ALHAMISI JUMA 23 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO 1Kor.8:1-7,11-13
Twajua ya kuwa sisi sote tuna ujuzi. Ujuzi huleta majivuno, bali upendo hujenga. Mtu akidhani
ya kuwa anajua neno, hajui neno lolote bado, kama impasavyo kujua. Lakini mtu akimpenda Mungu,
huyo amejulikana naye. Basi kwa habari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua
yakuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na yakuwa hakuna Mungu ila mmoja tu. Kwa maana
ijapokuwa wako waitwao miungu, ama mbinguni ama duniani, kama vile walivyoko miungu mingi
na mabwana wengi; lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka
kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwapo,
na sisi kwa yeye huyo. Bali ujuzi huu haumo ndani ya watu wote; ila wengine kwa kuizoelea ile
sanamu hata sasa hula kana kwamba ni kitu kilichotolewa sadaka kwa sanamu; na dhamiri zao, kwa
kuwa dhaifu, hunajisika. Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa ujuzi wako, naye ni ndugu ambaye
Kristo alikufa kwa ajili yake. Hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuitia jeraha dhamiri
iliyo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo. Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula
nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.139:1-3,13-14,23-24(K)24
1. Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu wazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze, Bwana, katika njia ya milele.
2. Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha. (K)
3. Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu,
Unijaribu, uyajue mawazo yangu;
Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu,
Ukaniongoze katika njia ya milele. (K)
SHANGILIO: Zab.147:12,15
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:27-38
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema
wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao
wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang’anyaye joho yako, usimzuilie
na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang’anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Na kama
mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao
ninyi, mwaonesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi
mkiwatendea mema wale wawatendao mema, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya
vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonesha fadhili gani?
Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui
zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi;
nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi,
iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu,
nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha
kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu.
Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, uliyetuhimiza kwa namna ya pekee kujivika
upendo ulio kifungo cha ukamilifu. Twakuomba:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Ili Baba Mtakatifu wetu F.,
Askofu wetu F. na
Mapadre wote, waendelee kuadhimisha Sadaka ya
Ekaristi Takatifu, ishara ya upendo ambao Mwanao
Yesu Kristo aliuonesha kwetu mpaka kufa msalabani. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wawaongoze watu kwa
tahadhari, kwani hakuna Mungu ila Wewe tu, uliye
Baba na mwumba wa vyote; nasi tunaishi kwako. Ee Bwana.
3. Ili tupate kuwapenda, kuwaombea na kuwabariki hata
adui zetu na wote wanaotuchukia, wapate kujirudi,
kutubu na kutenda mema. Ee Bwana.
4. Ili sisi sote tunaomfuasa Kristo tuweze kupendana,
kufundishana, kuonyana, kusaidiana na kuhurumiana
kama Wewe ulivyotuhurumia. Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu wapewe huruma yako na
kushirikishwa utakatifu wako milele. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tuwapimie wenzetu kipimo kizuri,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.