JAN.08 au JUMANNE BAADA YA EPIFANIA
MASOMO

Somo: 1 1Yoh.4:7-10
Wapenzi, tupendani; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.

Wimbo wa Katikati Zab.72:1-2,3-4,7-8 (K)11
1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

(K) Mataifa yote ya dunia watakusujudia, Ee Bwana

2. Milima itawazalia watu amani,
Na vilima navyo kwa haki.
Atawahukumu walioonewa wa watu,
Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea. (K)

3. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa Amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. (K)

SHANGILIO:
Aleluya, aleluya,
Naye Yesu alikuwa akihubiri Habari njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.
Aleluya

INJILI: Mk.6:34-44
Siku ile, Yesu aliona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi. Hata zilipopita saa nyingi za mchana, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na sasa kunakuchwa; uwaage watu hawa, ili waende zao mashambani na vijijini kandokando, wakajinunulie chakula. Akajibu, akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakamwambia, Je! Twende tukanunue mikate ya dinari mia mbili ili tuwape kula? Akawaambia, Mnayo mikate mingapi? Nendeni mkatazame. Walipokwisha kujua wakasema, Mitano, na samaki wawili. Akawaagiza wawaketishe wote, vikao vikao, penye majani mabichi. Wakaketi safu safu, hapa mia hapa hamsini. Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote. Wakala wote wakashiba. Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia. Na walioila ile mikate wapata elfu tano wanaume.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu aliwahurumia makutano waliokuwa kama kondoo wasio na mchungaji, akawafundisha na kuwalisha. Tumwombe ili, kwa huruma yake, tujaliwe mahitaji yetu ya kimwili na kiroho.

Kiitikio: Bwana utusikie, Bwana utusikilize.

1. Utuongezee watenda kazi katika shamba lako ili kondoo wako wasitindikiwe huduma zao za kimwili na kiroho.
2. Viongozi wa serikali waangaziwe mbinu mpya za kutatua matatizo ya raia wao, ili upendo wao udhihirike katika matendo yao mema.

3. Utuzidishie sisi sote hamu ya kuishiriki Ekaristi Takatifu, ambayo ni Karamu yako ya mbinguni.

4. Dhamiri zetu zitukumbushe daima kusali kabla na baada ya chakula; na hata wakati wa matukio muhimu, kama ishara ya kukutegemea wewe, kama alivyofanya Mwanao Yesu Kristo.

Ee Baba Mwema, huruma na upendo wa Mwanao Yesu Kristo kwa wahitaji vitufanye nasi wahudumu wa ndugu zetu wenye shida, ili nao waonje uwepo wake ndani yetu. Kwa huyo Kristo Bwana wetu. Amina.