ALHAMISI JUMA 2 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ebr.7:25-8:6
Yesu aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai siku zote ili awaombee. Maana
ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na
waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku,
mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe,
kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake.
Maana torati yawaweka wanadamu walio na unyonge kuwa makuhani wakuu; bali hilo neno la kiapo
kilichokuja baada ya torati limemweka Mwana, aliyekamilika hata milele. Basi, katika hayo tunayosema,
neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha
enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala
si mwanadamu. Maana kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye
awe na kitu cha kutoa. Kama angekuwa juu ya nchi, asingekuwa kuhani; maana wako watoao sadaka kama
iagizavyo sheria; watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu,
alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule
uliooneshwa katika mlima. Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe
wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.40:6-9,16 (K)7,8
1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja,
(K) Tazama nimekuja kufanya mapenzi yako, Ee Bwana.
2. Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
3. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa.
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
4. Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao.
Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe Bwana. (K)
SHANGILIO: 2Kor.5:19
Aleluya, aleluya,
Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake,
ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya.
INJILI: Mk.3:7-12
Yesu alijitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka
Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu, na Idumaya, na ng'ambo ya Yordani, na pande za Tiro na
Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea.
Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano,
wasije wakamsonga. Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate
kumgusa. Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe
ndiwe Mwana wa Mungu. Akawakataza sana, wasimdhihirishe.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, huku tukiwa na matumaini ya kuokolewa
kwa njia ya Yesu Kristo anayetuombea, tumwelekezee
Mungu shida zetu tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie makuhani wetu ule utakatifu wa Mwanao
Yesu Kristo. Ee Bwana.
2. Viongozi wasio wa dini wakumbuke kuwa nao wanapaswa
kutokuwa na uovu wala waa lolote mbele yako
na miongoni mwa watu wao na wako. Ee Bwana.
3. Utuepushe na roho ya wivu isiyopenda mafanikio
ya wengine; na utujalie urafiki wa kweli wakati wa
taabu na raha. Ee Bwana.
4. Kila mmoja wetu ajaliwe kumpokea Mwanao katika
Ekaristi Takatifu kwa moyo safi, apate kutoa huduma
bora zaidi kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Ee
Bwana.
5. Wagonjwa wote, wenye pepo, wenye misiba na marehemu
wote wakujie Wewe Mungu uliye kimbilio la
wazima na wafu. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu aliye
chakula chenye uzima wa milele. Amina.