JAN.09 au JUMATANO BAADA YA EPIFANIA
MASOMO

Somo: 1 1Yon 4:11-18
Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. Na sisi tumeona na kushuhudia ya kuwa Baba amemtuma Mwana kuwa Mwokozi wa ulimwengu. Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu. Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lilio kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.

Wimbo wa Katikati Zab.72:1-2,10,12-13 (K)11
1. Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako.
Na mwana wa mfalme haki yako.
Atawaamua watu wako kwa haki,
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.

(K) Mataifa yote ya ulimwengu, watakusujudia, ee Bwana.

2. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,
Na wingi wa Amani hata mwezi utakapokoma
Na awe na enzi toka bahari hata bahari,
Toka mto hata miisho ya dunia. (K)

3. Wafalme wa Tarshisi na visiwa walete kodi,
Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie. (K)

4. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi
Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa. (K)

SHANGILIO: Lk.4:18-19
Aleluya, aleluya,
Bwana amenituma kuwahubiri maskini habari njema, na kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao.
Aleluya

INJILI: Mk.6:45-52
Baada ya watu elfu tano kula na kushiba, mara Yesu aliwalazimisha wanafunzi wake wapande mashuani, watangulie kwenda ng’ambo hata Bethsaidia, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano. Hata alipokwisha kuagana nao akaenda zake mlimani kuomba. Na kulipokuwa jioni mashua ilikuwa katikati ya bahari, na yeye yupo peke yake katika nchi kavu. Akawaona wakitaabika kwa kuvuta makasia, kwa maana upepo ulikuwa wa mbisho; hata ilipopata kama zamu ya nne ya usiku akawaendea, akitembea juu ya bahari; akataka kuwapita. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe, kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope. Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao; kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu wapenzi, tunaaswa kuwa tusiwe na hofu kumwomba Mungu katika shida zetu, kwa sababu yeye anatupenda, yupo tayari na anao uwezo wa kutusaidia kwa lolote na katika hali yoyote. Basi, na tumwombe.

Kiitikio: Kwa huruma yako utusikie.

1. Utuimarishe katika imani juu ya uwezo wako wa kimungu, ili tukutegemee siku zote, hata katika dhoruba za maisha yetu.

2. Utubidishe katika kukupenda na kuliamini neno lako, ili ukae ndani yetu na sisi ndani yako.

3. Utuondolee hofu, fadhaa au unyonge katika utumishi wako mtakatifu; na uwe pamoja nasi katika safari yetu ya kukujia wewe.

4. Uwakinge marehemu wetu na adhabu, ili wafike kwako mbinguni na kukuona milele.

Ee Bwana, kwa kuwa Kanisa lako ni kama chombo chetu cha usafiri wa kukujia wewe, utujalie furaha ya kubaki humo na utufikishe salama nyumbani kwako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.