Des 31 OKTAVA YA NOELI
MASOMO
SOMO 1: 1Yoh.2:18-21
Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo
wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa
wa kwetu. Maana kama wangalikuwa wa kwetu, wangalikaa pamoja nasi. Lakini walitoka ili wafunuliwe kwamba si
wote wa kwetu. Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote. Sikuwaandikia ninyi kwa sababu
hamwijui iliyo kweli, bali kwa sababu mwaijua, tena kwamba hapana uongo wowote utokao katika hiyo kweli.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.96:1-2,11-13
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake,
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. (K)
(K) Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie.
2. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie,
Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo,
Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
Mbele za Bwana, kwa maana anakuja,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi. (K)
3. Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa uaminifu wake. (K)
Shangilio: Ebr.1:1-2
Aleluya, aleluya
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi na kwa namna nyingi na baba zetu kwa kinywa cha manabii,
siku hizi zilizo za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.
INJILI: Yn.1:1-18
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa
Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika. Ndani yake ndimo
ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza. Palitokea
mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote
wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi,
amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako,
wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo
wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi
ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona
utukufu wake, utukufu kama wa mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Yohane alimshuhudia, akapaza
sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa
maana alikuwa kabla yangu. Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema. Kwa kuwa
torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona
Mungu wakati wowote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.
--------------
--------------
MAOMBI tazama pia AU
Ndugu wapendwa, Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu tupate kumjua yeye na Baba aliyemtuma. Tuombe, ili
tuweze kuishi katika nuru halisi aliyotuletea.
Kiitikio: Utuhurumie na utusikilize.
1. Wote waliopakwa mafuta kwa Sakramenti mbalimbali wawe mstari wa mbele, katika kujilinda dhidi ya
wapinga Kristo ambao ni wengi. Ee Bwana.
2. Sikukuu ya Noeli iamshe ndani ya familia zetu za kikristo hali ya umoja na amani, itokayo katika
mapendo ya kweli. Ee Bwana.
3. Uwajalie watu wote duniani kumtambua Mwanao kuwa ndiye Nuru halisi na, wakiisha kumwamini, wapate
kumpokea na kukaa pamoja naye. Ee Bwana.
4. Uwapokee marehemu wetu wapate kuuona utukufu wa Mwanao. Ee Bwana.
Ee Bwana Mungu, kuzaliwa kwa Mwanao kumetuletea neema na kweli. Utujalie kuzitumia neema hizo na kudumu
katika ukweli huo, ili siku moja tupate kukuona wewe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
AU
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Yesu alitwaa ubinadamu wetu na akakaa kwetu tupate kumjua yeye na Baba aliyemtuma. Huku
tukimshukuru kwa neema alizotujalia katika mwaka huu tunaoumaliza leo, tumwombe ili, katika mwaka huo
mpya tutakaouanza, tuweze kuishi katika nuru halisi aliyotuletea.
1. Wote waliopakwa mafuta kwa Sakramenti mbalimbali wawe mstari wa mbele, katika kujilinda dhidi ya
wapinga Kristo ambao ni wengi.
2. Sikukuu ya Noeli iamshe ndani ya familia zetu za kikristo hali ya umoja na amani, itokayo katika
mapendo ya kweli.
3. Uwajalie watu wote duniani kumtambua Mwanao kuwa ndiye Nuru halisi na, wakishamwamini, wampokee
na kukaa pamoja naye.
4. Upokee shukrani tunazokutolea kwa neema nyingi ulizotujalia mwaka huu tunaoumaliza leo; na utujalie
tena kuuona mwaka mpya wenye kheri na fanaka tele.
5. Uwapokee marehemu wetu wapate kuuona utukufu wa Mwanao huko mbinguni.
Ee Bwana Mungu, kuzaliwa kwa Mwanao kumetuletea neema na kweli. Utujalie kuzitumia neema hizo na
kudumu katika ukweli huo, ili siku moja tupate kukuona wewe. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.