ALHAMISI JUMA 1 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.3:7-14
Roho Mtakatifu asema: Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha,
Siku ya kujaribiwa katika jangwa, Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini.
Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Siku zote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu;
Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu. Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo
mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja
wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na
mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;
WIMBO WA KATIKATI: Zab.95:6-11 (K)8
1. Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
2. Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
3. Miaka arobaini nalihuzunika na kizazi kile,
Nikasema, Hao ni watu waliopotoka mioyo,
Hawakuzijua njia zangu.
Nikaapa kwa hasira yangu Wasiingie rahani mwangu.(K)
SHANGILIO: Mt.11:25
Aleluya, aleluya!
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima
na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya!
INJILI: Mk.1:40-45
Siku ile mtu mwenye ukoma alikuja kwa Yesu, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka,
waweza kunitakasa. Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.
Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika. Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia,
Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajioneshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru
Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao. Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi,
na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali
pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu zangu, tunahitaji msaada wa Mungu aliye hai
tupate kutimiza mapenzi yake kwa moyo mnyofu na
imani thabiti. Kwa hiyo tuombe neema yake.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwaongezee Baba Mtakatifu, Maaskofu, na wakleri
wetu wote neema ya kulitangaza neno lako kwa
ufasaha na kuadhimisha Ekaristi Takatifu kwa uchaji.
Ee Bwana.
2. Uilainishe mioyo migumu ya watawala wasiopenda
kuzijua njia zako. Ee Bwana.
3. Uliepushe Kanisa lako na dhuluma ya aina yoyote;
na uliimarishe katika imani, matumaini na mapendo
kwako katika taabu na raha. Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu ujasiri wa kuonyana, wala
tusiendekeze ugumu kwa udanganyifu wa dhambi.
Ee Bwana.
5. Uwakaribishe ndugu zetu marehemu kwako mbinguni.
Ee Bwana.
Ee Mungu, Wewe upo tayari kuwatakasa wote wanaokujia
na kuomba huruma yako. Uyapokee maombi yetu hata
yale tusiyothubutu kuomba. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.