JAN.11 au IJUMAA BAADA YA EPIFANIA
MASOMO

Somo: 1 1Yoh.5:5-6,8-13
Wapenzi: Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu? Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika damu. Kwa maana wako watatu washuhudiao (mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja. Kisha wako watatu washuhudiao duniani), Roho, na maji, na damu; na watatu hawa hupatana kwa habari moja. Tukiupokea ushuhuda wa wanadamu, ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi; kwa maana ushuhuda wa Mungu ndio huu, kwamba amemshuhudia Mwanawe. Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.

Wimbo wa Katikati Zab.147:12-15,19-20 (K)12
1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
Maana ameyakaza mapigo ya malango yako,
Amewabariki wanao ndani yako.

(K) Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

2. Ndiye afanyaye amani mipakani mwako,
Akushibishaye kwa unono wa ngano.
Huipeleka amri yake juu ya nchi;
Neno lake lapiga mbio sana. (K)

3. Humhubiri Yakobo neno lake,
Na Israeli amri zake na hukumu zake.
Hakulitendea taifa lolote mambo kama hayo,
Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

SHANGILIO: 1Tim.3:16
Aleluya, aleluya,
Sifa kwako, Ee Kristo, uliyehubiriwa katika mataifa; Sifa kwako, Ee Kristo, aliyeaminiwa katika ulimwengu.
Aleluya

INJILI: Lk.5:12-16
Ikawa Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ile, tazama, palikuwa na mtu amejaa ukoma; naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa. Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukamwondoka. Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajioneshe kwa kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe ushuhuda kwao. Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao. Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, mara nyingi tunashindwa kumpokea Mwanao Yesu Kristo na hivi kuishi kinyume cha imani aliyotufundisha kwa sababu ya ukoma wa roho zetu. Tunapokumbuka hayo, tunakuomba:

Kiitikio: Pokea ombi letu.

1. Makasisi wetu wote watumie sawasawa vipawa walivyojaliwa katika kumshuhudia Mwanao, kama Wewe ulivyofanya.

2. Wakristo wote tuoneshe imani yetu kwa Mwanao kwa maneno na matendo, ili ushuhuda ulio ndani yetu upate kuzaa matunda.

3. Uunyoshe mkono wako juu ya kila mmoja wetu, ili tubandukane na kiini cha matatizo yanayotusibu mwilini na rohoni.

4. Uwatakase marehemu wetu na kuwaweka mahali pema huko mbinguni.

Tunakuomba hayo kwa unyenyekevu, Ee Mungu, kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.