12

Miriamu anaadhibiwa
1 Kisha Miriamu na Aroni walianza kumsema vibaya Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa.
2 Wakasema, “Hivi kwani Mwenyezi-Mungu amezungumza kwa kumwagiza Musa peke yake? Je, hajazungumza nasi pia?” Mwenyezi-Mungu aliyasikia maneno hayo.
3 (Musa alikuwa mtu mnyenyekevu kuliko watu wengine wote waliokuwa duniani.)
4 Halafu ghafla, Mwenyezi-Mungu akawaambia Musa, Aroni na Miriamu, “Njoni katika hema la mkutano, nyinyi watatu.” Basi, wote watatu wakaenda kwenye hema la mkutano.
5 Hapo Mwenyezi-Mungu akashuka katika nguzo ya wingu, akasimama kwenye mlango wa hema, akawaita Aroni na Miriamu. Wote wawili wakasogea mbele.
6 Kisha Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Sikilizeni maneno yangu: Kama kuna nabii miongoni mwenu, mimi Mwenyezi-Mungu hujifahamisha kwake katika maono na kuongea naye katika ndoto.
7 Lakini kumhusu mtumishi wangu Musa, hali ni tofauti kabisa. Yeye ana jukumu la kuwatunza watu wangu wote.
8 Mimi huongea naye ana kwa ana, waziwazi na si kwa kutumia mafumbo. Yeye huliona umbo langu mimi Mwenyezi-Mungu. Kwa nini, basi, hamkuogopa kusema vibaya dhidi ya mtumishi wangu Musa?”
9 Hapo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi yao, akaondoka, akaenda zake.
10 Wingu lilipoondoka juu ya hema la mkutano, Miriamu alionekana ana ukoma, mweupe kama theluji. Aroni alipogeuka na kumtazama Miriamu, alishangaa kuona kuwa ameshikwa na ukoma.
11 Hapo, Aroni akamwambia Musa, “Ewe bwana wangu, usituadhibu kwa kuwa tumetenda mambo ya kipumbavu na kufanya dhambi.
12 Usimfanye Miriamu awe kama mtu aliyezaliwa mfu, ambaye karibu nusu ya mwili wake umelika.”
13 Musa akamlilia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nakusihi, ee Mungu, umponye.”
14 Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Kama baba yake angemtemea mate usoni, je, hangeaibika kwa siku saba? Basi, mtoe nje ya kambi akae huko muda wa siku saba, kisha unaweza kumruhusu arudi kambini.”
15 Kwa hiyo, Miriamu akafukuzwa nje ya kambi kwa muda wa siku saba. Watu hawakuanza tena safari hadi Miriamu aliporudishwa tena kambini.
16 Baada ya hayo, watu walifanya safari kutoka Haserothi, wakapiga kambi katika jangwa la Parani.

Generic placeholder image