Des 30 OKTAVA YA NOELI
MASOMO
SOMO 1: 1Yoh.2:12-17
Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake. Nawaandikia ninyi,
akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nawaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mmemshinda yule mwovu.
Nimewaandikia ninyi, watoto, kwa sababu mmemjua Baba. Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye
tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda
yule mwovu. Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali
vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:7-10
1. Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu,
Mpeni Bwana utukufu na nguvu,
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake. (K)
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.
2. Leteni sadaka mkaziingie nyua zake,
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu,
Tetemekeni mbele zake, nchi yote. (K)
3. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
Atawahukumu watu kwa adili. (K)
Shangilio
Aleluya, aleluya
Siku takatifu imetung’aria: Enyi mataifa njoni mkamwabudu Bwana: Kwa sababu mwanga mkubwa umeshuka duniani.
Aleluya.
INJILI: Lk.2:36-40
Siku ile palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka
mingi alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne;
haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru
Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake. Basi, walipokwisha
kuyatimiza yote kama yaliyoagizwa katika sheria ya Bwana, walirejea Galilaya, mpaka mjini kwao, Nazareti. Yule
mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, neno la Mungu limeandikwa kwa watu wa rika zote bila kujali kabila, taifa au rangi. Maadamu
sisi sote tu wakosefu na twahitaji huruma na msaada wa Mungu, tuombe:
Kiitikio: Bwana utusikie, Bwana utusikilize.
1. Utuepushe sisi sote na tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima, ili tukupende wewe tu.
2. Kwa kuzaliwa kwa Mwanao, utusamehe dhambi zetu tupate kukujua wewe zaidi na kumshinda yule mwovu.
3. Utujalie moyo wa ibada, shukrani na unabii kama alivyofanya Ana binti Fanueli, ili wote wanaoutarajia
ukombozi katika dunia hii wapate kukujua wewe.
4. Wote waliozaliwa upya kwa Ubatizo Siku ya Noeli wazidi kukua katika imani, waongezewe nguvu na
kujazwa hekima, na neema yako iwe juu yao.
Ee Bwana Mungu, twatambua kuwa kuzaliwa kwa Mwanao ni ishara wazi ya mapendo yako kwetu. Utujalie
kudumu katika upendo wako siku zote. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.