JAN.12 au JUMAMOSI BAADA YA EPIFANIA
MASOMO
Somo: 1 1Yn.5:14-21
Wapenzi: Huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama
tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. Mtu akimwona ndugu yake
anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti.
Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi
iko isiyo ya mauti. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu
hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu.
Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi
tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima
wa milele. Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.
Wimbo wa Katikati Zab.149:1-6, 9 (K)14
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake.
2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
3. Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Na upanga mkali kuwili mikononi mwao.
Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa;
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. (K)
SHANGILIO: Lk.7:16
Aleluya, aleluya,
Nabii mkuu ametokea kwetu; Na Mungu amewaangalia watu wote.
Aleluya
INJILI: Yn.3:22-30
Siku ile, Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza.
Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu
wakamwendea, wakabatizwa. Maana Yohana alikuwa hajatiwa gerezani. Basi palitokea mashindano ya wanafunzi wa
Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso. Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabi, yeye aliyekuwa pamoja nawe
ng'ambo ya Yordani, yeye uliyemshuhudia, tazama, huyo anabatiza na watu wote wanamwendea. Yohana akajibu,
akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya
kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini
rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha
yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Mtume Yohane anatuthibitishia kuwa tukimwomba
Mungu kitu chochote sawasawa na mapenzi yake,
atusikia. Tukiwa na imani hiyo tuombe tukisema:
Kiitikio: Mungu wa huruma utusikie.
1. Utujalie sisi sote ari ya kupokea Sakramenti ya
Upatanisho, kila tunapohitaji kujipatanisha nawe na
jirani zetu.
2. Uzilinde nafsi zetu na sanamu ili tuwe daima ndani
ya Mwanao Yesu Kristo na kumwabudu yeye tu, aliye
Mungu sawa na Baba na Roho Mtakatifu.
3. Uamshe hamu ya Ubatizo kwa wakatekumeni, ili
waipate furaha ya kuwa pamoja na Yesu, Bwana arusi
na Mkombozi wetu.
4. Uwatakase marehemu wetu na dhambi zao, ili furaha
ya Mwanao itimizwe ndani yao.
Ee Mungu, Yohane Mbatizaji alijidhili na kujipunguza, ili
Mwanao azidi kuvuma. Utujalie unyenyekevu maishani
mwetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.