JANUARI 3 KIPINDI CHA NOEL
MASOMO
SOMO 1: 1Yn.2:29–3:6
Wapenzi: Kama mkijua ya kuwa yeye ni mwenye haki, jueni ya kuwa kila atendaye haki amezaliwa na yeye. Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo.
Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu
wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye;
kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye
alivyo mtakatifu. Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa
yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi
dhambi, kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1,3-6
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
2. Miisho yote ya dunia imeuona,
Wokovu wa Mungu wetu,
Mshangilieni Bwana nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
3. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO: Ebr.1:1-2
Aleluya, aleluya!
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi na kwa namna nyingi na baba zetu kwa kinywa cha
manabii, siku hizi zilizo za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya!
INJILI: Yn.1:29-34
Siku ile, Yohane alimwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye
dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu; ambaye
amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe
kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohane akashuhudia akisema,
Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye Akaka juu yake. Wala mimi sikumjua;
lakini yeye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji,
huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa
Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ni pendo la pekee sana kwetu sisi kuitwa wana wa Mungu. Lakini kwa vile pengine tunashindwa kutenda
haki kama wale wasiozaliwa na yeye, tuombe:
Kiitikio: Kwa huruma yako Bwana, utusikie.
1. Uzidi kuwaneemesha viongozi wa Kanisa katika juhudi zao, za kukutambulisha kwa watu kwa mahubiri yao.
2. Ulimwengu wote umkiri Kristo wako, kuwa ndiye Mwana Kondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia.
3. Utujalie sisi sote kulithamini tendo la kujitakasa dhambi zetu, kusudi tushirikishwe utakatifu wako.
4. Uwapokee marehemu wetu waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu, ili washiriki uzima wa milele huko
mbinguni.
Ee Bwana Mungu wetu, twakiri kuwa wabatizwa wote tunao wajibu wa kumshuhudia Mwanao mbele ya watu kuwa
ndiye Mwana Wako. Utusamehe dhambi zetu tupate kuwa wana Wako kweli. Tunaomba hayo kwa njia ya huyo Kristo
Bwana wetu. Amina.