3
Maono ya nne: Kuhani mkuu Yoshua 1 Katika maono mengine, Mwenyezi-Mungu alinionesha kuhani mkuu Yoshua amesimama mbele ya malaika wa Mwenyezi-Mungu, na upande wake wa kulia amesimama Shetani kumshtaki. 2 Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwambia huyo Shetani, “Mwenyezi-Mungu na akulaani, ewe Shetani! Naam, Mwenyezi-Mungu aliyeuteua mji wa Yerusalemu na akulaani! Mtu huyu ni kama kinga kilichonyakuliwa kutoka motoni!” 3 Kuhani mkuu Yoshua alikuwa amesimama mbele ya malaika, akiwa amevaa mavazi machafu. 4 Malaika akawaambia watumishi wake, “Mvueni kuhani mkuu Yoshua mavazi yake machafu.” Kisha akamwambia kuhani mkuu Yoshua, “Tazama, nimeiondoa dhambi yako, nami nitakupa mavazi ya thamani.” 5 Kisha akawaambia wamvike kilemba safi kichwani. Hivyo, wakamvika kilemba safi na mavazi; naye malaika wa Mwenyezi-Mungu alikuwa amesimama hapo. 6 Malaika wa Mwenyezi-Mungu akamwonya kuhani mkuu Yoshua, akamwambia, 7 “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Ukifuata mwongozo wangu na kuyazingatia maagizo niliyokupa, basi, utaisimamia nyumba yangu na nyua zake. Nami nitakuwezesha kuingia katika utumishi wangu kama hawa wanaosimama mbele yangu. 8 Sasa sikiliza kwa makini, ewe Yoshua, kuhani mkuu; sikilizeni pia enyi makuhani wenzake mlio pamoja naye, nyinyi mlio ishara ya wakati mzuri ujao: Nitamleta mtumishi wangu aitwaye Tawi. 9 Kumbukeni kuwa nimeweka mbele ya Yoshua jiwe moja lenye nyuso saba. Nami nitachora maandishi juu yake, na kwa siku moja tu, nitaiondoa dhambi ya nchi hii. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema. 10 Siku hiyo, kila mmoja wenu atamwalika mwenzake kufurahia amani na utulivu katika shamba lake la mizabibu na la mitini.’”