17

Fimbo ya Aroni
1 Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa,
2 “Waambie Waisraeli wakuletee fimbo kumi na mbili, kila kiongozi wa kabila fimbo moja. Liandike jina la kila mmoja wao kwenye fimbo yake,
3 na jina la Aroni liandike juu ya fimbo inayowakilisha kabila la Lawi. Patakuwa na fimbo moja kwa kila kiongozi wa kabila.
4 Zichukue fimbo hizo katika hema la mkutano na kuziweka mbele ya sanduku la agano, mahali ambapo mimi hukutana nawe.
5 Fimbo ya mtu nitakayemchagua itachipua. Kwa njia hii nitayakomesha manunguniko ya Waisraeli juu yenu.”
6 Musa akaongea na watu wa Israeli. Viongozi wao wote wakampa kila mmoja fimbo yake kulingana na kabila lake jumla zikawa fimbo kumi na mbili. Fimbo ya Aroni iliwekwa pamoja na fimbo hizo.
7 Musa akaziweka fimbo hizo zote mbele ya Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano.
8 Kesho yake asubuhi, Musa alikwenda katika hema la mkutano. Humo, aliikuta fimbo ya Aroni wa kabila la Lawi, imechipua na kutoa vichipukizi vilivyochanua maua na kuzaa matunda mabivu ya mlozi.
9 Kisha Musa akazitoa fimbo zote hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawaonesha Waisraeli wote, na kila kiongozi akachukua fimbo yake.
10 Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Irudishe fimbo ya Aroni mbele ya sanduku la agano. Hiyo itatunzwa mahali hapo, na ni onyo kwa waasi hao kwamba wasipoacha kuninungunikia, watakufa.”
11 Musa akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
12 Waisraeli wakamwambia Musa, “Angalia sasa! Tunaangamia! Tumekwisha! Sote tumekwisha.
13 Kila mtu atakayekaribia, hema la Mwenyezi-Mungu atakufa. Je, tutaangamia sote?”

Generic placeholder image