13

1 “Siku hiyo, kutatokea chemchemi ya kuwatakasa dhambi na unajisi wazawa wa Daudi na wakazi wote wa Yerusalemu.
2 Wakati huo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, majina ya vinyago vya miungu nchini nitayaondoa, wala hayatakumbukwa tena. Na wanaojidai kuwa manabii nitawaondolea mbali pamoja na tamaa zao za kuabudu sanamu.
3 Mtu yeyote akijidai kuwa nabii, baba na mama yake waliomzaa watamwambia, ‘Unapaswa kufa kwa kuwa unasema uongo kwa jina la Mwenyezi-Mungu’. Na haohao wazazi wake watamchoma kisu akiwa anatabiri.
4 Siku hiyo, kila nabii atayaonea aibu maono yake anapotabiri. Hawatavaa mavazi ya manyoya ili kudanganya watu,
5 bali kila mmoja atasema, ‘Mimi si nabii. Mimi ni mkulima tu; nimeimiliki ardhi tangu ujana wangu’.
6 Na mtu akimwuliza mmoja wao, ‘Vidonda hivi ulivyo navyo mgongoni vimetoka wapi?’ Yeye atajibu, ‘Vidonda hivi nilivipata katika nyumba ya rafiki zangu.’”
7 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Amka, ee upanga! Inuka umshambulie mchungaji wangu; naam, mchungaji anayenitumikia. Mpige mchungaji na kondoo watawanyike. Nitaunyosha mkono wangu, kuwashambulia watu wadhaifu.
8 Theluthi mbili za watu katika nchi zitaangamizwa; ni theluthi moja tu itakayosalimika.
9 Theluthi hiyo moja itakayosalia, nitaijaribu na kuitakasa, kama mtu asafishavyo fedha, naam, kama ijaribiwavyo dhahabu. Hapo wao wataniomba mimi, nami nitawajibu. Nitasema, ‘Hawa ni watu wangu’, nao watasema, ‘Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu wetu.’”

Generic placeholder image