Generic placeholder image

MARIA MAMA WA MUNGU
SALA ZA MCHANA

chagua SALA KABLA YA ADHUHURI
chagua SALA BAADA YA ADHUHURI
Kwa SALA YA ADHUHURI: endelea hapo chini

ADHUHURI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI
E Bwana Mbarikiwa
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.

Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.

Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;.
Na yote yanafanyika.
Kadiri unavyotaka.

Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu.
Milele inayodumu.

ANT.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.

Zab.123 Kuomba huruma
Wale vipofu wawili walipaaza sauti wakisema, Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuonee huruma! (Mt.20:30)

Ninakuinulia macho yangu, Ee Mungu*
unayekaa huko juu mbinguni.

Kama watumishi wamtegemeavyo bwana wao,*
kama mjakazi amtegemeavyo bibi yake,

ndivyo tunavyokutegemea wewe, Ee Mungu, Mungu wetu,*
mpaka hapo utakapotuonea huruma.

Utuhurumie, Ee Mungu, utuhurumie,*
maana tumedharauliwa mno.

Tumedharauliwa na wadhalimu wenye kiburi,*
tumepuuzwa vya kutosha na matajiri.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.124 Mungu kinga yetu
Bwana alimwambia Paulo katika ono: 'Usiogope,...maana mimi nipo pamoja nawe' (Mate.18:9-10)

Haya Israeli, sasa useme:*
"Kama Mungu asingalikuwa upande wetu;

kweli Mungu asingalikuwa upande wetu,*
wakati ule tuliposhambuliwa na watu,

hakika tungalimezwa wazimawazima,*
wakati hasira zao zilipotuwakia.

Hapo tungalikumbwa na gharika/
tungalifunikwa na mto wa maji,*
mkondo wa maji ungalituchukua!"

Atukuzwe Mungu,*
asiyetuacha makuchani mwao.

Tumeponyoka kama ndege*
katika mtego wa wawindaji!

Mtego umeteguliwa,*
nasi tukaokoka.

Msaada wetu watoka kwa Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Zab.125 Usalama wa watu wa Mungu
Amani na iwe kwa Israeli - Wateule wa Mungu (Gal.6:16)

Wale wanaomtumainia Mungu,/
ni kama mlima Sion,*
ambao hautikisiki, bali uko imara daima.

Kama Yerusalemu inavyozungukwa na milima,/
ndivyo Mungu awazungukavyo watu wake,*
tangu sasa na hata milele.

Maana hatawaruhusu waovu watawale nchi ya waadilifu;*
Wasije waadilifu nao wakafanya maovu.

Ee Mungu, uwe mwema kwa watu wema,*
kwa wale wanaozitii amri zako.

Adhabu unayowapa watu waovu*
uwape pia wanaokiuka miongozo yako.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant.: Maria aliyaweka hayo yote, akayatafakari moyoni mwake.

SOMO: Zek.9:9a
Furahi sana, Ee binti Sion; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu.

K. Miisho yote ya dunia inastaajabu, aleluya.
W. Imeuona uwezo wa kuokoa wa Mungu wetu, aleluya.

SALA:
Tuombe: Mungu, Baba yetu, kwa kuwa umewapa wanadamu mwokozi kwa njia ya Maria mwenye heri, bikira na mama, utujalie tuweze kuhisi nguvu ya maombezi yake wakati anapotuombea kwa Yesu Kristo, Mwanao, chanzo cha uzima, anayeishi na kutawala daima na milele.

W. Amina.

K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.