ALHAMISI JUMA 28 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Efe.1:1,3-10
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa mapenzi ya Mungu; kwa watakatifu wanaomwamini Kristo Yesu.
Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa Baraka zote za rohoni, katika
ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi
ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. Kwa kuwa alitangulia
kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na Uradhi wa mapenzi yake.
Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo,
kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, msamaha wa dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake. Naye
alituzidishia hiyo katika hekima yote na ujuzi; akiisha kutujulisha siri ya mapenzi yake, sawasawa
na Uradhi wake, alioukusudia katika yeye huyo. Yaani, kuleta madaraka ya wakati mkamilifu atavijumlisha
vitu vyote katika Kristo, vitu vya mbinguni na vitu vya duniani pia.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-6(K)2
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu,
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu. (K)
(K) Bwana ameufunua wokovu wake.
2. Bwana ameufunua wokovu wake,
Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
4. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana. (K)
SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
Neno lako ni taa ya miguu yangu, na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!
INJILI: Lk.11:47-54
Yesu aliwaambia wanasheria: Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio
waliowaua. Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea
maziara. Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao
watawaua baadhi yao na kuwafukuza, ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika
tangu kupigwa msingi wa ulimwengu; tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya
madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki. Ole wenu, enyi wanasheria,
kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.
Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi,
wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, haki ya Mungu inashuhudiwa na Torati na
Manabii. Kwa vile wote wamefanya dhambi na
kupungukiwa na utukufu wa Mungu, tuombe:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upokee Sadaka anayokutolea Askofu wetu F. na
Mapadre wote kwa niaba ya Mwanao Yesu Kristo,
ili kutupatanisha nawe katika damu yake kwa njia ya
imani. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wetu wa serikali za
kudhibiti vitendo vya uhalifu, hasa umwagaji damu
isiyo na hatia, ili tuishi kwa amani na upendo.
3. Uwakinge watu wako na umwagaji wa damu isiyo na
hatia; ili wote wakutafutao kwa moyo mnyofu wapate
fursa ya kukuabudu bila hofu. Ee Bwana.
4. Ekaristi Takatifu tunayoipokea itupe nguvu na ujasiri
wa kukuabu na kuilinda imani yetu bila kufadhaishwa
na jambo lolote. Ee Bwana.
5. Uwajalie marehemu wetu uzima mpya pamoja na
watakatifu wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetuhesabia haki kwa imani, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.