ALHAMISI JUMA 24 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: 1Kor.15:1-11
Ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo
mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa
mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzao yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, yakuwa
Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na yakuwa alizikwa;
na yakuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na yakuwa alimtokea Kefa; tena
na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi
hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa
watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake. Maana mimi ni mdogo
katika mitume, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu naliliudhi kanisa la Mungu. Lakini kwa
neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi
sana kufanya kazi kupita wao wote; wala si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami. Basi, kama
ni mimi, kama ni wale, ndivyo tuhubirivyo, na ndivyo mlivyoamini.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.118:1-2,15-17,28(K)1
Aleluya.
1. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
2. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K)
3. Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru,
Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza. (K)
SHANGILIO: Kol.3:16,17
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote,
Mkimshukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya!
INJILI: Lk.7:36-50
Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika Yesu ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake
yule Farisayo, akaketi chakulani. Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi,
alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya
marimari yenye marhamu. Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea
machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka
yale marhamu. Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu
kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya
kwamba ni mwenye dhambi. Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema,
Mwalimu, nena. Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia
tano, na wa pili hamsini. Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika
hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi? Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe
nyingi. Akamwambia, Umeamua haki. Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke
huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi
miguu yangu; na hakuacha kunibusu sana miguu yangu. Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu
amenipaka miguu yangu marhamu. Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni
nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo. Kisha alimwambia
mwanamke, Umesamehewa dhambi zako. Ndipo wale walioketi chakulani pamoja naye walianza kusema
mioyoni mwao, Ni nani huyu hata asamehe dhambi? Akamwambia yule mwanamke, Imani yako imekuokoa,
enenda zako kwa amani.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa vile sisi sote ni watenda kazi katika
shamba la Bwana, kwa imani tumpelekee Mungu maombi
yetu.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Maaskofu na Mapadre wetu wasiache kuitumia karama
ya unabii iliyomo ndani yao, ili wawe kielelezo
kwa waamini wao katika usemi na mwenendo, katika
upendo, na katika imani na usafi. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali watoe fursa kwa waamini kukuabudu
Wewe Mungu, ili neno lako lipate kuenea na
kuziokoa nafsi za watu wako. Ee Bwana.
3. Utuongezee sisi sote imani katika ukuu wako na katika
uwezo wako wa kuponya roho na mwili. Ee Bwana.
4. Tunawaombea matajiri, ambao kwa neema ya
Mungu wamekuwa kama walivyo, ili wazitumie
karama walizopewa kwa kulisaidia Kanisa na wote
wenye shida. Ee Bwana.
5. Uziokoe roho za ndugu zetu marehemu, wapate kufika
huko mbinguni na kukusifu milele. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetupatia imani iletayo wokovu, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.