Samaria na watu wa Benyamini wataimiliki nchi ya Gileadi.
20 Waisraeli walio uhamishoni Hala wataimiliki Foinike hadi Sarepta. Watu wa Yerusalemu walio uhamishoni Sefaradi wataimiliki miji ya Negebu.
21 Waokoaji watapanda juu ya mlima Siyoni ili kuutawala mlima Esau; naye Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye Mfalme.”

Generic placeholder image