ALHAMISI JUMA 22 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.3:18-23
Mtu asijidanganye mwenyewe; kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia
hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele
za Mungu. Kwa maana imeandikwa, yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao. Na tena,
Bwana anayafahamu mawazo ya wenye hekima ya kwamba ni Paulo, au Apolo, au Kefa; au dunia, au
uzima, au mauti; au vile vilivyopo sasa, au vile vitakavyokuwapo; vyote ni vyenu; nanyi ni wa
Kristo, na Kristo ni wa Mungu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6(K)1
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana.
2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
Wala hakuapa kwa hila. (K)
3. Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)
SHANGILIO: 1Thes.2:13
Aleluya, aleluya!
Lipokeeni neno la Mungu, siyo kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu.
Aleluya!
INJILI: Lk.5:1-11
Makutano walipomsonga Yesu wakilisikiliza neno la Mungu, yeye alikuwa amesimama kando ya
ziwa la Genesareti, akaona vyombo viwili vimekaa kando ya ziwa, lakini wavuvi wametoka,
wanaosha nyavu zao. Akaingia katika chombo kimoja, ndicho chake Simoni, akamtaka akipeleke
kidogo na pwani. Akaketi, akawafundisha makutano ali chomboni. Hata alipokwisha kunena,
alimwambia Simoni, Tweka mpaka kilindini, mkashushe nyavu zenu mvue samaki. Simony akajibu
akamwambia, Bwana mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa
neno lako nitazishusha nyavu. Basi, walipofanya hivyo walipata samaki wengi mno, nyavu zao
zikaanza kukatika; wakawapungia mikono washirika wao waliokuwa katika chombo cha pili, waje
kuwasaidia; wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, hata vikataka kuzama. Simoni Petro alipona
hayo, alianguka magotini pa yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi,
Bwana. Maana alishikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye, kwa sababu ya wingi
wa samaki waliopata; na kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa washirika
wa Simoni. Yesu akamwambia Simoni, Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu. Hata walipokwisha
kuviegesha pwani vyombo vyao, wakaacha vyote wakamfuata.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu wapendwa, Mungu Baba alituingiza katika ufalme
wa Mwana wa pendo lake kutoka nguvu za giza. Na hivi
tunamshukuru tukisema.
Kiitikio: Upokee shukrani zetu.
1. Kwa kuwa umelipatia Kanisa lako viongozi wa kuiendeleza
kazi ya Mwanao, ili tujipatie ukombozi, yaani msamaha wa
dhambi. Ee Bwana.
2. Kwa kuwa umeijalia nchi yetu watawala wenye
hekima na upendo na wanaohimiza haki, amani na
ushirikiano. Ee Bwana.
3. Kwa kuwa kwa kupewa mahitaji yao ya kimwili na
kiroho, watu wako wanapata fursa ya kuutambua ukuu
na utakatifu wako na kuongoka. Ee Bwana.
4. Kwa kuwa umetuachia Ekaristi Takatifu inayotupatia
saburi, uvumilivu, maarifa, furaha, amani na umoja. Ee Bwana.
5. Kwa kuwa ndugu zetu marehemu wanaombewa msamaha
na kupewa uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, uwe radhi kuzipokea hizi shukrani zetu
pamoja na nia zingine tulizonazo ambazo hatukuzitaja.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.