JANUARI 4 KIPINDI CHA NOEL
MASOMO
SOMO 1: 1Yn3:7-10
Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye
dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu
alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa
sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.
Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani
na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1,7-9
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
2. Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi, Milima na iimbe pamoja kwa furaha. (K)
3. Mbele za Bwana; Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa adili. (K)
SHANGILIO: Yn.1:14,12
Aleluya, aleluya,
Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; Wote waliompokea
aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya.
INJILI: Yn.1:35-42
Siku ile, Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea,
akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu.
Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu),
unakaa wapi? Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile.
Nayo ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia
Yohana na kumfuata Yesu. Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona
Masihi (maana yake, Kristo). Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni,
mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).
--------------
--------------
MAOMBI
Yesu Kristo Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili azivunje kazi za ibilisi. Tumwombe Mungu ili sisi wafuasi wa
Mwanae tulioachiwa kazi hiyo tujaliwe neema zake:
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Baba Mtakatifu F. na viongozi wote wa Kanisa wajaliwe bidii ya daima katika
kazi ya kumpeleka Mwanao kwa watu, wapate kumjua, kumpenda na kumtumikia.
2. Utuepushe sisi sote na mambo yaliyo kinyume cha haki, ili daima tutende yale yakupendezayo wewe.
3. Uwaite vijana wengi, wavulana na wasichana, wenye kujitolea kwa ajili ya kulihudumia Kanisa lako.
4. Marehemu wetu wote wajaliwe kuketi pamoja na Yesu Kristo Mwanao huko mbinguni.
Ee Baba uliye kimbilio la wote wakutafutao, Mwanao aliwapokea wafuasi waliomwendea kwa imani na matumaini
ya kupata msaada. Utupokee sisi na maombi yetu kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.