ALHAMISI JUMA 30 LA MWAKA WA 2
MASOMO
SOMO: Efe.6:10-20
Wapenda mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu,
mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama;
bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika
ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu,
na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii
ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; zaidi ya yote mkiitwaa ngao
ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo
ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika
Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi,
nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo kwa ajili
yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.144:1-2,9-10(K)1
1. Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu,
Anifundishaye mikono yangu vita,
Vidole vyangu kupigana.
(K) Ahimidiwe Bwana, mwamba wangu.
2. Mhisani wangu na boma langu,
Ngome yangu na mwokozi wangu,
Ngao yangu niliyemkimbilia,
Huwatiisha watu wangu chini yangu. (K)
3. Ee Mungu, nitakuimbia wimbo mpya,
Kwa kinanda chenye nyuzi kumi nitakuimbia.
Awapaye wafalme wokovu,
Amwokoa Daudi, mtumishi wake, na upanga wa uovu. (K)
SHANGILIO: Zab.119:18
Aleluya, aleluya!
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya!
INJILI: Lk.13:31-35
Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine,
kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na
kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika
njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu. Ee
Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga kwa mawe waliotumwa kwako, mara ngapi nimetaka
kuwakusanya watoto wako kama vile kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake, wala
hamkutaka. Angalieni, mmeachiwa nyumba yenu! Nami nawaambia, Hamtaniona tena kamwe, hata mtakaposema,
Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa kuwa twaamini kuwa hakuna chochote
kitakachotutenga na upendo wa Mungu ulio katika
Kristo Yesu Bwana wetu, tuombe tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwalinde Wachungaji wa Kanisa lako dhidi ya wote
wenye nia mbaya na utume wao, ili waendelee
kuutangaza ukweli wa Injili yako. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali wazidi kuwa hodari na
kukutegemea Wewe, Mungu, katika uweza na
nguvu zako dhidi ya shetani na maadui wote;
wavae silaha wapate kuwapigania watu wako. Ee Bwana.
3. Wote wanaohubiriwa habari za Mwanao waongoke
na kumkiri, kwani ndiye “Mbarikiwa” ajaye kwa
jina lako. Ee Bwana.
4. Utujalie imani thabiti kwako hata katika madhulumu,
tukitumaini kuwa katika mambo hayo yote tutashinda,
kwa jina la Mwanao Yesu Kristo aliyetupenda. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wakaribishwe kwenye makao yako
ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.