MAOMBI:KAWAIDA YA KUTABARUKU KANISA (Ibada ifanyikapo katika kanisa husika) Kwa njia ya imani Mungu ametufanya kuwa hekalu lake hai na watu wake wa kikuhani. Tumwombe Mungu kwa ajili ya ustawi wa Kanisa na kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Kiitikio: Pokea ombi letu. 1. Uwabariki Papa wetu F., Askofu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa lako lililosafishwa na kuimarishwa na Roho Mtakatifu ili, kwa mafundisho, sala na maongozi yao, liweze kuwakusanya watu wote katika zizi moja chini ya Mchungaji mmoja. Ee Bwana. 2. Ili viongozi wetu wa serikali na wa vyama mbalimbali vya siasa wapate neema yako na, kwa kushirikiana na viongozi wa Kanisa, watetee uhai, haki, amani na usawa kwa raia wote. Ee Bwana. 3. Ili kwa ukumbusho wa kutabarukiwa Kanisa hili, jumuiya yetu ipate tena ile hadhi furahivu ya kuwa milki yako Baba na bibi arusi wa Mwanao, Yesu Kristo. Ee Bwana. 4. Ili wafanyakazi, wakulima, wana Vyuo, wanafunzi na wote wanaosali katika kanisa hili wazidishiwe na Roho Mtakatifu furaha na ari ya kuyavumilia mahangaiko yao katika wajibu zao za kila siku. Ee Bwana. 5. Wote wenye matatizo mbalimbali ya kimwili na kiroho wasikie uwepo wako Bwana ulio hai na wenye faraja; na marehemu wetu wapokelewe katika makao yako huko mbinguni. Ee Bwana. Ee Mungu unayetukusanya katika nyumba yako ili tukusifu na kuyaadhimisha mafumbo ya wokovu, usikilize maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKUKUU YA BIKIRA MARIA Katika Bikira Maria, Mama wa Mkombozi wetu Yesu Kristo, Mungu ametufunulia ukubwa wa pendo lake; kwa maombezi yake tumwombe Mungu kwa unyenyekevu tukisema: Kiitikio: Pokea ombi letu. 1. Kwa ajili ya Baba Mtakatifu wetu F., Askofu wetu F. na Wachungaji wote wa Kanisa lako, ili kwa mfano wa Bikira Maria mpole, mnyenyekevu na mwaminifu walitangulie na kuliongoza kwa Kristo kundi ulilowakabidhi. Ee Bwana. 2. Ili watawala wote wa dunia watumie vema vyeo vyao kwa ajili ya kuwalinda wanyonge, na kujenga amani na haki za raia wao. Ee Bwana. 3. Kwa ajili ya wote wamwaminio Kristo, ili Bikira Maria awasaidie kuonja furaha ya kumpokea Mwanao katika Sakramenti za Kanisa na kuishi kwa moyo mmoja na roho moja katika taabu na raha. Ee Bwana. 4. Ili sisi sote tudumu katika imani sahihi ya kikristo hata wakati wa majaribu; na tuwafariji wote wenye matatizo kwa kuwatembelea, kuwaombea na kuwahudumia kimwili na kiroho. Ee Bwana. 5. Ili marehemu wetu F. washirikishwe ufufuko wa Mwanao na uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana. Utujalie hayo kwa maombezi ya Bikira Maria na kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKUKUU ZA MITUME Mungu amewafanya mitume kuwa mashahidi na watangazaji wa kwanza wa ufufuko wa Mwanae Yesu Kristo. Tumwombe Mungu ili kazi ya kitume tuliyopewa kwa Ubatizo izae matunda ya wokovu. Kiitikio: Pokea ombi letu. 1. Ili Askofu wetu F. na wote walioirithi kazi ya mitume wako wazidi kuwa mfano bora wa umoja na upendo katika imani moja, Bwana mmoja na Ubatizo mmoja. Ee Bwana. 2. Kwa maombezi ya mtume (mitume F.) uwaamshie roho ya upendo, haki na amani duniani, wote wenye mamlaka katika serikali, vyama vya siasa na jumuiya mbalimbali. Ee Bwana. 3. Ili waamini wote wasikie sauti yako inayowaita kuishi kadiri ya wito uliowaitia na waimarishwe katika kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo mema. Ee Bwana. 4. Kwa ajili ya jumuiya (parokia) yetu, ili kwa kuumega mkate pamoja, na kwa mfano wa maisha yetu ya kitume, tukutukuze Wewe Mungu na kuwavutia kwako ndugu zetu waliojitenga na Kanisa lako. Ee Bwana. 5. Ili, kwa sala za mitume wako, ndugu zetu marehemu F. wapokelewe katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana. Hayo tunayaomba kwako, Ee Mungu Baba, kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKKUU ZA MASHAHIDI Kwa mfano wa watakatifu Mashahidi, imani na sala zetu kwa Mungu vinarutubishwa katika Kristo aliye kielelezo cha wafiadini wote. Tuombe msaada wa Mungu tukisema: Kiitikio: Mungu wa wafiadini, utusikie. 1. Ili Baba Mtakatifu wetu F., Askofu wetu F. na wote wenye Daraja Takatifu wachukue daima nafasi ya kwanza katika kukemea maovu na kumshuhudia Kristo kwa ujarisi wote. Ee Bwana. 2. Watawala wote wa dunia watoe kwa raia wao uhuru wa kukuabudu Wewe Mungu wa kweli. Ee Bwana. 3. Ili sote tuliokombolewa kwa damu ya Kristo tushirikiane na wote wenye nia njema katika kuishuhudia Injili yako bila woga hata kukiwa madhulumu dhidi ya imani yetu kwako. Ee Bwana. 4. Wote wanaodhulumiwa kwa ajili ya jina lako wafarijiwe kwa tumaini la kupewa taji la wafiadini na, kwa huruma yako, waokolewe na yule mwovu. Ee Bwana. 5. Marehemu wetu F. na wote waliomwaga damu yao kwa ajili ya kuitetea imani tuliyopewa na Mwanao wapewe uzima wa milele. Ee Bwana. Ee Mungu uliye kimbilio letu siku zote, katika taabu na raha, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKUKUU ZA WALIMU WA KANISA Mungu amewaweka katika Kanisa lake Watakatifu Walimu wa Kanisa waliojaa hekima, akili na karama ya kutoa mafundisho ya dini kwa ufasaha, ili kuwaimarisha waamini katika hekima itokayo juu. Katika Sikukuu hii (ya...) tumwombe tukisema: Kiitikio: Twakuomba utusikie. 1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa ari ya kuwa watetezi wa imani sahihi uliyotufundisha kwa njia ya Mwanao Yesu Kristo na walimu wote wa dini. Ee Bwana. 2. Watawala wote wa dunia wazingatie haki ya raia wao ya kupata mafunzo ya dini ya kweli na ya ulimwengu huu na ujao. Ee Bwana. 3. Ili wataalamu na waandishi wote wa makala ya kidini na kijamii wawe waaminifu katika kuwaelimisha watu wako katika ukweli na maadili mema. Ee Bwana. 4. Ili sisi sote tulioipokea imani kwa Ubatizo na tukaimarishwa kwa Sakramenti mbalimbali na kwa mafundisho ya walimu wa dini, tuwe na ari ya kuisoma Biblia na maandishi ya Walimu wa Kanisa lako tupate kuiishi na kuilinda vema imani yetu. Ee Bwana. 5. Marehemu wetu F. wapokelewe katika kundi la watakatifu wako huko mbinguni. Ee Bwana. Ee Mungu uyapokee maombi yetu, hata yale tusiyothubutu kuyataja. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKUKUU ZA WATAKATIFU WACHUNGAJI Mungu ni Mchungaji mwema anayelilisha kundi lake kwa neno lake na Sakramenti zake kwa njia ya Wachungaji wake. Tunapofanya Sikukuu ya mtakatifu F. tumwombe Mungu tukisema: Kiitikio: Pokea ombi letu. 1. Ili Baba Mtakatifu wetu F., Askofu wetu F., Maaskofu na Mapadre wote wa Kanisa lako wasichoke kuwahubiria waamini neno lako na kuwatakatifuza kwa Sakramenti zako. Ee Bwana. 2. Ili watawala wa dunia daima wakumbuke kuwa raia wao wanayo haki ya kuhudumiwa kimwili na kiroho chini ya uongozi wa serikali na wa dini takatifu. Ee Bwana. 3. Wazazi washirikiane vema na wachungaji wao na wote wenye nia njema katika kuwalea watoto wao na kuwapa mfano bora kwa maisha yao matakatifu. Ee Bwana. 4. Ili sisi sote tunaomfuasa Kristo Mchungaji mwema tuige mfano wa watakatifu kwa kupendana kidugu sisi kwa sisi na kwa kuwasaidia kadiri tuwezavyo wote wenye shida za kimwili na kiroho. Ee Bwana. 5. Uwapokee katika kundi la watakatifu wako ndugu zetu marehemu F. Ee Bwana. Ee Mungu Baba, uyapokee maombi yetu kwa njia ya Kristo Mwanao, Bwana na Mchungaji wetu mwema. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKUKUU ZA MABIKIRA Ndugu, watakatifu Mabikira wamemfuasa Kristo kwa moyo usiogawanyika. Tumwombe Mungu katika mahangaiko yetu ya kutafuta utakatifu. Ee Mfalme wa mabikira: Kiitikio: Twakuomba utusikie. 1. Ulijalie Kanisa lako kujiweka daima katika hali ya bibi arusi aliye tayari kwa ujio wa Bwana wake Yesu Kristo. Ee Bwana. 2. Ili viongozi wetu wa dini na wa serikali daima wahimize maadili mema yanayowapeleka watu wako kwenye utakatifu. Ee Bwana. 3. Wazazi na walezi wote wa watoto na vijana wetu wawe mifano myema kwa kuishi maisha safi na kuyakataa yote yaliyo kinyume cha imani sahihi na Amri Kuu ya mapendo. Ee Bwana. 4. Ili wote walio katika hatua ya malezi ya kimwili na kiroho waweze kukua katika moyo wa utii, heshima, shukrani na mapendo kwa Mungu na kwa watu wote. Ee Bwana. 5. Uwaondolee madoa ya dhambi marehemu wetu F. na kuwakaribisha kwako mbinguni. Ee Bwana. Ee Mungu Baba, uyapokee maombi yetu kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKUKUU ZA WATAWA Kwa wito wa utawa Mungu anawaita wanaume na wanawake wenye kujitakatifuza na kujitoa kabisa kwa ajili ya ufalme wake na kwa huduma ya ndugu zao katika imani. Tukikumbuka neema hii tuombe: Kiitikio: Twakuomba utusikie. 1. Baba Mtakatifu wetu F. na Maaskofu wote wa Kanisa lako wazidi kuyaenzi majimboni Mashirika ya kitawa yenye mwamko katika imani, matumaini na mapendo kwako na kwa taifa lako. Ee Bwana. 2. Ili wote wenye madaraka katika jamii zetu wasimamie vema mali za jamii zipate kutumika kwa ajili ya utukufu wako na ustawi wa watu wako. Ee Bwana. 3. Waamini wote wafuate mashauri ya kiinjili, wazazi wawalee watoto wao kadiri ya miito yao na wawe mfano bora katika kujitoa na kulihudumia Kanisa lako. Ee Bwana. 4. Ili wote walioitwa kuishi maisha ya wakfu wajikabidhi daima mikononi mwako na mwa watakatifu wako, wapate kudumu kiaminifu katika utume wao na wawe kivutio kwa vijana wengine wengi wenye wito huo. Ee Bwana. 5. Tunawakabidhi mikononi mwako ndugu zetu marehemu F. ili wajaliwe raha ya milele pamoja na watakatifu wako. Ee Bwana. Ee Mungu uliye mtakatifu na asili ya utakatifu, uyapokee maombi yetu tunayokutolea. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA SIKUKUU ZA WATAKATIFU Ee Mungu unayetuita sisi sote kuwa watakatifu, (kwa maombezi ya...) twakuomba: Kiitikio: Pokea ombi letu. 1. Uwajalie viongozi wote wa Kanisa roho ya umoja na utakatifu kama Kanisa lako lilivyo moja na takatifu. Ee Bwana. 2. Ili, hata miongoni mwa viongozi wasio wa dini, tupate watu wanaoishi kitakatifu kwa uchaji wao kwako, na kwa huduma zao bora kwa jamii wanazoziongoza. Ee Bwana. 3. Wabatizwa wote walioondolewa dhambi ya asili na kupewa alama ya utakatifu, waudumishe utakatifu huo kwa maisha na mifano yao bora. Ee Bwana. 4. Ili sisi sote tuijongee mara kwa mara Sakramenti ya Upatanisho, iletayo amani ya kweli ndani yetu na kati yetu na Wewe. Ee Bwana. 5. Uwajalie marehemu wetu F. raha ya milele pamoja na watakatifu wako huko mbinguni. Ee Bwana. Ee Mungu mtukufu, tunakushukuru kwa mifano mizuri ya watakatifu na, kwa maombezi yao, upokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA MISA YA MAZISHI Ndugu, iwe tunaishi au tumekufa sisi tu mali ya Bwana. Tumwombe Bwana Mungu aliye uzima na ufufuo wetu kwa ajili ya ndugu yetu F. na kwa ajili ya sisi wenyewe tulio bado safarini kuyaelekea makao ya milele. Kiitikio: Mungu wa uzima, utusikie. 1. Kwa ajili ya ndugu yetu F. uliyemwita kwako kutoka dunia hii, ili asamehewe mapungufu yake na kuuona uso wako mtukufu. Ee Bwana. 2. Ili kifo na ufufuko alivyovipata ndugu yetu F. kwa njia ya Ubatizo, vimsadie sasa kuingia katika ukamilifu wa maisha mapya ya ufufuko wa Mwanao Yesu Kristo. Ee Bwana. 3. Ili uchungu walio nao ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu F. upoozwe kabisa na ukweli huu, kwamba kifo hakivunji umoja wetu na Kristo ambaye ndanimo sisi sote tunaishi. Ee Bwana. 4. Ili Kanisa lihubiri daima juu ya ushindi wa Kristo Mfufuka dhidi ya shetani, dhambi na mauti na kuwahimiza watu wamfuase Kristo aliye uzima na ufufuo wetu. Ee Bwana. 5. Kwa ajili yetu sote tunaomwombea ndugu yetu F., ili kwa kuadhimisha Pasaka ya Bwana wetu Yesu Kristo, tufe kuhusu dhambi na tufufuke kwa maisha mapya yenye kukupendeza Wewe na jirani zetu, hasa wale wenye shida. Ee Bwana. Ee Bwana Mungu, sikia kilio cha watu wako wenye uchungu wa kifo na matumaini ya ufufuko wa wafu. Kwa njia Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA MISA ZA WAFU Ndugu wapendwa, Mungu Baba amewakabidhi watu wote kwa Mwanae Yesu Kristo wapate kupokelewa na kuokolewa katika jina lake. Tumwombe Mungu tukisema:- Kiitikio: Pokea ombi letu. 1. Kwa ajili ya marehemu wetu F. na ndugu wote walio tutangulia, ili wakishapokelewa nawe wapate raha isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana. 2. Ili kifo cha F. kiwaimarishe ndugu, jamaa na marafiki katika imani, matumaini ya ufufuko na mshikamano wa kiutu, kidugu na wa kikristo. Ee Bwana. 3. Ili viongozi wa Kanisa, wa serikali na wa taasisi mbalimbali washirikiane katika kuwahudumia watu, hasa wenye matatizo ya pekee na walio katika hatari ya kufa. Ee Bwana. 4. Kwa ajili ya sisi sote tuliopo hapa, ili tukumbuke kuwa ndugu zetu marehemu walioko tohorani daima wanahitaji wokovu kwa sala zetu kama vile za watakatifu walioko mbinguni. Ee Bwana. 5. Ili kila mmoja wetu ajiandae vema kwa siku yake ya mwisho, ambapo atapaswa kutolea hesabu ya maisha yake yote ya hapa duniani mbele yako Mungu, hakimu mwenye huruma, haki na upendo. Ee Bwana. Ee Mungu uliyetuweka hapa duniani ili siku moja tufike kwako na kukuona uso kwa uso, upokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA MAAFA AU JANGA LOLOTE Ee Mungu, tukiwa tumejawa huzuni, mahangaiko na majonzi kufuatia maafa yaliyo tupata (janga lililo), twaja mbele yako tukiomboleza na kuomba msaada wako tukisema:- Kiitikio: Kwa huruma yako, utuokoe. 1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa moyo na ari ya kuwaimarisha waamini wao, katika imani ya uwepo wako Mungu mwenye huruma kati ya watu wako, hata katika matatizo kama haya yaliyotupata. Ee Bwana. 2. Viongozi wetu wa serikali na wa taasisi zetu wasisite wala wasichoke kuungana na jamii nzima iliyoathirika na maafa haya (na janga hili) katika kutafuta uwezekano wa kuturudishia amani na utulivu. Ee Bwana. 3. Kila mmoja wetu adumu katika imani na matumaini kwa Mungu mwenye huruma na upendo, na ajitahidi kutoa mchango wa hali na mali, ili kuirejesha hali njema ya maisha yaliyoathirika na maafa haya (na janga hili). Ee Bwana. 4. Wale wote walioathirika kwa namna ya pekee na maafa haya (na janga hili) wajikabidhi kwa imani mikononi Mwako, Mungu, wapate nguvu na saburi ya kuyavumilia mateso haya ya kupita. Ee Bwana. 5. Ili ndugu zetu marehemu waliofariki dunia (katika maafa haya/ janga hili) wasamehewe dhambi zao na kujaliwa makao ya kudumu milele huko mbinguni. Ee Bwana. Ee Mungu uliye kati yetu wakati wa raha na wakati wa taabu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA KUMSHUKURU MUNGU Ee Mungu mwema na Mpaji wa vyote, tunakutolea sala ya shukrani tukisema:- Kiitikio: Upokee shukrani zetu. 1. Kwa kuwa, kwa neema yako, Askofu wetu F. na Mapadre wetu wanazidi kuliongoza Kanisa lako, kuihubiri Injili na kutolea sadaka ya wokovu wa dunia. Ee Bwana. 2. Kwa kuwa viongozi wetu wa serikali na wa jumuiya zetu wanautambua uwepo wako na wanajitahidi kulihudumia taifa na jamii kwa upendo. Ee Bwana. 3. Kwa kuwa umetujalia uhai, marafiki, majirani, maliasili na vipaji vyenye kutuletea mafanikio na matumaini ya kuanza maisha mapya yenye fanaka. Ee Bwana. 4. Kwa kuwa unawaita watu wengi na kuwateua waishi miito mitakatifu ya ndoa, ukatekista, utawa na upadre wapate kulitakatifuza Kanisa lako. Ee Bwana. 5. Kwa kuwa ndugu zetu marehemu wanaombewa msamaha wa dhambi na kupewa uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana. Ee Mungu, shukrani zetu na ziwe maungamo ya unyonge wetu mbele yako, na ya ukuu na uweza wako, Mungu mkarimu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KUOMBA HALI NZURI YA HEWA Ndugu, Mungu ametuumba sisi na vitu vyote vya ulimwengu na akapanga majira mbalimbali. Kwa vile hali ya hewa inazidi kuwa mbaya, tumwombe Mungu tukisema. Kiitikio: Mungu wa huruma, utusikie. 1. Utujalie hali nzuri ya hewa kwa mimea na mifugo yetu, ili kazi tulizozifanya zisipotee bure, bali zizae matunda tunayoyatamani siku zote. Ee Bwana. 2. Ili, hali hii inayotishia pia uhai wetu ikishaondolewa, tuweze kupata mazao mazuri yatakayotupatia nguvu ya kuendelea kukutumikia vema. Ee Bwana. 3. Utusamehe kosa la uharibifu wa mazingira linalochangia uwepo wa hali mbaya ya hewa, na utupe ari ya kuonyana ili tuitunze vema dunia uliyotukabidhi. Ee Bwana. 4. Ili tujaliwe kuepukana na njaa na kukingwa na magonjwa na hatari zote zitokanazo na hali hii mbaya ya hewa. Ee Bwana. 5. Ili, tukishapata mazao ya kutosha, tuweze kujiwekea akiba, kuwasaidia pia wenzetu wenye shida na kujipatia mahitaji mengine ya kimwili na kiroho. Ee Bwana. Ee Mungu uliyeufanya udhaifu wetu kuwa dawa yetu, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:SHUKRANI KWA MAVUNO Ee Mungu, kwa kuwa tunatambua kuwa mema yote tuliyonayo yatoka kwako, na ni fahari yako kubwa kutusaidia sisi wanadamu kwa neema yako, tunakushukuru na kukutukuza tukisema.- Kiitikio: Utukuzwe, Ee Mungu. 1. Kwa kuwa umetupatia mazao mengi na mazuri katika msimu huu wa mavuno, ingawa hatustahili. 2. Kwa kuwa ulitujalia hali nzuri ya hewa na yenye kufaa kwa ustawi wa mimea yetu mashambani na mifugo tuliyonayo. 3. Kwa kuwa umetupatia uhai, afya na nguvu tupate kuvitawala viumbe vyote vya ulimwengu badala yako, na kuzaa matunda yenye kukupendeza. 4. Kwa kuwa shukrani zetu kwako, Ee Mungu, hazikuzidishii kitu, bali zatufaa sisi wenyewe kupata wokovu. 5. Kwa kuwa watusamehe makosa yetu na kutujalia neema mbalimbali, tupate kuuona wema wako wa kila siku katika kuishi, kujimudu na kuwa na uhai ndani yako. Ee Mungu, upokee sifa hii ambayo ni paji lako tunalokurudishia kwa shukrani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KATIKA IBADA YA WATOTO Ee Mungu unayewapenda na kuwabariki watoto, twakuomba:- Kiitikio: Twakuomba utusikie. 1. Upokee shukrani zetu kwa kutupatia Mapadre na Makatekista wanaotufundisha neno lako. Ee Bwana. 2. Utujalie heshima na utii kwa wazazi, walimu, walezi na wakubwa wetu wote. Ee Bwana. 3. Uwabariki wote wanaotusaidia kimwili na kiroho, na wote wanaotetea haki za watoto. Ee Bwana. 4. Utujalie adabu njema, nidhamu nzuri na bidii katika kazi na masomo, tupate sifa nzuri na maisha mema. Ee Bwana. 5. Utuepushe na kila hatari, utujalie upendo wa kidugu na ushirikiano katika kutenda mema. Ee Bwana. Ee Mungu Baba, Mwanao Yesu Kristo alisema: “Waacheni watoto wadogo waje kwangu.” Uipokee sala ya watoto wako. Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.
MAOMBI:KUWAOMBEA WAGONJWA Ee Mungu mwenye nguvu na uweza wa kuponya mwili na roho, tukiwa wanyonge na dhaifu, twaja mbele yako kwa matumaini ya kupata msaada na huruma yako tukisema:- Kiitikio: Upokee ombi letu. 1. Uwajalie viongozi wetu wa Kanisa nguvu na afya, wapate kuwahudumia kondoo wao wenye shida, kwa niaba ya Kristo Mwanao aliye tabibu wa mwili na roho. Ee Bwana. 2. Viongozi wa serikali na taasisi husika, watoe huduma zote muhimu na za haki kwa madaktari na waganga wetu, ili wapate kutuhudumia kwa moyo mkunjufu. Ee Bwana. 3. Ubariki juhudi za madaktari na waganga wetu za kuwatibu wagonjwa, na uwajalie kuzitatua kero zao za kikazi kwa njia za haki, amani, upendo na saburi. Ee Bwana. 4. Wote wanaowatunza na kuwahudumia wagonjwa, wajaliwe uvumilivu, upole, huruma na upendo kwa wagonjwa wetu. Ee Bwana. 5. Wagonjwa wetu wawe na imani katika uwezo wako wa kuponya kwa njia ya matabibu, wafuate maelekezo yao kiaminifu na wajaliwe uvumilivu katika mateso yao. Ee Bwana. Ee Mungu mwenye huruma na Mponyaji, usikie sala yetu ili wagonjwa wetu wapate afya na nguvu ya kukutumikia Wewe na jirani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.