JAN.07 au JUMATATU BAADA YA EPIFANIA
MASOMO
Somo: 1 1Yoh.3:22-4:6
Wapenzi: Lolote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo
machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana
sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake,
kwa huyo Roho aliyetupa. Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na
Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho
ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu. Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani
na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani.
Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu; nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko
yeye aliye katika dunia. Hao ni wa dunia; kwa hiyo wanena ya dunia na dunia huwasikia. Sisi twatokana na
Mungu. Yeye amjuaye Mungu atusikia; yeye asiyetokana na Mungu hatusikii. Katika hili twamjua Roho wa kweli,
na roho ya upotevu.
Wimbo wa Katikati Zab.2:7-8,10-11 (K)8a
1. Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia,
Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako,
Na miisho ya dunia kuwa milki yako.
(K) Nitakupa mataifa kuwa urithi wako.
2. Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili,
Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe.
Mtumikieni Bwana kwa kicho;
Shangilieni kwa kutetemeka. (K)
SHANGILIO: Mt.4:16
Aleluya, aleluya,
Watu wale waliokaa katika giza wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa
mauti mwanga umewazukia.
Aleluya
INJILI: Mt.4:12-17,23-25
Siku ile, Yesu aliposikia ya kwamba Yohane amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya; akatoka Nazareti,
akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali: ili litimie neno lililonenwa
na nabii Isaya, akisema, Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani,
Galilaya ya mataifa, Watu wale waliokaa katika giza. Wameona mwanga mkuu, nao waliokaa katika nchi na
uvuli wa mauti mwanga umewazukia. Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana
ufalme wa mbinguni umekaribia. Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi
yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu. Na habari
zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na
mteso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya. Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya,
na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mungu husikiliza maombi yetu tuombayo daima.
Lakini mara nyingi sisi twamlipa mabaya kwa kutenda
yasiyopendeza machoni pake. Tumwombe Bwana Mungu
tukisema:
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umuimarishe Askofu wetu (F.) katika imani,
matumaini na mapendo; na utujalie sisi sote hekima
ya kuwatambua na kuwakataa kwa moyo mmoja
manabii wa uwongo.
2. Utudumishe katika kuishika amri ya kuliamini jina la
Mwana wako Yesu Kristo na kupendana sisi kwa sisi.
3. Uwaamshie moyo wa toba wote wasiolikiri jina lako
wapate kutubu na kuiamini Injili.
4. Utuongezee moyo wa huruma kwa wagonjwa,
walemavu na maskini kama alivyofanya Mwanao;
na uwapokee kwako ndugu zetu marehemu.
Utukirimie hayo, Ee Bwana Mungu, kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.