ALHAMISI JUMA 2 MAJILIO
MASOMO
SOMO 1: Isa.41:13-20
Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi
nitakusaidia. Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema Bwana,
na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria,
chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. Utawapepeta, na
upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia Bwana, utajitukuza katika
Mtakatifu wa Israeli. Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu;
mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima,
na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya
maji. Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari,
na mteashuri pamoja; ili waone, na kujua wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa Bwana ndio
uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:1,9-13
1. Ee Mungu wangu, Mfalme nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. (K)
(K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
2. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi,
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K)
3. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
Shangilio: Isa.45:8
Aleluya, aleluya,
Dondokeni, enyi mbingu toka juu, Mawingu yamwage haki; nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu.
Aleluya.
INJILI: Mt.11:11-15
Siku ile, Yesu aliwaambia makutano: Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye
mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yeye. Tangu
siku za Yohane Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. Kwa
maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohane. Na ikiwa mnataka kukubali, yeye ndiye
Eliya atakayekuja. Mwenye masikio, na asikie.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Bwana Mungu, wewe ndiwe Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wetu. Tunapongojea ujio wa Mwanao, twakuomba:
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uyabariki majitoleo ya Askofu wetu F. katika kulistawisha Jimbo letu kimwili
na kiroho na ulitimizie Kanisa lako lote ahadi yako ya kuletewa Mkombozi.
2. Ututakase ili tuwe vyombo bora vyenye kuyatenga mabaya mbali na yote yakupendezayo.
3. Uwafariji wenye njaa na kiu ya haki, ili matatizo yao yasiwatenganishe nawe, bali yawaunganishe zaidi nawe.
4. Uwapepete na kuwatawanya maadui zetu wanaotusonga katika maisha yetu ya imani, pia uwapokee na kuwaweka
mahali pema mbinguni marehemu wetu F..
Ee Baba Mwema, Mwanao amesema aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yule aliye mkuu kuliko
wote katika uzao wa wanawake. Utufanye wanyenyekevu na kutuweka miongoni mwa wateule wako. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.